Jatu afikisha siku 111 za majadiliano na DPP

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Jatu PLC, Peter Gasaya (33), anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka mawili, likiwemo la kujipatia Sh 5.1bilioni kwa udanganyifu, amefikisha siku 111 tangu aanze majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) ya kuimaliza kesi yake.

Hata hivyo, Serikali imedai bado haijafikia tamati katika majadiliano yao.

Gasaya anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka Saccos ya Jatu kwa madai kuwa fedha hizo atazipanda kwenye kilimo cha mazao, ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo.

Mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,Dar es Salaam.

Machi 12, 2024 Mahakama hiyo ilitoa siku 30 kwa upande wa mashtaka kuanza vikao vya majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo, baada ya mshtakiwa huyo kumwandikia barua DPP ya kukiri na kuomba apungiziwe adhabu.

Hata hivyo, tangu Mahakama hiyo itoe muda huo hadi leo, Julai mosi, 2024 mshtakiwa hiyo amekuwa katika vikao vya majadiliano ya kuimaliza kesi yake na DPP kwa siku 111 ambazo, sawa na miezi mitatu na siku 20.

Leo, Wakili wa Serikali Eva Kassa, ameieleza Mahakama hiyo bado hawajamaliza vikao vya majadiliano na kutokana na majadiliano hayo kuchukua muda mrefu, wanaomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na vikao vya majadiliano.

“Mheshimiwa hakimu, Serikali bado inaendelea na majadiliano na Gasaya na haijafikia tamati, hivyo tunaiomba Mahakama yako itupangie tarehe nyingine, ili tuendelee na vikao,” amedai Kassa.

Tofauti na siku nyingine ambapo kesi yake huendeshwa kwa njia ya video, leo mshtakiwa huyo ameletwa mahakamani kwa ajili ya kesi yake kutajwa na upande wa mashtaka kutoa taarifa ya maendeleo ya kikao cha majadiliano pamoja na kuendelea na vikao vya majadiliano.

Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mhini anayesikiliza shauri hilo, alikubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hadi Julai 15, 2024 itakapotajwa. Mshtakiwa yupo rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kwa mara ya kwanza, Gasaya alifikishwa mahakamani hapo Desemba 29, 2022 na kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Katika kesi ya msingi, mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kujipatia kiasi hicho cha fedha pamoja na kutakatisha Sh5.1 bilioni katika kesi ya uhujumu uchumi namba 8/2023.

Katika shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa katika ya Januari mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam, akiwa kama Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo kwa ya udanganyifu alijipatia Sh 5,139,865,733 kutoka Saccos ya Jatu.

Mshtakiwa wanadaiwa kujipatia fedha hizo kwa udanganyifu kutoka Saccos ya Jatu kwa kujipambanua kwamba fedha hiyo ataipanda kwenye kilimo cha mazao, jambo ambalo alijua kuwa sio kweli.

Shtaka la pili ni kutakatisha kiasi hicho cha fedha tukio analodaiwa kulitenda kati ya Januari mosi, 2020 na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam.

Siku hiyo ya tukio na eneo hilo, mshtakiwa akiwa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa Jatu Saccos, alijihusisha na muamala wa Sh 5,139,865,733 kutoka akaunti ya Jatu Saccos iliyopo Benki ya NMB, tawi la Temeke kwenda katika akaunti ya Jatu PLC liyopo Benki ya NMB tawi la Temeke, wakati akijua fedha hizo zinatokana na kosa tangulizi la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Related Posts