TAMISEMI: Tuige mfano wa CRDB Bank Foundation kutoa fursa kwa vijana na wanawake

Dar es Salaam. Tarehe 29 Juni 2024: Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Adolf Ndunguru ameipongeza Taasisi ya CRDB Foundation kwa jitihada zake za kuwafungulia fursa vijana na wanawake na kuzitaka taasisi nyingine kuiga mfano huo ili kuongeza ujumuishi wa kifedha na kuharakisha maendeleo ya taifa.


Ndunguru ametoa wito huo alipofungua semina ya wajasiriamali wanawake na vijana iliyoandaliwa na Taasisi ya CRDB Bank Foundation na kufanyika makao makuu ya Benki ya CRDB.

“Ili kuwawezesha zaidi wajasiriamali wanawake na vijana, ni muhimu wadau wote wa maendeleo wakashiriki. Serikali pekee haitoweza kutatua changamoto zote zinazotukabili kwa kasi tunayoitarajia. Lazima tufanye kazi pamoja ili kujenga mazingira ambayo kila mwanamke na kijana anapata fursa ya kufanikiwa. 

 

Niipongeze CRDB Bank Foundation kwa kuja na programu hii ambayo inalenga kuboresha biashara za vijana na wanawake kwa kuwapa mafunzo na ushauri wa namna bora ya kusimamia na kuendesha biashara zao, kuwapa mitaji wezeshi, na kuwaunganisha na masoko ya ndani na nje ya nchi,” amesema Ndunguru.


Katibu mkuu huyo pia ameusifu utaratibu wa CRDB Bank Foundation kushirikiana na vikundi na taasisi za uwezeshaji wa wanawake na vijana nchini katika sekta mbalimbali za maendeleo kwamba unawafanya wananchi wajione ni sehemu ya benki na wanawajibika kwa maendeleo yao binafsi baada ya kupewa kemkem zilizopo kuweza kujikwamua kiuchumi.

“Kitendo cha kuwafikia wanawake wajasiriamali zaidi ya 400,000 na kutoa mitaji wezeshi yenye thamani ya shilingi bilioni 10 ndani ya muda mfupi kinaonyesha ni kwa namna gani mmejipanga kuleta matokeo makubwa kwa jamii yetu. Nivipongeze pia vikundi na taasisi mnazoshirikiana nazo katika kutekeleza Programu ya Imbeju. Serikali tunajivunia tukiona tulizozipa kibali cha kuchochea ujumuishi wa kifedha kwa wananchi na kukuza ustawi wa jamii zinakitimiza malengo yake kwa ufasaha,” amesisitiza Ndunguru.


Katibu mkuu ametoa pongezi hizo baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa kueleza kuwa malengo ya taasisi hiyo ni kutoa elimu ya fedha, kukuza ubunifu na teknolojia, kuwawezesha wajasiriamali kwa mtaji, kuongeza ujumuishi wa kifedha na kiuchumi ili kuboresha  maisha ya vijana na wanawake. 

“Najivunia kukujulisha kuwa CRDB Bank Foundation imeshatoa mafunzo kwa wanawake na vijana zaidi ya 400,000 sambamba na mitaji wezeshi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 10. Wajasiriamali hawa, licha ya kufunguliwa Akaunti ya Imbeju, wana fursa ya kuwa mawakala wa Benki ya CRDB, kupata bima ya mazao na mifugo, kufahamu masoko mapya ya huduma au bidhaa zao pamoja na kufanya biashara ya kimataifa kupitia mpango Eneo Huru la Biashara Huria la Africa (AfCFTA),” amesema Tully.


Ili kuwafikia wanufaika wengi zaidi, Tully amesema wanashirikiana na wadau wa ndani na wa kimataifa BUTA VICOBA Endelevu, Bunju Women Entrepreneurs (BWE), Mbweni Women Empowerment (MWE), Eden Group,  UWABISORA, Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Tume ya TEHAMA (ICTC), Sokoine University Graduate Entrepreneurs Cooperative (SUGECO),  pamoja na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Kabla ya kumkaribisha geni rasmi kuzungumza na zaidi ya washiriki 350 wa semina hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki y CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema wanawake na vijana ni kundi lenye uwezo mkubwa wa kuliinua taifa kuondokana na umasikini ndio maana bodi ya wakurugenzi na menejimenti wameridhia kuelekeza nguvu kubwa kuwawezesha kushiriki kuujenga uchumi.


“Wanawake na vijana ni makundi yanayokabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi ndio maana Benki yetu ya CRDB kupitia CRDB Bank Foundation iliona kuna kila sababu ya kutoa elimu na kuwapa mitaji wezeshi wale wanaokidhi vigezo ili kujenga uchumi jumuishi na shirikishi ili kuwa na maendeleo endelevu,” amesema Nsekela.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki y CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya wajasiriamali
wanawake na vijana iliyoandaliwa na Taasisi ya CRDB Bank Foundation na
kufanyika katika makao makuu ya Benki ya CRDB, mwishoni wa wiki.

Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bank Foundation, Martin Warioba akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya wajasiriamali
wanawake na vijana iliyoandaliwa na Taasisi ya CRDB Bank Foundation na
kufanyika katika makao makuu ya Benki ya CRDB, mwishoni wa wiki.


Related Posts