Rais Samia Suluhu Hassan amesema yeye binafsi atabeba gharama zote za matibabu ya kijana Edgar Mwakabela, maarufu kama Sativa anayedaiwa kutekwa, kuteswa na kutupwa katika pori la Hifadhi ya Katavi akiwa na majeraha mbalimbali mwilini. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Sativa ambaye anaendelea na matibabu katika hospitali ya Aga Khan kuanzia usiku wa tarehe 30 Juni mwaka huu, alidaiwa kutoweka tarehe 23 Juni mwaka huu na kupatikana tarehe 27 Juni mwaka huu katika pori hilo.
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne na Kiongozi wa zamani wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema amezungumza na Rais Samia kwa njia ya simu na kumhakikishia kwamba atagharamia matibabu kuanzia sasa mpaka atakapopona kabisa, pamoja na kuhakikisha unafanyika uchunguzi wa jambo hili.
Zitto amesema amechukua uamuzi wa kumpigia Rais Samia simu baada ya kumtembea Sativa hospitalini hapo na kuzungumza naye pamoja na ndugu zake.
“Mara baada ya kutoka hospitali, nilifanya jitihada za kumtafuta Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuzungumza naye, kumuelezea tukio la Sativa kutekwa,
kupigwa risasi, na kutupwa msituni Katavi, pamoja na matukio mengine ya watu kupotea, ambayo yamekithiri katika siku za karibuni.
“Nimemueleza, yeye kama Rais na Amiri Jeshi Mkuu anao wajibu wa kulinda usalama wa raia, na kwamba matukio ya namna hii yanachafua taswira na haiba yake, na yanaondoa murua wa R Nne zake (4R’s).
“Nimemnasihi Rais juu ya umuhimu wa yeye binafsi kuagiza ufanyike uchunguzi wa vyombo vya ulinzi na usalama juu ya tukio hili pamoja na mengine ya namna hii,” amesema.
Zitto amesema kama Taifa, kunahitajika ushirikiano pamoja kukomesha mambo ya watu kutekwa, kuuawa, kupigwa na kutupwa misituni.
Amesema kwa kuwa Rais Samia amesikiliza, na ameahidi kufanyia kazi ushauri wangu kwake, anamshukuru kwa mwanzo huo.
“Kila safari ndefu, inaanza na hatua ya kwanza. Naamini sasa tutaanza safari ya kwenda kule tunakotaka, ambako tabia za kutekana na kutesana zitakomeshwa,” amesema Zitto.