NMB yavifikia vijiji 1,000 nchini ambavyo havikuwa na huduma za kifedha

*Yajivunia kuwekeza katika teknolojia na mifumo bora

Na Safina Sarwatt, Zanzibar

Vijiji zaidi ya 1,000 ambavyo havijafikiwa na huduma za kibenki zimefanikiwa kupata huduma baada ya Benki ya NMB kupeleka huduma za kifedha.

Akizugumza katika mkutano wa 38 wa ALAT Taifa uliofanyika Visiwani Zanzibar Aprili 23,2024 Afisa Mtendaji Mkuu benki ya NMB, Ruth Zaipuna amesema lengo ni kufungua akanti milioni 1.5.

“Kwa upande wa matawi ya benki yetu ya NMB, takribani tupo katika kila wilaya kwa asilimia 99, na kwa zile halmashauri chache ambazo nazo tunaendelea kuzifanyia kazi kuhakikisha kwamba tunafikisha huduma zetu kwa asilimia 100,” amesema Zaipuna.

Amesema benki imeendelea kushirikiana vyema na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato.

“Tumewekeza katika teknolojia na mifumo bora na rahisi ya kusaidia Serikali katika makusanyo ya mapato na kuwezesha kukusanya zaidi ya Shilingi Trilioni 9.8 kuanzia mwaka 2018, kupitia matawi yetu yapatayo 231, NMB WAKALA, NMB Mkononi, intaneti benki na mifumo yetu mingine,” amesema Zaipuna.

Amesema kuwa Benki ya NMB imekuwa mshirika mkubwa na wa karibu sana kupitia Halmashauri nchini.

Amesema kuwa ushirikiano huo umejikita katika maeneo mbalimbali ikiwemo utoaji wa huduma za kifedha, ukusanyaji wa mapato kwa Halmashauri zote, kuboresha miundombinu ya elimu, afya, kilimo, barabara na kuchangia katika kutunza azingira na vyanzo vya maji.

Amesema lengo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na utoaji wa huduma bora kwa watanzania huku aitaja baadhi ya maeneo ambayo benki imekuwa ikishiriki kuleta maendeleo ya Taifa.

“Katika kipindi cha miaka miwili (2022 – 2023) Benki yetu imetoa kiasi cha zaidi ya Sh Bilioni 7 kwenye sekta ya elimu, afya, mazingira, kilimo na uokoaji kipindi cha maafa katika kutekeleza sera yake ya kurudisha sehemu ya faida kwa jamii,” amesema Zaipuna.

Amesema kwa mwaka jana, waliboresha jengo la wazazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na mpaka sasa tayari Shilingi milioni 350 zimeshatumika.

“Benki yetu imeendelea kufanya vizuri kwa viashiria vyote muhimu vya ki-benki. Mwaka uliopita tuliweka historia kwa kutengeneza faida ya Sh Bilioni 542 baada ya kodi.

“Kutokana na faida na kutambua umuhimu wa kuwa na maendeleo endelevu, Benki ilitangaza rasmi kutenga Sh bilioni 5.4 kwa ajili ya kurejesha kwa jamii (Corporate Social Investment– CSI).

“Tuna programu ya ufadhili wa masomo ya Nuru Yangu Scholarship and Mentorship, ambapo wanafunzi wenye ufaulu mzuri na wanaotoka familia zenye uhitaji, tunawapa ufadhili wa kusoma elimu ya juu,” amesema Zaipuna na kuongeza kuwa:

“Tunalipa gharama zote za msingi ikiwa ni pamoja na ada ya masomo, vifaa vya shule, usafiri, tunawapa kompyuta, bima ya afya na pia kuwapa mafunzo ya vitendo na ushauri, ili kuwajenga kuwa vijana wenye uadilifu na uzalendo kwa nchi yetu mpaka sasa, tuna wanafunzi 130 chini ya program hii na wako wanasoma vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini.

