Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam. limesema bado halijafanikiwa kuwatia mbaroni wanafunzi 10 wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) wanaokabiliwa na tuhuma za kufanyiwa mitihani.
Katika sakata hilo, wanaotakiwa kukamatwa ni wanafunzi 17 na hadi juzi Jumamosi, Juni 29, 2024 ni wanafunzi saba pekee walithibitishwa kutiwa nguvuni kwa mujibu wa jeshi hilo, huku likiendelea kuwasaka wengine.
Chanzo cha mtanziko huo kinatokana na taarifa iliyotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Elifas Bisanda kusema waliwakamata watu 17, kwa kosa la kuwafanyia mitihani wanafunzi wa chuo hicho, kuanzia Juni 18, 2024 katika vituo vya Ilala na Kinondoni, Dar es Salaam wakiwa na vitambulisho vya kughushi na tiketi za kuingia katika ukumbi wa mitihani.
Akizungumza na Mwananchi, leo Julai mosi, 2024 Kaimu kamanda wa kanda hiyo, SACP Foka Dinya amesema bado wanaendelea na msako hadi watimie kulingana na idadi ya watuhumiwa wanaoshikiliwa kwa kuwafanyia mitihani.
“Idadi ya wanafunzi tunaowashikilia bado walewale saba, tunaendelea kuwasaka wale 10 waliobakia, naona wamekimbia baada ya kusikia tunawatafuta, tumeshatega mifumo ya kuwakamata,”amesema.
Kwa mujibu wa maelezo yake SACP Dinya, amebainisha kuwa wanajua watu wakifanya makosa huwa wanahangaika namna ya kujificha, lakini wameweka mipango kwa kushirikiana wananchi pamoja na chuo kuona wanakamatwa.
“Jeshi liko makini kuwafuatilia na kuwakamata, ili kuja kujibu tuhuma zinazowakabili na ikithibitika wafikishwe kwenye vyombo vya dola kukabiliana na mashtaka yao,” amesema.
Kamanda huyo amesema watuhumiwa hao 24, wako chini ya ulinzi katika Kituo cha Polisi Oysterbay, Kinondoni na wanaendelea kuhojiwa na mkuu wa upelelezi, ili kupata vielelezo vya uthibitisho kulingana na tuhuma zinazowakabili.