Wakenya waandamana kumshinikiza Rais Ruto ajiuzulu – DW – 02.07.2024

Waandishi wa habari wa shirika la habari la Reuters wameshuhudia mapema leo wingu la moshi ya gesi ya kutoa machozi katika barabara kuu katikati ya jiji la Nairobi kabla ya mchana wa leo ambako polisi wa kutuliza ghasia waliokuwa wamevalia kofia za chuma walionekana wakirandaranda tangu asubuhi.

Vituo vya televisheni vya Kenya aidha vimeonyesha picha ya mamia ya waandamanaji wakiwa wanatembea kwa amani. Katika mji wa Mombasa, pwani ya Kenya waandamanaji hao walikuwa wamebeba matawi ya miti, na wengine katika mji wa Kisumu ulioko pembezoni mwa Ziwa Victoria. Kusinimagharibi mwa nchi hiyo kuliko na mji wa Migori, waandamanaji walishuhudiwa wakichoma moto matairi.

Wafuasi kwenye maandamano hayo yasiyo na kiongozi na ambayo kwa kiasi kikubwa yanaratibiwa kupitia mitandao ya kijamii wamekataa miito ya majadiliano iliyotolewa na Rais William Ruto hata baada ya kuutupilia mbali muswada wa fedha uliochochea maandamano hayo.

Maandamano katika jiji la Nairobi nchini Kenya
Maafisa wa polisi wakiwa manamburuta mmoja ya waandamanaji waliokuwa wakipinga mauaji ya raia na muswada wa fedha wa 2024/2025 walioandamana kwa amani nchini Kenya. Picha: Monicah Mwangi /REUTERS

Soma pia:Rais wa Kenya Ruto asaini mswada wa fedha 2023

Makumi ya raia wameuawa kwenye maandamano hayo, huku pia kukishuhudiwa makabiliano baina ya polisi na waandamanaji tangu Juni 18, ambapo wengi miongoni mwao walipigwa risasi na polisi kwenye maandamano yaliyofanyika Jumanne iliyopita wakati baadhi ya waandamanaji walipojaribu kuvamia jengo la bunge ili kuwazuia wabunge kuuidhinisha muswada huo uliokuwa na mapendekezo ya kuongeza kodi.

Wengi wa waandamanaji hii leo wanaonekana kughadhabishwa na vifo hivyo ambavyo kulingana na Tume ya serikali ya Haki za Binaadamu, KNHCR, ni 39. Sasa wanamshinikiza Rais Ruto kujiuzulu.

Soma pia: Ruto: “Sina hatia” na vifo vya waandamanaji

Tume hiyo imelaani vurugu na matumizi ya nguvu kupita kiasi yaliyofanywa dhidi ya waandamanaji, watumishi wa afya, wanasheria na waandishi wa habari.

Hata hivyo, Rais Ruto ametetea hatua za jeshi la polisi akisema walifanya kazi nzuri licha ya kuwa kwenye mazingira magumu.

Related Posts