MOI yapokea majeruhi 700 kwa mwezi, bodaboda zaongoza

Dar es Salaam. Taasisi ya Tiba na Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI), imesema inapokea takribani majeruhi wa ajali za barabarani 700 kwa mwezi.

Kati ya majeruhi hao, asilimia 60 ambayo ni sawa na wajeruhi sita kati ya 10 wanatokana na ajali zinazohusiana na pikipiki maarufu kama bodaboda.

Takwimu hizo zimetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa MOI, Dk Lemeri Mchome leo Jumanne, Julai 2, 2024 hospitalini hapo, wakati akipokea msaada wa fedha pamoja na viti mwendo kutoka kampuni ya Watu Credit.

“Kwa kiwango kikubwa wagonjwa wengi wana uhusiano wa moja kwa moja na ajali za pikipiki aidha walikuwa abiria, dereva wa bajaji au gari limepata ajali kwa sababu lilikuwa linakwepa bodaboda au bajaji,” amesema Dk Mchome.

Amesema asilimia 75 ya majeruhi hao hawana ndugu na hawana msaada wa kifedha kugharamia matibabu kwa kuwa ajali zikitokea wanaletwa na raia wema pamoja na askari wa usalama barabarani.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya MOI, Dk Lemeri Mchome, akipokea msaada wa viti mwendo kutoka kampuni ya Watu Credit Limited leo Jumanne Julai 2, 2024 ambapo mbali ya yote ametoa takwimu za wagonjwa wa majeruhi wa ajali za pikipiki.

“Asilimia 25 iliyobakia ni vijana ambao hawana ndugu kabisa, walikuja mjijni kutafuta kipato. Tunakaa nao kwa zaidi ya miezi mitatu, gharama zinaongezeka,” ameeleza Dk Mchome.

Pia amesema wengi wao wanaumia vichwani, huku asilimia 75 wanaumia mikono na miguu: “Uhitaji wa vifaa ni kwa wale wagonjwa waliovunjika migongo na mifupa mikubwa, ndio tunawaomba wadau waje kuwasaidia.”

Hivyo, amesema kutokana na Sera ya Afya, Wizara inawagharamia matibabu, lakini baadaye ndugu wakijitokeza wanaombwa kuchangia matibabu hayo.

Dk Mchome ametoa rai kwa waendesha vyombo vya usafiri kubadili tabia zao na kuwa makini barabarani kwa kufuata sheria, kanuni na alama zilizopo.

“Katika jitihada za kupunguza ajali za barabarani tunashirikiana na wenzetu kwa kuingia makubaliano na Chuo cha Usafirishaji NIT kwa ajili ya kuhakikisha madereva wanapata mafundisho na tafiti zinazofanyika hospitali zinazotokana na ajali.

“Pia, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mnyororo huu wote ili kupunguza ajali za barabarani,” amebainisha.

Pamoja na hayo, ameishukuru kampuni ya Watu Credit kwa msaada huo ambao utawawezesha wagonjwa 13 kufanyiwa upasuaji pamoja na kupata viti mwendo. Ameomba wadau wengine kujitokeza kusaidia wagonjwa hao wanaohitaji msaada.

Kwa upande wake, Meneja Seuri Kuoko ambaye ni Meneja Mkuu Msaidizi wa Kampuni hiyo ya Watu Credit Tanzania Limited inayokopesha Watanzania ikiwemo pikipiki za miguu miwili na mitatu, amesema msaada huo utawawezesha wagonjwa hao kurudi katika hali yao ya kawaida kama ilivyo lengo lao.

“Lengo kubwa zaidi ni kuboresha huduma za afya kwa kuwasaidia wagonjwa waliotokana na ajali za vyombo vya moto. Msaada huu ni karibu Sh7 milioni ambapo miongoni kuna nepi za watu wazima na viti mwendo,” amebainisha Kuoko.

Hata hivyo, Daktari Bingwa Mbobezi wa Mifupa MOI, Dk Joseph Mwanga wakati akielezea matukio yanayohusisha majeruhi wa pikipiki wanaopokelewa kwenye taasisi hiyo Januari 9, 2024 alisema”

“Ajali hizi za pikipiki zinaongoza kusababisha majeruhi na wanaume ndilo kundi linaloathirika zaidi kwa asilimia 70, majeruhi wengi wa bodaboda hupata mivunjiko mikubwa ya mifupa, hali inayochangia ukubwa wa gharama za matibabu,” amesema.

Dk Mwaga alisema kwa miaka 18 iliyopita, kitengo cha dharura cha MOI kilikuwa kinapokea majeruhi watatu hadi watano kwa siku, ukilinganisha na sasa ambapo majeruhi ni kati 20 hadi 25 kwa siku.

Related Posts