ALIYEWAHI kuwa mwenyekiti na mfadhili wa Yanga, Yusuf Manji, alifariki dunia juzi wakati akipatiwa matibabu katika hospitali moja iliyopo Florida, Marekani alikokuwa akiishi, lakini takriban miezi miwili iliyopita alifanya mahojiano na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam na kufunguka mambo mengi.
Mahojiano ya gazeti hili na Manji yaliyolifanyika Aprili 21, mwaka huu ndiyo yaliyokuwa ya mwisho kufanya na chombo cha habari hapa nchini, ikiwa ni siku chache tangu alipohudhuria mchezo wa pili wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Yanga uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa.
Kila alipokuja Tanzania, Manji aliwasiliana na mwandishi wa makala hii na kuzungumza mambo mbalimbali huku akisisitiza yasiandikwe popote, lakini Aprili 16 akiwa nchini alimtaka mwandishi kutafuta nafasi ili aizungumzie Yanga.
Manji alipanga nafasi na kumjulisha mwandishi kukutana naye kwa ajili ya kufanya mahojiano.
Ikiwa ni siku 72 tangu mahojiano hayo yalipofanyika, Mwanaspoti linakuletea kile alichozungumza shabiki huyo kindakindaki wa Yanga na hapa akiwahusia Wananchi na watani zao, Simba mambo mbalimbali. Twende pamoja…
Katika mahojiano hayo, Manji alizungumzia misimu mitatu mibovu ya Simba ambapo imepoteza ubingwa wa Ligi Kuu Bara mbele ya Yanga akisema: “Tatizo la Simba ni mtu huyu.”
Alisema kinachoitesa Simba ni baada ya kifo cha Zacharia Hans Poppe ambaye aliwahi kuwa bosi wa kamati ya usajili wa timu hiyo na kinara wa kundi la Friends of Simba.
Tangu Hans Poppe alipofariki dunia Septemba 10, 2021, Simba imekuwa haina matokeo mazuri, huku Yanga ikionekana kulitawala soka la Tanzania baada ya kutwaa ubingwa mara zote.
Kabla ya kufariki dunia, Hans Poppe aliiongoza Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne mfululizo, huku Yanga ikionekana kuhaha kila msimu.
“Unajua wakati nikiwa Yanga, mtu pekee aliyekuwa ananipa wakati mgumu ni Hans Poppe. Huyu jamaa alikuwa anafanya kazi yake kuonesha kabisa kuwa Dabi inatakiwa kuwa na mvuto, alikuwa akizungumza na watu wanamuelewa, alinipa wakati mgumu sana.
“Hata niliposikia amefariki, ukweli kibinadamu nilisikitika sana kwa kuwa alikuwa ni mtu muhimu kwenye soka, lakini nilijua kabisa kuwa Simba inakwenda kupata wakati mgumu na hiki ndiyo kinatokea leo, nafikiri mechi umeiona na msimamo unaonesha hali halisi ilipo Yanga na Simba kwa sasa,” alisema Manji ambaye alidumu Yanga kwa miaka 13 kama mfadhili na mwenyekiti.
Manji ambaye alifanya usajili wa wachezaji wengi mastaa akiwa na Yanga kama mfadhili na baadaye mwenyekiti, amesema pamoja na kwamba walikuwa wanapambana na Hans Poppe kwa ajili ya kuhakikisha timu zao zinapata mafanikio, lakini nje walikuwa marafiki na walikuwa wanazungumza.
“Tulikuwa tunapambana sana uwanjani, lakini tulikuwa marafiki. (Hanspope) alikuwa akizungumza lazima nijue amesema nini. Huyu alikuwa ana nguvu kubwa sana kwenye soka la Tanzania na alikuwa anaweza kufanya jambo lolote na watu wakamuelewa.
“Nafikiri unakumbuka wakati tulipoichapa Simba mabao matatu hadi mapumziko, baadaye wakaja kurudisha yote. Hapa Hans Poppe alihusika, siwezi kukuambia alifanyaje, lakini nguvu yake ilisababisha Simba wakapata sare kwenye huo mchezo, alikuwa na ushawishi wa hali ya juu sana kwa wachezaji,”alisema Manji ambaye alijiuzulu uenyekiti Yanga, Mei 21, 2017.
