Arusha. Jumla ya watu 32,186 wamehudumiwa katika kambi ya madaktari bingwa na wabobezi iliyokamilika leo Jumatatu Julai mosi, 2024 katika Viwanja vya Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Akitoa tathmini ya kambi hiyo iliyofanyika kwa siku nane, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkombachepa, amesema kati ya watu hao, wapo watoto 4,616 waliohudumiwa katika kambi hiyo.Wanawake walikuwa 19,546 huku wanaume 12,640.
Mkombachepa amesema ugonjwa wa macho ndiyo uliongoza kuwa na wagonjwa wengi ambao ni 9,834 ikifuatiwa na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu walikuwa 2,601.
“Kati ya wagonjwa hao wagonjwa waliopewa rufaa ni 1,820 ambao kati ya hao 1,292 wamepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mt Meru, wengine katika hospitali na taasisi nyingine za kiafya nchini,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Arusha, Paul Makonda, ameshukuru madaktari na wataalamu wa afya zaidi ya 500 waliojitolea kuhudumia wananchi hao waliotoka mikoa mbalimbali nchini.
Makonda amesema kwa waliokuwa wamepewa namba hadi jumamosi Juni 29, 2024 watahakikisha wanapatiwa matibabu wote bila kuwaacha.