KOCHA mpya wa Singida Black Stars, Patrick Aussems amejipa wiki tatu hadi nne za kuwasoma wachezaji wake kabla ya kutoa dozi ya mbinu zake katika maandalizi ya msimu ujao ambao anaamini wanaweza kutoa ushindani mbele ya Yanga, Azam, Simba na Coastal Union ambazo zilimaliza msimu uliopita katika nafasi nne za juu.
Mbelgiji huyo ambaye aliwahi kuifundisha Simba, alisema jambo la kwanza kwake katika mpango wa kukifanya kikosi hicho kuwa tishio ni kuwasoma wachezaji wake huku nao wakiwa na jukumu la kusoma falsafa zake.
Kocha huyo anakumbukwa nchini kwa soka safi la kuvutia ambalo Simba ilikuwa ikitandaza kipindi chake huku mashambulizi yakianzia nyuma, alifanya hivyo pia hata alipotua Afrika Kusini na Kenya akiwa na Black Leopards na AFC Leopards.
“Jambo la kwanza ni kufahamiana, mimi kama kocha nina mtindo wangu ambao wachezaji watatakiwa kuujua, tukishakuwa na programu kadhaa za mazoezi tutaona kama kutakuwa na umuhimu wa kuongeza nguvu katika maeneo ambayo tutabaini kama kuna haja ya kufanya hivyo, nimeona Singida ina wachezaji wengi na wenye uwezo,” alisema.
Kuhusu kutoa changamoto ya ushindani kwa vigogo wa ligi hiyo, Aussems ambaye alipachikwa jina la utani la Uchebe wakati akiwa Simba kutokana na staili yake ya ndevu, alisema kila kitu ni hatua kwa hatua lakini mpango wake ni kuifanya Singida Black Stars kuwa moja ya timu tishio katika ligi.
“Tusubiri tuone, nimevutiwa sana na maono ya klabu ndio maana niliamua kufanya uchaguzi wa kurejea tena Tanzania kwa mara nyingine,” alisema.
Aussems aliiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2018/19 na kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo waliondolewa baada ya kufungwa na TP Mazembe kwa jumla ya mabao 4-1 katika mechi mbili walizokutana.