USAJILI WAKE MKUBWA YANGA
Manji ambaye mwaka 2012 aligombea uenyekiti Yanga na kushinda ikiwa ni siku chache baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 5-0 na Simba, anasema moja ya usajili ambao anaukumbuka ni wakati alipomchukua kipa Juma Kaseja kutoka Simba, huku Hans Poppe akiwepo.
“Pamoja na uwepo wa Hans Poppe, lakini naamini kuwa niliwahi kumuumiza, nakumbuka Juma Kaseja akiwa na kiwango cha hali ya juu nilimsajili akitokea Simba kwa kitita cha shilingi milioni hamsini, hiyo ni mwaka 2014,” alisema Manji ambaye amekuwa akifuatilia soka la Tanzania kwa kipindi chote.
“Huu ndiyo ulikuwa usajili wangu mkubwa zaidi kwa kipindi chote nilichokaa madarakani, lakini pia alifanya kazi kubwa akiwa nasi kwani alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.”
Mbali na Kaseja pamoja na umafia wa Hans Poppe, Manji aliibomoa Simba kwa kuwasajili nyota wengine kama Mrisho Ngassa, Ally Mustapha ‘Barthez’, Kelvin Yondani, Deogratius Munishi ‘Dida’, Athuman Idd ‘Chuji’ na wengineo.
Kwa kipindi cha miaka mitano ambacho Manji alikaa madarakani, Simba haikuwahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu baada ya Yanga kuuchukua mara nne (2012/13, 2014/15, 2015/16 na 2016/17) na Azam mara moja (2013/14), baadaye mambo yakabadilika.
Akiizungumzia Yanga, Manji alisema katika kikosi hicho kwa sasa staa mkubwa ni mmoja tu. Stephane Aziz Ki na ndiye anamwelewa uwanjani.
Manji ambaye alikuwa katika Uwanja wa Mkapa, Aprili 20 akiishuhudia Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba alisema ameona mechi kadhaa za timu hiyo msimu huu, ikiwemo ile ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns pamoja na Dabi ya Kariakoo, lakini anaupongeza uongozi wa Yanga kwa kumsajili Aziz Ki.
“Nilifanikiwa kuutazama mchezo ule wa Yanga kule Afrika Kusini dhidi ya Mamelodi ambao Yanga ilifungwa kwa penalti. Niliwaona wamecheza vizuri sana, lakini kuna mchezaji mmoja nilimuona ana nywele za blonde (blichi), alionyesha kiwango cha juu sana na nimemuona pia kwenye mechi ya dabi (Dar),” alisema.
“Sijamfahamu vizuri jina lake, unajua siku hizi siyo kama zamani sasa navaa miwani na umri umeenda.”€ Lakini alipoonyeshwa picha tofauti za wachezaji wa Yanga na Mwanaspoti alipomuona Aziz Ki alisema: “Huyohuyo ndiye ninamaanisha, huku akicheka. (Aziz Ki) anakwenda uwanjani akijua nini anakwenda kufanya. Ndiye ananivutia sana akiwa na Yanga nafikiri kila mmoja atakubaliana nami.”
Hata hiyo alisema kuwa ameona mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha Yanga na wachezaji wanaonyesha uwezo wa juu uwanjani. “Nimefanikiwa kuwaona wachezaji wote wanaonyesha viwango vy juu uwanjani pamoja na kwamba huyo niliyemtaja ndiye bora, lakini wengine wote wamenifurahisha wanavyocheza. Timu inacheza vizuri sana,” alisema
Manji ambaye aliwahi kusajili mastaa wakubwa kwenye kikosi cha Yanga akiwemo kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima, alisema anafurahi kuona timu hiyo inafika sehemu ambayo ilikuwa ndoto yake.
KWANINI ALIGOMEA MAMILIONI?
Manji pia alieeleza sababu iliyomfanya wakati akiwa mwenyekiti wa Yanga agomee kitita cha fedha za udhamini kilichokuwa kikitolewa na chombo kimoja cha televisheni.
Chombo hicho ambacho kwa sasa kinadhamini ligi kiliingia mkataba na timu za Ligi Kuu ikiwemo Yanga na Simba ambapo inadaiwa kilikuwa kikitaka kutoa kitita cha Sh100 milioni kwa timu zote.
