Geita. Mahakama Kuu kanda ya Geita imemuachia huru Stephano Mlenda (31) Mkazi wa Chigunga Wilaya ya Geita, aliyekuwa akishtakiwa kwa kosa la kumuua mtoto wake wa miaka tisa kwa kutokusudia.
Baba huyo anadaiwa kumchapa kwa fimbo mwanawe huyo baada ya kubaini ameiba Sh700 na kwenda kununua soda.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu Julai Mosi, 2024 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina, baada ya mshtakiwa kukiri kutenda kosa hilo.
Kesi hiyo namba 12,387 ya mwaka 2024, ilikuja mahakamani hapo kwa ajili ya upande wa mashtaka kuleta mashahidi, na kabla ya ushahidi kuanza kutolewa, mshtakiwa alikiri kutenda kosa la kuua bila kukusudia.
Ilivyokua kabla ya hukumu
Awali, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Luciana Shaban ameeleza Mahakama Kuu kuwa Mlenda anashtakiwa kwa kumuua Fredrick Stephano (9) bila kukusudia kinyume na kifungu cha 95 na 98 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kilichofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Amedai Mahakamani hapo kuwa siku ya tukio huko Chigunga Wilaya ya Geita saa moja usiku, Fredrick (marehemu) aliiba Sh700 na kwenda kununua soda na mtuhumiwa ambaye ni baba yake alimkuta anakunywa soda hiyo ndipo akaanza kumchapa kwa fimbo huku wakielekea nyumbani kwao.
Amedai baada ya kufika nyumbani, baba huyo aliifunga miguu na mikono ya mtoto huyo kwa kamba na akaendelea kumchapa sehemu mbalimbali za mwili wake na siku iliyofuata, Novemba 17, 2023 mtoto huyo alifariki dunia.
Tukio hilo liliripotiwa polisi na askari walifika na kumkamata mshtakiwa, katika mahojiano alikiri kusababisha kifo cha mtoto wake kutokana na kipigo.
Uchunguzi wa kidaktari ulibaini chanzo cha kifo cha mtoto huyo kilitokana na majeraha kwenye ubongo.
Hata hivyo, mwendesha mashtaka ameieleza Mahakama kutokana na mshtakiwa kukiri mashtaka na Mahakama kumkuta na hatia ya kosa la kuua kwa kutokukusuida, amesema upande wa Jamhuri hauna kumbukumbu ya makosa ya jinai aliyowahi kuyafanya mshtakiwa.
Hivyo, akaiomba Mahakama kutoa adhabu itakayokuwa fundisho kwake na kwa wazazi wengine kuwa waangalifu watakapokuwa wanawaonya watoto wao wasiwaletee madhara.
Wakili wa upande wa utetezi, Elizabeth Msechu akaieleza Mahakama kuwa mtuhumiwa huyo ni kijana mdogo na Taifa bado linamtegemea kama nguvu kazi yake.
Lakini pia ni baba wa watoto wanne wenye umri chini ya miaka tisa wanaohitaji malezi ya baba.
Pia, mtuhumiwa huyo anawalea watoto wawili wa dada yake ambaye ni marehemu, na kwa kuwa hakuwa na nia ya kumuua mtoto wake na miezi minane aliyokaa mahabusu, hivyo ameshajutia kosa lake.
Hivyo, akaiomba Mahakama impunguzie adhabu na ikiwezekana apewe kifungo cha nje.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji Mhina amesema kilichotokea siku hiyo ilikua lengo la mzazi kumuadhibu au kumuonya mtoto wake kwa kuwa aliiba pesa na sio kuua.
“Pia, kutokana na mshtakiwa kutokuwa na kumbukumbu yoyote ya makosa ya jinai na kukiri kwake mapema kabisa alipofikishwa polisi na leo hapa mahakamani, hivyo kwa sababu hizo, mshtakiwa anastahili kupata huruma ya mahakama,” amesema jaji.
Amesema kutokana na sababu hizo, Mahakama chini ya Kifungu cha 38(1) cha Makosa ya jinai, inamwachia mshtakiwa huru kwa masharti ya kutofanya kosa lolote la jinai kwa kipindi cha miezi 12 kuanzia leo.