Dar es Salaam. Vilio vya watu kutoweka na kutekwa vimeendelea kuibua hofu na wasiwasi nchini, huku wadau wakiinyooshea kidole Serikali kwa kushindwa kuvikomesha.
Kwa mujibu wa wadau hao wa kada mbalimbali, pia vipo viashiria vya ushiriki vyombo vya dola, ikidaiwa baadhi ya watekaji wanapomchukua mtu hudai wao ni askari, madai ambayo Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni ameyakanusha akisema ni uhalifu kama mwingine.
Ukimya wa mamlaka zinazohusika na hatua dhidi ya watekaji hao ni jambo lingine lililotajwa na wadau hao, kusababisha mashaka zaidi kuhusu wahusika na matukio hayo.
Mashaka hayo yanaibuliwa katika kipindi ambacho kumekuwa na mfululizo wa matukio ya kutoweka kwa watu kutokana na kutekwa katika siku za hivi karibuni.
Edgar Mwakabela maarufu Sativa ni kielelezo cha matukio hayo, alitoweka Juni 23 jijini Dar es Salaam na Juni 27, mwaka huu akapatikana katika Hifadhi ya Katavi akiwa amejeruhiwa.
Kwa mujibu wa maelezo yake, alitekwa na watu wasiojulikana, walimlaza katika karakana ya Polisi Oysterbay kisha wakampeleka Arusha na Katavi alikotupwa porini.
Kijana huyo kwa sasa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Agha Khan jijini Dar es Salaam.
Tukio la Sativa limefuatana na la Kombo Mbwana, mwanachama wa Chadema, Wilaya ya Handeni, Mkoa wa Tanga aliyetoweka Juni 29, mwaka huu na hadi sasa hajaonekana.
Kombo alitoweka baada ya kufuatwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake na kumchukua kwa nguvu kwa mujibu wa mama yake, Hellena Joseph.
Desemba 7, 2023, mfanyabiashara Mussa Mziba naye alitekwa na watu wasiojulikana, akiwa ofisini kwake Mikocheni, Dar es Salaam na hadi sasa hajapatikana.
Mwingine ni Deo Mgassa naye wa Dar es Salaam aliyetekwa Oktoba 14, mwaka jana na kwa mujibu wa ndugu zake, alifuatwa nyumbani na askari wawili kisha wakaondoka naye na hadi sasa hajapatikana.
Kuhusu Mgassa, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne amewahi kusema Jeshi la Polisi halihusiki, isipokuwa nalo linamtafuta kwa kuwa ni mtuhumiwa wa wizi wa kutumia silaha.
Hiyo ni mifano michache kati ya mingi ya watu waliotekwa, wengine wakipatikana hai, wengine hadi sasa haijulikani walipo na wengine imepatikana miili yao.
Vilio vya watu kutoweka ama kutekwa, kwa siku za karibuni vilisikika wakati wa ziara za aliyekuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda katika mikoa Simiyu, Singida, Mwanza, Mara, Mbeya, Rukwa na Kigoma.
Katika ziara hizo, Makonda ambaye sasa ni mkuu wa Mkoa wa Arusha, wananchi waliojitokeza kwenye mikutano walimweleza ndugu zao walivyopotea na kuomwomba awasaidie kupatikana kwao.
Miongoni mwa matukio yaliyoibua gumzo ni lile lililotokea Desemba 26, 2021 katika eneo la Kamata, Kariakoo jijini Dar es Salaam ambapo vijana watano, Tawfiq Mohamed, Self Swala, Edwin Kunambi, Hemed Abas na Rajabu Mdoe walikamatwa na watu waliokuwa wamevalia sare za polisi na hadi leo hawajulikani walipo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Julai 1, 2024, Mwenyekiti wa Shura ya Maimamu, Sheikh Issa Ponda ameyahusisha matukio ya utekaji na mamlaka za Serikali, hasa vyombo vya dola.
Sheikh Ponda amesema kuna viashiria lukuki kwamba matukio hayo, ama yanafanywa na vyombo vya dola au vinahusika nayo kwa namna yoyote.
Akifafanua hoja yake, Sheikh Ponda amesema mara nyingi watekwaji au familia zao, wanapopatikana hueleza walioonekana kutenda matukio hayo, walijitambulisha ni maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Hisia zake hizo haziishii kwenye kujitambulisha pekee, amesema hata wanapofika aghalabu huwa na silaha, magari hasa aina ya Land Cruiser na vitu ambavyo si rahisi kumilikiwa na mtu binafsi.
Kama hiyo haitoshi kwa mujibu wa Sheikh Ponda, wahusika kama inavyosimuliwa na familia zilizowahi kushuhudia ndugu zao wakitekwa, hutekeleza vitendo hivyo bila wasiwasi.
“Nini kinawafanya wajiamini, kwanini wasiogope kukamatwa ni kwa sababu wanajua wao wenyewe ndiyo wakamataji, kwa hiyo wanachokifanya hatatokea wa kuwakamata mwingine,” amesema.
Kutokana na viashiria hivyo, Sheikh Ponda amesema Serikali inapaswa ieleze inapata faida gani vyombo vyake kutenda vitendo hivyo vinavyoweka rehani amani ya wananchi wake.
Hata hivyo, amesema kwa mwenendo uliopo, amesema hakuna dalili inayoonyesha kwamba vitendo hivyo vitakoma, kwa sababu Serikali haijaonyesha utashi wa kujichunguza.
“Serikali kwa namna moja au nyingine inahusika kwenye hali ngumu inayowakuta wananchi, itueleze kuna faida gani kwa watu kutekwa.