Klabu nyingine ikiwemo Simba zilikubaliana na dili hilo, lakini Yanga ikiwa chini ya Manji iligomea kwa kauli moja tu kuwa ni kiasi kidogo kutokana na ukubwa wa timu. “Tulikaa mezani mara kadhaa tukazungumza, lakini nilichokuwa nataka ni kuona timu za Simba na Yanga kwa kuwa zina mashabiki wengi, basi kiwango chao kiwe tofauti na timu nyingine za ligi,” alisema.
“Hili lilikataliwa lakini sisi tuliendelea kushikilia msimamo kuwa hatuchukui na wakati wote nilipokuwa kiongozi hatukuchua fedha hizo.
“Unajua wakati huo Azam FC ilikuwepo kwenye ligi, wakati huohuo kampuni mama ikawa inataka kudhamini ligi niliona kuwa kutakuwa na mgongano wa kimaslahi, ilikuwa jambo moja aidha kampuni isidhamini au waondoe timu kwenye ligi.”
Hata hivyo, Manji alisema hakupinga suala la mashabiki kuangalia mpira kwenye televisheni kwa kuwa ni maendeleo makubwa kwenye soka la Tanzania, lakini aliona kuna mambo mengi hayaendi sawa kwenye yale makubaliano.
“Mfano, sijui kama hilo leo lipo, lakini nilitaka kuona kama mechi ya Simba inachezwa Dar es Salaam, basi televisheni isionyeshe mechi hizo hapa jijini bali kwenye mikoa mingine, lakini hata kama Mtibwa inacheza Arusha pale mechi isionyeshwe kwenye televisheni.
“Kufanya hivyo kutawafanya mashabiki kwenda uwanjani kwa kuwa timu zote zinategemea viingilio, kuuza jezi, skafu na vitu vingine vya klabu sasa ukionyesha kwenye mkoa husika watu watabaki majumbani. Huwezi kuufanya mchezo huu ukaendelea kuwa wa furaha na watu kukutana viwanjani,” alisema.
Manji ambaye alichukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne akiwa na Yanga na kipindi chote timu ilishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, alisema anafurahi kuona ndoto zake zinatimia kwenye timu hiyo.
Alipoulizwa kama anaweza kurudi Yanga au kuwa mwekezaji alisema: “Kwa sasa siwezi. Kwanza umri umeenda siwezi zile pilikapilika za kusimamia timu.
“Unajua hata kama utakuwa ofisini tabia yangu ni kwamba napenda kufanya kazi zote nikiwa karibu. Naweza kuwa na viongozi wengine lakini nitalazimika kusafiri na wachezaji. Nahakikisha kila kitu chao kinaenda vizuri. Ukweli kwa kipindi hiki sitakuwa na uwezo tena wa kufanya hivyo wanatakiwa kufanya vijana,” alisema.
Mfanyabiashara huyo alisema alichukulia soka ni mchezo wa jamii ndiyo maana alifanya vitu vingi kama sehemu ya kuifurahisha badala ya kuwaza fedha.
“Nilianzisha mfumo wakati mwingine wa kununu tiketi zinaenda kugawiwa kwenye matawi ya Yanga kwa kuwa nilitaka kurudisha kwa jamii, kama unakumbuka mchezo wa Yanga na TP Mazembe kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza mashabiki waliingia bure,” alisema.
“Pale haikuwa bure kama ambavyo inafanyika sasa bali nilinunua tiketi zote zikagawiwa kwa mashabiki wa Yanga kupitia kwa viongozi wa matawi yao, nia ilikuwa ni kuhakikisha mchezo huu unarudi kwa jamii yetu.”
Alisema nia yake ya kwanza ilikuwa kutafuta muafaka kwa makundi yaliyokuwepo Yanga ambayo ni Yanga Asili, Yanga Kampuni na Yanga Akademia.
“Moja ya jambo ambalo nakumbuka nililifanya na kuisaidia Yanga hii kufika hapa ni kuweka umoja, wakati naingia nilikuta migogoro mingi kulikuwa na makundi matatu, nakumbuka moja liliitwa Yanga Asili, lingine Yanga Kampuni na moja liliitwa Yanga Akademia.
“Nilitumia ushawishi wangu wote na kuhakikisha haya makundi yanaisha na Yanga ikasimama, nafikiri imewasaidia hadi leo ndiyo maana kuna umoja,” alisema.
Manji aliajiri makocha kadhaa wakubwa Yanga wakiwemo Konstadian Papic, Milutin Sredojevic Micho, Sam Timbe, Ernest Brandts na Tom Santifiet.