BAADA ya fainali ya mashindano ya kikapu taifa kumalizika na Kigoma kuibuka mabingwa upande wa wanaume, huku Mara ikibeba kwa wanawake, gumzo lililobaki ni namna mastaa wa mchezo huo walivyooyesha ubabe.
Mashindano hayo yalifanyika kuanzia Juni 19 katika viwanja vya Chinangali, Dodoma yalishirikisha nyota na mikoa 18, lakini ni wakali kadhaa walioonyesha mambo makubwa na ya kusisimua wakiacha simulizi nyuma yao.
Mchezaji bora katika mashindano hayo upande wanaume, Amin Mkosa kutoka Kigoma alionyesha umahiri katika kulibeba chama lake hadi fainali akionekana katika kila eneo uwanjani kupora na kushuti mipira.
Mkosa na Noela Renatus wa Mara walioibuka nyota bora walijishindia Sh500,000 kila mmoja.
Kwa upande wa mfungaji bora kwa wanaume aliyechaguliwa alikuwa Tryone Edward wa Kigoma ambaye mitupo yake ya mbali katika nyavu za wapinzani iliwakosha mashabiki, kwani katika kila mchezo hakukosa mitatu mpaka minne.
Mwingine aliyetisha na kuchaguliwa bora ni Jesca Julius wa Mara ambaye kama Tryone alilimiliki vyema dimba la kati katika kila mchezo kuchezesha wenzake na kunyang’anya mipira. Washindi hao kila mmoja alilamba Sh300,000.
Naye Tumaini Ndosi kutoka timu ya Unguja alichaguliwa kuwa mzuiaji bora na katika michezo yote aliyokuwa uwanjani umahiri wake ulionekana kila mashabulizi yalipoelekezwa langoni kwao, ambapo kwa pamoja na Fotius Ngaiza kutoka Dodoma upande wa wanaume walikabidhiwa Sh300,000 kila mmoja.
Akizungumza na Mwanaspoti, mchezaji bora wa mashindano, Mkosa alisema ushindi walioupata ulitokana na juhudi za wachezaji na moto walioanza nao mwaka huu hautapoa..
Unajua fainali ilikuwaje? Timu ya wanaume ya Mkoa wa Kigoma ilibeba ubingwa baada ya kuifumua Dodoma kwa pointi 58-54, ilhali upande wa wanawake Mara iliifumu Unguja kwa pointi 57-56.Â