“Kama watu hawa ni watuhumiwa mamlaka zipo, zitumike kuwapeleka mahakamani ili hatua zichukuliwe dhidi yao, sio kuwateka,” amesema.
Sheikh Ponda amesema Shura ya Maimamu imeandika kitabu kinachohusisha familia 200 za watu waliotekwa na wakati wa uzinduzi baadhi zilikuwepo na Serikali ilikuwepo, lakini hakuna chochote kilichofanyika kudhibiti matukio hayo.
Si Sheikh Ponda tu mwenye mashaka, Dk Anna Henga, mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), yeye anahoji kwa nini Serikali inaonekana kushindwa kuwajua watekaji wakati ina nguvu na uwezo wa kufanya hivyo.
“Hata kama aliyetekwa hana simu janja, lakini Serikali ina mifumo yake ya kuangalia hali ya usalama hadi ngazi ya chini, hasa vijijini, tena katika mtaa akiingia mtu au mgeni anajulikana,” amesema.
Kwa mkono mrefu ilionao Serikali, Henga amesema ni rahisi kufuatilia mwenendo wa usalama na kuwajua, kadhalika kuwamata wanaohusika na vitendo hivyo.
“Nadhani haijashindikana kuwakamata kwa haraka wanaodaiwa kuhusika na vitendo hivi, kinachotakiwa ni Serikali kuweka kipaumbele zaidi, kwamba mtu anapopotea kuwepo na uharaka wa kumtafuta ili aliyetekwa asipate madhara ya kujeruhiwa,” amesema Henga.
Amesema matukio kama hayo muda mwingine yanakuwa ya kihalifu au kuhusishwa na masuala ya uchaguzi.
Bagonza: Inashangaza sana
Akizungumza na Mwananchi, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza pia ameeleza kushangazwa na Serikali kushindwa kuwakabili watekaji, akirejea tukio la Sativa.
Amesema kwa maelezo ya Sativa, watekaji hao walipita naye kutoka Dar es Salaam hadi Arusha kisha Katavi, imeshindikanaje waliomteka kujulikana licha ya vizuizi vyote vilivyopo barabarani.
“Yaani mtu achukuliwe Dar es Salaam, apelekwe Arusha hadi Katavi na vizuizi vilivyopo barabarani waliombeba wasijulikane,” amehoji.
Pia ameonyesha wasiwasi kwamba imewezekanaje kupatikana haraka kwa waliohusika na mauaji ya mtoto Asimwe Novath mwenye ualbino na ishindikane kwa watekaji.
“Juzi mkoani Kagera aliuawa mtoto mwenye ualbino, Rais akatoa tamko kesho yake ndani ya saa 24 wahusika walipatikana, ebu fikiria? Sasa mengine yanatokea viongozi wanakaa kimya hadi mtu anachukua wiki kuonekana baada ya kutekwa, hapo tueleweni nini,” amehoji Askofu Bagonza.
Akizungumzia hilo, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa amesema umefika wakati Rais Samia aone umuhimu wa kuunda kamati maalumu ya kufanya uchunguzi wa matukio hayo.
Umuhimu wa uamuzi huo, amesema ni kujirudia mara kwa mara kwa aina hiyo ya matukio, ambayo kimsingi yanavunja misingi ya haki ya kuishi.
Hata hivyo, ameeleza iwapo Rais Samia hatafanya hivyo, atarajie kuona matukio ya namna hiyo yakiendelea kwa kuwa wahusika hawatakuwa na hofu ya kuteka.
Licha ya mitazamo hiyo, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema ametangaza kukutana na familia za waliotekwa nyumbani kwake mkoani Arusha.
Akiwa katika mkutano wa hadhara mkoani Tanga, Lema amesema atazungumza na kupata mlo na waathirika hao, kisha atakodisha magari kuwapeleka Ikulu ya Dodoma ili waeleza kilio chao.
Pia Lema amemtaka Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati matukio hayo, la sivyo yana hatari ya kusababisha machafuko siku zijazo.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 1, Waziri Masauni amesema hakuna uwezekano wa vyombo vya ulinzi na usalama kuhusika katika matukio ya utekaji au kutoweka kwa watu yaliyotokea katika siku za karibuni.
Hata hivyo, amesema kauli yake hiyo haimaanishi kwamba hakuna mtumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama anayeweza kujihusisha na matukio hayo, lakini si kwamba Serikali inafanya hivyo.
Akifafanua, amesema kumewahi kutokea uhalifu uliowahusisha watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama na hatua zilichukuliwa dhidi yao.
Kama ilivyofanyika kwa hao waliochukuliwa hatua, amesema ikibainika mtumishi mwingine yeyote anayejihusisha na uhalifu wa aina yeyote, atachukuliwa hatua za kisheria kama inavyotakiwa.
Hata hivyo, Waziri Masauni amezihusisha shutuma dhidi ya Serikali na michakato ya kuelekea uchaguzi, akisema wapo wanasiasa wanaoamua kutafuta kura kwa kuichafua Serikali.
Kwa mujibu wa Masauni, lipo tukio moja la kihalifu lililotokea siku za karibuni ambalo uchunguzi wake upo katika hatua nzuri na mmoja wa watakaofikishwa mahakamani, ni mtu ambaye jamii itathibitisha kwamba Serikali haimvumilii yeyote, hata mtendaji wake anapofanya kosa.
Kuhusu tukio la Sativa, amesema mamlaka husika zinaendelea na uchunguzi na waliohusika watapatikana.