Wazalishaji sukari wavunja ukimya, wadai kutotendewa haki sakata la sukari

Dar es Salaam. Umoja wa Wazalishaji wa sukari nchini (TSPA) umekanusha madai ya kuficha sukari ili kuongeza bei kwa faida yao binafsi.

Wamesema hawana nia ya kuwa waagizaji kwa sababu lengo lao ni kuzalisha zaidi, huku wakilalamika kwamba wametuhumiwa na kuhukumiwa bila kupewa nafasi ya kusikilizwa.

Wamesema wao hawana nia ya kuwa waagizaji wa sukari, kwa sababu lengo la biashara yao ni kuzalisha zaidi.

Akizungumza kwa niaba ya wazalishaji wa sukari leo Jumatatu, Julai 1, 2024, mbele ya vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Wazalishaji wa Sukari nchini, Ammi Mpungwe, amesema tangu utabiri wa hali ya hewa ulipotangazwa na kuonesha kwamba kutakuwa na mvua za El Nino, wazalishaji waliwasiliana na mamlaka za Serikali kuzitaarifu kwamba Desemba mwaka jana kungekuwa na tatizo.

Kwa hivyo, waliomba utaratibu wa uagizaji sukari uwekwe.

Licha ya ufafanuzi huo, itakumbukwa siku chache zilizopita, kulikuwa na mijadala sehemu mbalimbali ikiwamo kwenye Bunge lililoahirishwa Ijumaa Juni 28, 2024 iliyokuwa  ikiwatuhumu wafanyabiashara hayo kuhusika katika kusababisha bei ya sukari kupanda bei.

Baadhi ya watu katika mijadala hiyo walidai wazalishaji wanatengeneza nakisi ya sukari kwa makusudi ili waweze kujinufaisha, jambo ambalo Mpungwe anasema si kweli.

“Kulikuwa na mawasiliano na si mara moja wala  mbili, tulikuwa tunakumbushia na kweli ilipofika Desemba hali ikaanza kuwa vile tulivyosema,” amedai Mpungwe.

Amesema cha kushangaza, hadi  Desemba vibali vya kuagiza sukari vilikuwa havijatoka na Kampuni ya Sukari Kilombero ikalazimika kuizuia meli yake iliyokuwa inapeleka tani 45,000 ya sukari nchi nyingine na kuagiza iingizwe nchini kwa lengo la kufidia upungufu mkubwa uliojitokeza.

Mpungwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kilombero Sugar, amesema si kweli kwamba kampuni hizo zilipewa vibali vya kuagiza sukari na kuviuza.

Amesema kazi ya uagizaji sukari kutoka nje si yao, wao ni wazalishaji tu na hulazimika kuingilia kati kwenye usambazaji kama kuna uhaba nchini kama walivyofanya kwa lengo la kukabiliana na uhaba na vurugu kama zilizokuwepo.

“Sisi kama Kilombero hatutaki kuingia katika biashara ya kuagiza sukari, tuko katika biashara ya kuzalishaji sukari, hili wazo la kuweka chombo cha Serikali kuagiza sukari nadhani lingekuja tangu mwanzo tungeunga mkono,” amesema Mpungwe.

Amesema wazalishaji hao waliamua kukaa kimya pale waliporushiwa maneno kwa sababu  walikuwa wakiwasiliana na Spika wa Bunge ili wapate nafasi ya kuzungumza na Kamati ya Kilimo na Viwanda, lakini walipangiwa kukutana Agosti, mwaka huu.

“Tulipewa nafasi ya kukutana na kamati ya uchumi na bajeti wiki iliyopita, lakini ilikuwa ni kuzungumzia muswada wa fedha, tulijitahidi kuwa na mawasiliano lakini uamuzi umetoka bila sisi kuhusishwa tumekuwa watuhumiwa hadi tumehukumiwa bila sisi kusikilizwa,” amesema Mpungwe.

Amesema kutuhumiwa kwamba hawawafikirii Watanzania zaidi ya milioni 60 si sawa, kwa sababu wamefanya uwekezaji mkubwa unaodumu kwa zaidi ya miaka 60.

“Tumeshutumiwa kuwa sisi ni cartel ni tuhuma nzito katika biashara, huwezi kuwa na mpango mkubwa wa kuwekeza ukajiingiza katika mambo haya na tuhuma hizi haziamriwi kisiasa,” amesema.

Amesema kama kuna hofu kuwa wawekezaji hawa wanacheza mchezo mchafu kwenye biashara, wapelekwe Tume ya Ushindani (FCC), wakajibu tuhuma zao huko.

 Naye Mwakilishi wa Bagamoyo Sugar, Hussein Sufian amesema kauli ya kuvitaka viwanda vya sukari kutoficha sukari wakati hakuna kiwanda kilichowahi kuficha sukari, sio sahihi.

Amesema wamejengewa taswira mbaya isiyo na ukweli kwa washirika wa maendeleo ya sekta ya sukari na umma kwa jumla.

Kuhusu dhamira ya kuondokana na uzalishaji sukari nchini ili kuleta sukari ya nje na wakulima kuhamasishwa kulima mazao mbadala kama mpunga, amesema inadhoofisha jitihada zilizokwishafanyika za kuleta utulivu kwenye sekta ya sukari.

Wakati hayo yakisemwa, Sufian amesema pia sekta hiyo inaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya gharama kubwa za uzalishaji.

“Gharama za mahitaji muhimu kwa kilimo cha miwa na uzalishaji sukari zimeongezeka sana katika miaka ya hivi karibuni pia uwepo wa sera zisizotabirika za soko la sukari ni tatizo,” amesema Sufian.

Mwananchi ilimtafuta Msemaji wa Serikali, Thobias Makoba kutaka kujua undani wa malalamiko hayo, akajibu kwa ujumbe wa maandishi kuwa; “Ningekushauri kwa hoja kama hizi ni vyema ukaanza na wizara ya sekta husika.”

Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi alipoulizwa kuhusu barua zilizoandikwa na TSPA aliomba kutumiwa ujumbe mfupi ambao haukujibiwa.

Kwa upande wa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe na Naibu wake, Joseph Silinde na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Mweri simu zao ziliita bila kupokelewa.

Related Posts