Mikakati kufikia tani 120,000 za mkonge yabainishwa

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) imeeleza mikakati mbalimbali inayofanywa ili kuhakikisha uzalishaji wa mkonge unafikia tani 120,000 mwaka 2025 kutoka tani 56,000 za sasa.

Ofisa Kilimo wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Emmanuel Lutego (kushoto), akiwasikiliza wateja waliotembelea banda la bodi hiyo kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), Dar es Salaam.

Takwimu zinaonyesha mahitaji ya mkonge duniani ni tani 500,000 lakini zinazozalishwa kwa sasa ni 250,000 huku Tanzania ikiwa ya kwanza kwa kuzalisha mkonge wenye ubora.

Akizungumza Julai Mosi,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba, Ofisa Kilimo wa TSB, Emmanuel Lutego, amesema kwa sasa wakulima zaidi ya 12,000 wanajihusisha na kilimo hicho nchini huku kukiwa na ongezeko la wakulima wadogo wadogo.

“Tunahamasisha wakulima wengi wajiunge kwenye kilimo cha mkonge, tunahamasisha wakulima wadogo, wa kati na wakubwa wapanue ukubwa wa mashamba yao kwa kupanda mkonge mpya ili tuweze kufikia mahitaji ya mkonge duniani na kama nchi kufikia lengo la kuzalisha tani 120,000 au zaidi ya hizo.

“Tumejipanga kuongeza tija ya uzalishaji, kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za mkonge na Serikali imekuwa ikigawa mbegu bure kuhamasisha wakulima wengi wajiunge na kilimo cha mkonge na imeanzisha vituo vya uchakataji kwa wakulima wadogo,” amesema Lutego.

Kwa mujibu wa Lutego, vituo hivyo vya uchakataji vipo katika Wilaya za Handeni, Mkinga na maeneo mengine ambako mwitikio wa wakulima wa mkonge umekuwa mkubwa.

Ametaja fursa zilizopo katika sekta ya mkonge kuwa ni uzalishaji wa mbegu kutokana na mwitikio mkubwa wa wakulima, uwekezaji wa mashamba makubwa, ya kati na madogo, uwekezaji katika mnyororo wa thamani yaani uchakataji wa nyuzi za mkonge na utengenezaji wa bidhaa zinazotokana na mkonge kama kamba, asali, spirit na nyingine.

Ofisa huyo amesema zao la mkonge halitegemei msimu kulinganisha na mazao mengine ambapo mkulima au mfanyabiashara anaweza kuvuna na kuuza wakati wowote katika mwaka na kuwahamasisha wadau wanaotaka kuingia kwenye sekta hiyo kutohofia masoko kwani moja ya jukumu la bodi ni kuwaunganisha wakulima na masoko ya mkonge.

Related Posts