Dar es Salaam. Wanaharakati na marafiki wa kijana Japhet Matarra, anayetumikia kifungo cha miaka mitano gerezani kwa makosa ya mtandao kupitia mtandao wa X, wamechangisha Sh8.5 milioni kwa ajili kumtoa gerezani kijana huyo.
Matarra alihukumiwa Juni 2023 na Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa kosa la mtandao la kuhoji utajiri wa marais nchini Tanzania.
Adhabu aliyopaswa kuitumikia ilikuwa kulipa faini ya Sh7 milioni au kutumikia kifungo cha miaka mitano, gerezani.
Kutokana na familia kutomudu faini hiyo, kijana Matarra alianza kutumikia adhabu yake katika gereza la Karanga tangu mwaka jana.
Twaha Mwaipaya ni miongoni mwa wanaharakati wanaoratibu michango mtandaoni kwa ajili ya kumtoa kijana huyo gerezani, amezungumza na Mwananchi kwa njia ya simu na kusema kuwa utaratibu wa kisheria unaendelea na kijana huyo atakuwa huru kuanzia leo Jumatatu Julai mosi, 2024.
“Kuanzia jana ndani ya saa 12 tayari tulichangisha Sh7.2 milioni na leo michango imefika Sh8.5 milioni, wanasheria wetu wanaendelea na utaratibu wa kumtoa na leo atakuwa huru, fedha nyingine tutampatia akaanzie maisha baada ya kutoka gerezani,” amesema.
Akielezea mkasa uliompata kijana huyo, Mwaipaya amesema “Japhet Matara alifungwa Juni 2023 kwa makosa ya mtandao uliohusisha yeye kuhoji utajiri wa marais na hapo alikamatwa na polisi kesi yake kwenda Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Wilaya ya Moshi na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani au faini ya shilingi milioni saba,” ameeleza.
Twaha amesema baada ya hukumu hiyo wakili wake alikata rufaa, lakini ilikataliwa hivyo kuendelea kusota gerezani.
Kutokana na hali hiyo, marafiki na wanaharakati juzi walikubaliana kuchangishana fedha kupitia mtandao wa X kwa ajili ya kwenda kumlipia faini kijana huyo.
Kuhusu familia, Twaha amesema Japhet ni baba wa watoto wawili na mkazi wa Moshi mkoa wa Kilimanjaro tangu alipohukumiwa gerezani, mkewe hakwenda kumjulia hali kutokana na ugomvi walionao.
“Watu walipokwenda kumtembelea alishukuru sana, akatueleza kuwa hakuna mtu aliyewahi kwenda kumuangalia gerezani,” amesema.
Kwa upande wa wazazi kutokwenda gerezani kumjulia hali mtoto wao, Twaha amesema wazazi wa kijana huyo ni wazee na hawana uwezo wa kusafiri kutoka Mkoa wa Mara kwenda Kilimajaro katika gereza la Karanga alikohukumiwa.
Baba mzazi wa Japhet, Ibrahim Matarra amesema hakuwahi kwenda kumjulia hali kutokana na ugumu wa maisha.
Amesema hakuna jambo angelifanya kumuona mtoto wake akiwa hai na kila kitu alimuachia Mungu.
“Sikuwa na jinsi ya kufanya, miaka ni mingi na faini ni kubwa sina kitu cha kumsaidia, kipato changu chote nilikitumia kumsomesha, nilifuta mategemeo ya kumuona nikiwa hai, niliambiwa nikikata rufaa huenda adhabu ikaongezwa, nilibaki njia panda kwa sababu nilitegemea huyu kijana angenisaidia. NI mtoto wangu wa kwanza,” amesema Matarra.
Mzee Matarra amesema mkwe wake alikorofishana na kijana wake kabla ya kuhukumiwa gerezani, hivyo hata alipohukumiwa hakuwa na muda naye.
Baba huyo amesema ni furaha isiyo na kifani kwake kumuona mtoto wake akiwa uraiani, huku akitoa shukranI kwa wote wanaoshiriki kumtoa gerezani.
Hatua ya kutumia mtandao wa X kuchangisha ni ya pili kwa wiki chache zilizopita ambapo kijana Edger Mwakalebela maarufu mtandaoni kama ‘Sativa’ aliyedaiwa kutoweka na baadaye kupatikana akiwa amejeruhiwa, alichangiwa Sh11 milioni kwa ajili ya matibabu.
Hivyo ndani ya kipindi kifupi mtandao wa X umetumika kuchangisha zaidi ya Sh19 milioni kwa watu wawili.