“Katika kushiriki kufanikisha miradi yakimkakati kama ujenzi barabara, madaraja, reli ya kasi (SGR) na mengineyo benki imekua ikitoa masuruhisho na dhamana kwa wakandarasi wandani na wa nje,” amesema.

Zaipuna amefafanua zaidi kuwa benki imetoa dhamana kwa wakandarasi zaidi ya 580 waonatekeleza miradi ya TARURA yenye thamani ya Sh Bilioni 49 kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa miundombinu.

Aidha, benki pia imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuzihudumia sekta zote na kwa zile zakimkakati kwa kuongeza nguvu kubwa zaidi.

“Kwa mfano sekta ya kilimo tumeongeza mikopo kutoka Bilioni 557 mwaka 2020 mpaka Trilioni 1.6 mwaka 2023, na hivyo hivyo kwa sekta kama za nishati, uzalishaji na biashara.

“Benki inaendelea kuongeza Ujumuishwaji wa Watanzania wengi zaidi, kwenye Sekta rasmi ya Kifedha, hasa Watanzania wenzetu walioko vijijini.

“Kupitia huduma yetu mpya ya NMB Pesa, tumerahisisha masharti ya kufungua akaunti hii, ambapo kwa Sh 1,000, Mtanzania naweza kufungua akaunti na haina makato ya mwezi, huku mteja akipewa uwezo wa kujiunga na NMB Mkononi kurahisisha miamala yake,” amesema Zaipuna.

Amesema baada ya kujenga miamala, Mteja atakuwa na uwezo wa kukopa hadi Sh laki tano kwa simu, bila kufika tawini, kwa kutumia huduma ya MshikoFasta.

“Benki yetu ya NMB imeendelea kuwa mshirika wa kimkakati kwa Serikali kwenye maeneo mbalimbali kwa mfano, kwa kipindi cha ya miaka nane tumelipa kodi ya zaidi ya shilingi Trilioni 1.8.

“Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitutambua kama Mshindi wa Jumla Kitaifa; kama Mlipa Kodi bora na Mkubwa zaidi Tanzania (Sekta zote), hii ikiwa ni mara ya pili na Taasisi Bora inayolipa Kodi kwa hiari kwa kuzingatia misingi na kanuni bora za ulipaji kodi (yaani Most Compliant Tax Payer) na Mshindi wa Kwanza; Mlipa Kodi Mkubwa Zaidi katika Kundi la Taasisi za Fedha nchini (mara ya tatu mfululizo),amesema Zaipuna.

“Naomba nianze kwa kukupongeza kwa kazi kubwa unayoifanya kulijenga taifa letu na juhudi za Serikali yako za kuwaletea wananchi wa Tanzania maendeleo na kwa keundelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara ikiwemo taasisi za fedha,”amesema Ruth .

Afisa Mtendaji Mkuu huyo pia ametumia fursa hiyo kuushukuru uongozi wa ALAT kuialika Benki ya NMB na kuwa Mdhamini Mkuu katika mkutano huu wa 38 wa ALAT.

“Ni heshima kubwa sana kwangu na kwa Benki ya NMB kusimama mbele ya wajumbe zaidi ya 500 kutoka katika Halmashauri zote 184 Tanzania Bara na Halmashauri 11 toka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (7-Unguja na 4-Pemba) na Waheshimiwa wabunge ambao ni wajumbe wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa (ALAT) pamoja na wadau wengine wa maendeleo,” amesema.

“Aidha tulishuhudia uzinduzi wa ZALGA (Zanzibar Association of Local Government Authorities) hapa Zanzibar, chombo ambacho kina majukumu sawa na ALAT kwa hapa Zanzibar na kwamba ni namna ya pekee niwapongeze ZALGA ikiongozwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Zanzibar-Mwenyekiti, kwa kufanikisha uzinduzi huu,Benki yetu kama mshirika wa karibu, tunaahidi kushirikiana na chombo hiki ili kutimiza malengo ya uanzishwaji wake,” amesema Zaipuna.

Related Posts