TIMU ya Taifa ya Uganda imetwaa ubingwa wa kwanza wa kombe la mpira wa miguu kwa wanawake wasio na makazi Afrika (Afrika Homeless Women’s Cup 2024), baada ya kuichapa Tanzania mabao 6-1 katika mchezo wa fainali.
Ubingwa huo unaipa moja kwa moja nafasi Uganda kushiriki mashindano ya dunia ya wanawake (Homeless World Cup) yatakayofanyika Korea Kusini, Novemba, mwaka huu yakishirikisha zaidi ya timu 64 wanachama wa taasisi ya wanawake wasio na makazi.
Katika mashindano hayo yaliyofanyika kwa siku mbili katika viwanja vya AICC jijini Arusha na kushirikisha nchi nane za Afrika, Tanzania waliokuwa wenyeji wanafikiriwa kuungana na Uganda kuwakilisha Bara hili.
Katika mashindano hayo yaliyofanyika mara ya kwanza nchini mshindi wa tatu aliibuka Kenya baada ya kuichapa Zambia mabao 5-2.
Nchi zingine zilizoshiriki katika mashindano hayo ni Namibia, Malawi, Zimbabwe na Afrika Kusini.
Akizungumza katika mashindano hayo, Mtendaji Mkuu wa Homeless World Cup, James Mcmeekin alisema kuwa mashindano hayo ni ya kwanza kufanyika kwa nchi za Afrika na kuahidi kusapoti nchi zingine kuandaa kila mwaka.
“Kwa mwaka huu Uganda imefanikiwa kuwa chaguao la kwanza kwa nchi za Afrika kuwakilisha kwenye michuano hii, lakini kwa ushindani wa Tanzania tumevutiwa na mpira wao na tutaona namna ya kuwaingiza kwenye ratiba ya kushiriki michuano hiyo ya dunia itakayofanyika Korea Kusini,” alisema Mcmeekin.
Mkurugenzi wa taasisi ya kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya soka Tanzania inayojulikana kwa jina la Future Stars, Alfred Itaeli alisema kama wanachama wa Homeless World Cup wamefurahi kuipatia Tanzania uenyeji wa michuano hiyo.
Alisema lengo la mashindano hayo ni kuwalinda wanawake walio katika mazingira hatarishi dhidi ya Unyonyaji ambayo imetoa fursa kwa Tanzania kujulikana katika ulimwengu wa soka na pia kukuza utalii.
Naye kocha wa Uganda, Nkugwa Stiga alisema ushindi huo ni moja ya malengo ya kukuza michezo kwa nchi ya Uganda na pia kuiwakilisha zaidi Afrika kwenye michuano ya kimataifa.
Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA), Zakayo Mjema alisema mashindano hayo ni uzoefu tosha kuelekea Afcon 2027.