Dar es Salaam. Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) Julai 3, 2024.
Nyusi atapokelewa nchini Tanzania kesho Jumanne, Julai 2 na Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam, ataambatana na mwenyewe wake katika ufunguzi wa maonyesho hayo.
Hata hivyo, taarifa iliyotolewa leo Julai mosi, 2024 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imeeleza Rais Nyusi anatarajia kuwasili nchini leo jioni Julai mosi,2024 na atafanya ziara ya kiserikali ya siku tatu.
Rais Samia na mgeni wake watashiriki mazungumzo ya pamoja yatakayojikita katika sekta ya biashara, uwekezaji, ulinzi na usalama na kisha kushuhudia uwekaji saini wa makubaliano katika sekta mbalimbali za ushirikiano.
“Ziara hii itaendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria, kidugu na kidiplomasia uliopo baina ya Tanzania na Msumbiji ambao uliasisiwa na viongozi wetu, kiongozi wa kwanza wa chama tawala cha nchi hiyo (Frelimo), Hayati Eduardo Chivambo Mondlane na Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere,” imeeleza taarifa hiyo.
Rais Nyusi ataondoka nchini Julai 4, 2024. Awali alipotoa taarifa ya ziara hiyo Jumapili, Juni 30, 2024 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Afrika Mashariki, January Makamba alisema:
“Sambamba na mazungumzo kuhusu ushirikiano, ujio wa Rais Nyusi pia unalenga kuja kuwaaga Watanzania anapohitimisha miaka 10 ya uongozi wake nchini Msumbiji.”
Makamba alisema, hatua yake ya kuwaaga Watanzania inathibitisha uimara wa ushirikiano kati ya nchi hizo, ulioasisiwa tangu enzi za ukombozi.
Rais Nyusi ameiongoza Msumbiji kwa miaka 10 hadi sasa na Oktoba mwaka huu taifa hilo linatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu wa kumpata Rais mpya.