Dar es Salaam. Raia wa Oman, Hatem Mohamed (37) na mwenzake Ally Ally (26), wamehukumiwa kwenda jela miezi 12, baada ya kushindwa kulipa faini ya Sh1 milioni kila mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya kughushi kadi ya mpiga kura na kudanganya maofisa uhamiaji.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatatu Julai mosi, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi wa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, baada ya washtakiwa hao kukiri kosa hilo. Ally, ambaye ni Mtanzania anayeishi nchini Oman pamoja na Mohamed, wanadaiwa kutengeneza kitambulisho hicho cha mpiga kura kwa ajili ya kukitumia katika matembezi waliyokuwa wamepanga kuyafanya visiwani Zanzibar Juni 21, 2024.
Washtakiwa hao wametiwa hatiani baada ya wakili kutoka Idara ya Uhamiaji, Raphael Mpuya kuwasomewa mashtaka yao katika kesi ya jinai namba 17967 ya mwaka 2024 na kisha washtakiwa hao kukiri mashtaka hayo na kuomba wapunguziwe adhabu.
“Washtakiwa mmetiwa hatiani kama mlivyoshtakiwa baada ya kukiri mashtaka yenu mawili ambapo kila mshtakiwa anatakiwa kulipa faini ya Sh500,000 au kwenda jela miezi sita kwa kila shtaka,” amesema Hakimu Mushi.
Kabla ya kutolewa hukumu hiyo, Hakimu Mushi amewauliza washtakiwa iwapo wana lolote la kusema, ili Mahakama iwafikirie kabla ya kutoa hukumu.
Mshtakiwa Ally aliomba Mahakama impunguzie adhabu kwa sababu walikutana na watu ambao waliwarubuni kughushi kitambulisho na haikuwa dhamira yake.
“Kosa tulilofanya halikuwa lengo letu na mimi nilikuwa Oman kwa muda wa miaka mitatu, sasa tulikutana na watu wakatulaghai na mimi sikuwa nafahamu taratibu zozote za Uhamiaji,” amedai Ally.
Kwa upande wake, Mohamed aliomba Mahakama iwapunguzie adhabu na kwamba hawatarudia tena.
Washtakiwa baada ya kujitetea, Wakili Mpuya amesema upande wa mashtaka hauna kumbukumbu ya makosa ya nyuma dhidi ya mshtakiwa huyo, lakini ameomba mahakama itoe adhabu kali dhidi ya washtakiwa.
“Vitendo vya kudanganya Mamlaka (Idara ya Uhamiaji) vimekuwa vikishamiri kila siku, hivyo naiomba Mahakama yako itoa adhabu kali, ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hii” alidai Mpuya.
Katika kesi ya msingi, shtaka la kwanza linamkabili Mohamed pekee yake, ambalo ni kukutwa na kadi ya mpiga kura, kinyume cha sheria.
Mohamed anadaiwa Juni 21, 2024 katika Bandari ya Dar es Salaam iliyopo wilaya ya Ilala, akiwa raia wa Oman alikutwa na kitambulisho cha mpiga kura chenye namba T-1027-9077-0988-9, kinyume cha sheria.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kukionyesha kitambulisho hicho kwa maofisa wa Uhamiaji, akijifanya kimetolewa na mamlaka husika kwa lengo la kukitumia katika matembezi yake visiwani Zanzibar, wakati akijua kuwa ni kosa kisheria.
Shtaka la pili ni kudanganya maofisa Uhamiaji wakiwa katika majukumu yao, linawakabili washtakiwa wote, ambapo siku na eneo hilo, washtakiwa kwa pamoja waliwadanya maofisa Uhamiaji kwa kumtambulisha Mohamed kuwa ni raia wa Tanzania na kitambulisho chake kimetolewa na mamlaka husika wakati wakijua kuwa ni uongo.
Wakili Mpuya amewasomea hoja za awali, ambapo alidai Mohamed aliingia nchini April 2024 akiwa na hati ya kusafiria yenye namba H 189567 na alipewa visa ya miezi mitatu kuishi nchini.
Pia, amedai Ally ambaye ni raia wa Tanzania anayeishi Oman ndio alikuja na Mohamed hapa nchini, alipanga kumpeleka Mohamed, Visiwani Zanzibar kwa ajili ya matembezi na kwenda kuona ndugu, jamaa na marafiki wa Ally.
Hata hivyo, wakati wanapanga mpango huo wa kwenda Zanzibar, mshtakiwa Ally alimsaidia Mohamed kughushi kitambulisho cha mpiga kura chenye jina la Hatem Mohamed kwa lengo la kukitumia katika matembezi yao huko Zanzibar.
“Akiwa Bandari ya Dar es Salaam katika maandalizi ya kwenda Zanzibar, washtakiwa hao walitiliwa shaka na maofisa wa Uhamiaji, ambapo mshtakiwa kwanza (Ally) alidai kuwa ni Mzanzibar na kutoa kitambulisho chake, huku Mohamed naye akitoa kutambulisho hicho cha kughushi,” amedai Mpuya.
“Maofisa Uhamiaji waliwataka waende ofisi za Bandarj kwa ajili ya mahojiano na wakati wakiendelea na mahojiano, Mohamed alikiri kuwa yeye ni raia wa Oman na aliingia nchini Tanzania kwa ajili ya matembezi akiwa na mwenyeji wake (Ally) na walikuwa wanaelekea Zanzibar kutembelea ndugu, jamaa na marafiki wa Ally,” alidai wakili.