Wasichana 10,100 waliokatisha masomo warejeshwa shule

Dodoma. Jumla ya wasichana 10,100 waliokatiza masomo, wamerejeshwa shuleni nje ya mfumo wa rasmi wa elimu kwa kipindi cha miaka mitatu tangu mwaka 2022 hadi mwaka 2024.

Wengi wa wanafunzi hao ni wale waliokatisha masomo kwa kupata ujauzito na utoro, ambao wamerejeshwa shuleni kupitia vituo vya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, ikiwa ni miaka mitatu  tangu Serikali ilipotoa mwongozo maalumu wa urejeshwaji wa wanafunzi hao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 2, 2024 na Kitengo cha mawasiliano serikalini cha Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi) Dk Charles Msonde.

Dk Msonde alikuwa akifungua kikao cha utekelezaji wa shughuli za elimu maalumu kwenye mikoa na halmashauri kilichowakutanisha maofisa elimu watu wazima ngazi ya mkoa na halmashauri nchi nzima mkoani Morogoro.

Akizungumza, Dk Msonde amesema hatua hiyo ni mafanikio makubwa katika historia ya nchi juu ya uboreshaji wa sekta ya elimu.

Amesema kutokana na hatua hiyo, ndiyo maana Serikali ilielekeza idara zote za elimu zisimame imara kuhakikisha utendaji kazi ngazi na idara mbalimbali unaimarishwa, ili kutekeleza azma ya Serikali kuhakikisha elimu inakuwa imara.

“Ni lazima tuimarishe elimu ya watu wazima, elimu nje ya mfumo rasmi wa elimu, elimu ya msingi na elimu ya sekondari, maana zote hizi ni elimu msingi na zikikaa kwa pamoja, zikiimarika kwa pamoja watoto wakapata ujuzi na watu wazima wakapata ujuzi umahiri unaongezeka ndipo tunaposema sasa elimu imekuwa bora,” amesema.

Amesema mtu yoyote anayetaka kuzitenganisha idara hizo, Serikali itachukua hatua na kwamba hiyo ndiyo sababu ya kufanya kikao hicho na kuwekeana mikakati ya kuwezesha hilo kufanikiwa.

Awali, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Watu Wazima wa Tamisemi, Ernest Hinju amesema pamoja na masuala mengine, pia kikao hicho cha siku nne kitatoa fursa ya washiriki kupata uzoefu kutoka kwa wastaafu na wabobezi wa elimu ya watu wazima na elimu maalumu.

Pia watapata nafasi ya kufahamu mambo mbalimbali kutoka kwa wadau mbalimbali wanaojishughulisha na masuala ya elimu ya watu wazima na elimu maalumu.

Mbali na wasichana waliokatisha masomo kujiunga na elimu nje ya mfumo rasmi, Novemba 24, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan aliruhusu wanafunzi wanaokatiza masomo kwa sababu mbalimbali, ikiwemo ujauzito kurejea shuleni na kuendelea na masomo kwa mfumo rasmi.

Uamuzi huo ulitengua marufuku iliyowekwa na Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli Juni mwaka 2017, ya kutaka wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari waliopata ujauzito kutoruhusiwa kuendelea na masomo kwenye mfumo rasmi wa elimu.

Januari mwaka 2023, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omari Kipanga aliliambia Bunge kuwa katika kipindi cha mwaka 2021 na 2022 wanafunzi wa shule za msingi waliopata ujauzito ni 1,554 na sekondari ni 7,457.

Alisema hadi Januari 2023 wanafunzi waliorejea shuleni baada ya kukatiza masomo kwa sababu ya ujauzito na kuendelea na masomo ya elimu ya sekondari walikuwa ni 1,692.

Related Posts