SIMBA inadaiwa ipo katika harakati za kunasa saini ya kiungo wa Asec Mimosas, Josephat Arthur Bada zilizoingia ugumu baada ya Ismaily ya Misri kuingilia kati dili hilo.
Simba ilikuwa ya kwanza kuonyesha nia ya kumtaka Bada aliyemaliza mkataba na Asec, lakini inaelezwa Ismaily imeweka ugumu dili hilo kukamilika baada ya kuweka mkwanja mrefu mezani.
INAELEZWA Kagera Sugar wapo kwenye hatua za mwisho kukamilisha dili la kiungo, Samweli Onditi kutoka Geita Gold ambayo imeshuka daraja msimu uliopita. Kiungo huyo ambaye alikuwa anaitumikia Geita Gold kwa mkopo akitokea Azam FC yupo kwenye mazungumzo ya kusaini mkataba wa miaka miwili baada ya kuwa mchezaji huru.
YANGA Princess inadaiwa kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa TP Mazembe, Sabina Thom kwa mkataba wa mwaka mmoja. Sabina ambaye anacheza pia nafasi ya winga zote mbili aliwahi kucheza Tanzania msimu wa 2021/22 akiitumikia Simba Queens katika Ligi Kuu ya Wanawake.
NYOTA wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga katika timu ya Besiktas ya Uturuki, Opah Clement anatajwa kutaka kujiunga na Club León Femenil inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Mexico. Kama Opah atajiunga na klabu hiyo ataungana na mtanzania mwenzake beki, Juletha Singano anayechezea Juarez.
BAADA ya Simba Queens kubeba viungo wawili kutoka kwa watani wao, Yanga. Upande wao nao wamelipiza kisasi kwa kuwabeba Danai Bhobho raia wa Zimbabwe na Joanitha Ainembabazi (Uganda) ambao wamewapa mikataba ya mwaka mmoja baada ya Simba kuonyesha nia ya kutoendelea nao.
CEASIAA Queens ipo kwenye hatua nzuri ya kumsajili mshambuliaji wa Simba Queens, Koku Kipanga. Huo utakuwa usajili wa pili kwa Ceasiaa kuufanya msimu huu. Timu hiyo na nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu zinajipanga kwa msimu ujao ambao unatarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake kutokana na usajili unaoendelea.
SIMBA Queens na Yanga Princess zimeingia kwenye vita ya kutaka saini ya kiungo wa JKT Queens, Amina Bilal anayemaliza mkataba na klabu hiyo. Yanga ilikuwa ya kwanza kumfuata kiungo huyo na sasa Simba imeingia kati dili hilo ikimtaka mchezaji huyo kwa ajili ya kujiimarisha kutokana na kushiriki pia mashindano ya kimataifa msimu ujao.