Kutana na mwanamke mwenye nywele ndefu zaidi duniani

Mwanamitindo maarufu nchini Ukraine, Aliia Nasyrova (35) ametajwa kuvunja rekodi ya ‘Guinness” ya kuwa mwanamke mwenye nywele ndefu zaidi duniani.

Awali, nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Smita Srivastava kutoka India, ambaye mwaka 2023 alitangwazwa kuwa mwanamke mwenye nywele ndefu zaidi duniani, zikiwa na urefu wa sentimita 236.22.

Kwa mujibu wa tovuti ya Guiness Word, nywele za mlimbwende huyo zinafikia urefu wa sentimita 257.33 ambazo zinatajwa kuzidi hadi kimo chake ambacho ni sentimita 165.

Si yeye tu, urefu wa nywele hizo unatajwa kumzidi hata mtu anayetajwa kuwa mrefu zaidi duniani Sultan Kösen aliyekuwa na urefu wa sentimita 251.

Katika mahojiano aliyofanya na tovuti hiyo, Nacyrova ambaye ni mkazi wa mji wa Slovakia amedai katika maisha yake hajawahi kukata nywele zake na kutoa wito kwa wanawake wengine kujivunia vile ambavyo Mungu amewabariki.

Nasyrova amesema kilichomsukuma kukuza nywele zake hadi kufikia urefu huo ni kuvutiwa kwa namna ambavyo mama na bibi yake walikuwa na nywele ndefu, alisimuliwa simulizi ya Rapunzel ambayo ni maarufu kwa watoto wengi duniani.

Alipoulizwa kuhusu siri ya ukuaji wa nywele zake, Nacyrova hakuwa mchoyo alibainisha baadhi ya mambo ambayo huwa anayazingatia, ikiwemo usafi wa nywele zake.

Amesema huwa anaosha nywele zake mara moja kwa wiki na humchukua takribani dakika 30 kutakata kutokana na wingi na urefu wake.

Baada ya kuosha nywele hutumia ‘steaming’ ambayo kutokana na wingi wa nywele zake hutumia takribani saa mbili kuzifikia nywele zote.

“Huwa situmii vifaa vya kukaushia nywele, naziosha zikauke zenyewe kwa upepo, napaka bidhaa asili ambazo ninaziandaa mwenyewe na kujiepusha na kuchana nywele zikiwa hazijakauka vizuri,” ameeleza.

Pia amesema moja kati ya siri ya kuwa na nywele ndefu ni pamoja na kula mlo kamili pamoja na kujiepusha na ulevi.

Nasyrova amesema pamoja na kupata umaarufu urefu wa nywele zake, pia unampatia kipato kwa kutumiwa kama mwanamitindo, muigizaji pamoja na kutengeneza maudhui katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwemo Youtube, Facebook na Instagram.

Related Posts