Dar es Salaam. Kukiwa na upepo mkali Jumatano ya Aprili 18, 2024 simu yangu iliingia ujumbe mfupi kutoka kwa aliyekuwa mwenyekiti na mfadhili wa Yanga, Yusuf Manji akinitaka tuende uwanjani kutazama mechi ya Simba na Yanga.
Hivyo ndivyo anaanza kusimulia mwandishi wa habari Zourha Malisa ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Manji aliyezikwa nchini Marekani leo Julai Mosi, 2024 baada ya kufariki Jumamosi iliyopita akiwa hospitalini Florida.
Kwa mujibu wa taarifa ambayo mtoto wa marehemu Mehbub Manji, amelitumia Mwananchi inasema kuwa mfanyabiashara huyo atazikwa saa tisa na kama familia wanashukuru kwa jinsi ambavyo Watanzania wameendelea kuombeleza kifo hicho.
Zourha ambaye alifanya mahojiano marefu na Manji miezi miwili iliyopita, alikuwa mmoja kati ya marafiki wa familia ya Mwenyekiti huyo wa zamani wa Yanga na kila mara alikuwa akifika hapa nchini ni lazima atawasiliana naye.
“Manji alifika hapa nchini Aprili 18 na siku hiyohiyo akanitumia meseji kuwa anataka tuende uwanjani kutazama Dabi Aprili 20, lakini bahati mbaya nilikuwa kwenye kikao muda huo, hivyo sikuuona ujumbe wake, dakika chache baadaye akanipigia simu, lakini pia sikuweza kuipokea,” anaanza kusimulia Zourha huku akionyesha huzuni.
Mashabiki wa Yanga watamkumbuka Manji kwa mafanikio makubwa akiwa madarakani ambapo alichukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne akianza 2012/2013 na mara tatu mfululizo 2014/2015, 2015/2016 na 2016/2017 huku kwa kipindi chake chote Simba ikishindwa kutawala kwenye soka la Tanzania.
“Baadaye nilimtafuta simu yake haikupokelewa, lakini majira ya saa moja usiku alinitumia meseji akaniambia yupo nchini na anafahamu kuwa siwezi kwenda naye uwanjani kutazama mechi kwa kuwa mimi ni mwandishi wa habari kama nitakwenda. Nitaenda peke yangu.
“Tulichati kidogo, baadaye akaniambia anataka kupumzika tutaonana baada ya mechi Aprili 20, tukaagana na kila mmoja kuendelea na shughuli zake.”
Zourha anasema tangu anamfahamu Manji alikuwa mtu mpole, lakini mwenye mapenzi ya hali ya juu na Yanga, ndiyo maana alikuwa anaweza kusafiri kutoka mbali kuja kuitazama timu hiyo ikicheza na hata mechi ya Yanga na Mamelodi kule Afrika Kusini alihudhuria.
“Sikuwasiliana naye tena, siku ya mechi alinitumia meseji akiwa uwanjani na kuandika ‘Tafadhali weka kwenye gazeti lako. Unafikiria nini? Kila shabiki wa Yanga ananishangilia hapa uwanjani na wengine wanataka kupiga selfie nami. Unajua kila mechi ya Yanga ambayo nimewahi kuja uwanjani, hatujawahi kupoteza mchezo. Nilimjibu ni vizuri sana, akasema tupange muda tufanye mahojiano. Nilishtuka kwa kuwa siyo kawaida yake,” anasema.
Katika mchezo huo, Yanga ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, ambapo mabao ya Yanga yalifungwa na Stephene Aziz KI na Joseph Guede huku lile la Simba likifungwa na Freddy Michael.
“Kwa upande wangu ilikuwa kama bahati ya pekee, kwanza nilipata hofu kwa kuwa kwa kipindi chote Manji hakuwahi kukubali kufanya mahojiano kuhusu Yanga pamoja na ukaribu ambao tulikuwa nao.
“Ila siku ile ilikuwa tofauti sana kwani mwenyewe ndiye alitaka mahojiano yale na akawa ananiuliza tufanye lini?” Alisema Zourha.
Zourha anasema Aprili 21, ndiyo walikubaliana na Manji kufanya mahojiano hayo na ilipofikia jioni majira ya saa 11, mfanyabiashara huyo ambaye alikuwa mmiliki wa Quality Group Company, alimpigia simu na kumueleza kuwa yupo tayari.
“Baada ya mechi aliniambia anakwenda Dodoma na tutafanya mahojiano Aprili 21 jioni hivyo siku hiyo nilijiandaa na kuzungumza na baadhi ya watu ofisini ili waniongezee maswali ingawa wengi waliamini kuwa sitafanikisha mahojiano hayo.
“Baadaye alinitumia location kwenye simu yangu kunionyesha kuwa yupo sehemu gani, niliwasha gari na kwenda kumfuata alipo,” alisema Zourha.
Zourha aliendelea kusimulia kuwa: “Mara nyingi nilikuwa nikienda kuonana na Manji nyumbani kwake au ofisini ananipokea mwenywe, lakini safari hii nilishangaa sana.
“Nilipofika aliponielekeza nilimuona ndugu yake akija upande wangu na kunichukua kwenda sehemu ambayo alikuwa amekaa. Nilishtuka.
“Manji alikuwa amekaa kwenye kiti, akionekana kuwa mnyonge huku sauti yake ikitoka kwa shida sana tofauti na jinsi ambavyo nilikuwa nimemzoea siku za nyuma, alikuwa mchangamfu na mcheshi sana lakini siku hiyo ilikuwa tofauti.”
Zourha anasema kuwa mwenyekiti huyo wa zamani ambaye aliingia madarakani siku chache baada ya Simba kuichapa Yanga mabao 5-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara alikuwa anafahamu kuhusu matatizo ya kifamilia ambayo alikuwa ameyapata mwezi mmoja uliopita, hivyo alianza kwa kumpa pole.
“Tulipoanza mazungumzo yetu ilinibidi niwe makini sana kumsikiliza kwani sauti yake ilikuwa inatoka kwa shida sana, huku wakati mwingine akitulia kimya kwa zaidi ya sekunde 40 hadi 50 ndiyo anajibu swali.
“Mazungumzo yetu yalikuwa yanazungumzia maswala ya soka la Tanzania tu, Yanga na Simba na wakati mwingine Ligi Kuu kwa ujumla lakini kwa hakika alionekana kufurahishwa na maendeleo ya Yanga kwa sasa, huku akipongeza kuhusu uwekezaji unaofanyika kwenye klabu hiyo.”
Anaendelea kusema, Manji alikuwa hana tabasamu kama kawaida yake na alimuuliza anajisikiaje kuona Yanga imeshinda michezo yote miwili kwa msimu mmoja dhidi ya Simba, ambapo alimjibu.
“Nilipomuuliza hili swali alianza kuzungumza nambo mengi kuhusu Yanga, uwekezaji unaofanyika, akisema ni matunda yale ambayo alikuwa anayapigania, lakini jambo ambalo siwezi kulisahau alisema kama Yanga itakuwa na fedha, basi inaweza kuchukua ubingwa miaka kumi mfululizo.”
Kwenye mahojiano hayo, ambayo yalichapishwa na Mwananchi, Manji alizungumzia uwezo wa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Stephane Aziz KI na kusema kuwa ndiye mchezaji mahiri zaidi kwenye kikosi hicho chini ya Kocha Miguel Gamondi
“Hata hivyo, wakati tunazungumza, walionekana baadhi ya ndugu zake wakipanga vitu vyake ambapo nilipomuuliza alinijibu kuwa usiku anaondoka kurudi Marekani.
“Alinishtua ghafla wakati tunazungumza. Aliniambia unaona jinsi nilivyo kwa sasa, nitazame vizuri, haya maisha siyo ya kwetu, hapa duniani tunapita tu.”
Zourha anasema alimuuliza kwanini hivi sasa amekubali kufanya mahojiano wakati kwa kipindi chote alikuwa anagoma, akasema amefanya hivyo kwa kuwa anaipenda Yanga na anataka wafahamu hivyo.
Asimama baada ya saa mbili
“Baada ya saa mbili tukiwa tunafanya mahojiano tulimaliza na Manji akasimama kwa mara ya kwanza, alikuwa akitembea taratibu sana lakini akionekana kuwa na maumivu na kuingia ndani ambapo alikaa kwa zaidi ya dakika kumi, akarejea na kuniaga nikaondoka.”
Zourha anasema baada ya Manji kufika Marekani alimtumia ujumbe mfupi kuwa amefika salama.
Anasema siku tatu mbele waliwasiliana na ujumbe wa mwisho ambao Manji alimtumia, alimwambia TUOMBEANE, hadi juzi mwanaye Mehbub alipomtumia ujumbe kuwa baba yake amefariki.
“Niliona taarifa kwenye mitandao, nilipomtumia meseji mwenyewe ilionekana imefika lakini haikujibiwa, mwisho niliwasiliana na mwanaye Mehbub ambaye aliwahi kunitambulisha kwake na kunieleza kuwa baba yake amefariki.”