Rais Nyusi aanza ziara ya siku tatu nchini Tanzania – DW – 02.07.2024

Rais Filipe Nyusi yuko katika ziara ya siku tatu nchini Tanzania, ambapo amemweleza mwenyeji wake Rais Samia ya kwamba makundi yaliyodhibitiwa ni yale ya kigaidi yaliyokuwa yakidhibiti eneo la kaskazini mwa Msumbiji.

Ziara hiyo ambayo kwa sehemu kubwa inahusiana na masuala ya kibiashara na uwekezaji, imetumika kutoa picha ya hali halisi ya hali ya usalama katika eneo la Cabo Delgado ambalo tangu mwaka 2021 liliandamwa na mapigano baina ya makundi ya kigaidi.

Rais Nyusi amesema kupelekwa kwa vikosi vya Tanzania chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC), kumetokana na kuwepo kwa makundi ya wapiganaji wenye mafungamano na kundi la kigaidi la al Qaeda.

Amesema hali kwa sasa ni shwari katika eneo hilo kiasi cha kuwafanya baadhi ya wananchi waliyoyakimbia makazi yao kuanza kurejea wakiwa na matumaini mapya.

Soma pia: Rais Nyusi asema mji mwingine umevamiwa na wanamgambo

Mosambik Soldaten
Baadhi ya wanajeshi wa kulinda amani wakifanya doria karibu na hoteli ya Amarula Palma katika jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji, Agosti 15, 2021. Picha: Marc Hoogsteyns/AP Photo/picture alliance

Nyusi amesema “Watu waliharibiwa maisha yao kutokana na ugaidi, lakini mchango wa SAMIM, ambapo Tanzania imekuwa sehemu yake, tumeona matokeo.”  

Nyusi asisitiza umuhimu wa kutumia vikosi vya kikanda

Mbali na hilo Rais huyo ambaye baadaye mwaka huu anamaliza muhula wake wa pili madarakani, amekumbusha umuhimu wa kutumia vikosi vinavyoundwa na nchi za Kiafrika kwa ajili ya kushughulikia mizozo inayolikumba bara hili.

Kwa upande wake, Rais Samia ambaye nchi yake inachangia vikosi vinavyoundwa na nchi za SADC amesema kurejea kwa hali ya utulivu katika eneo hilo ni habari njema na kwamba hatua hiyo ni muhimu kwa mustakabali wa wananchi wa taifa hilo na jirani yake Tanzania.

“Tumekubaliana kuanzisha ulinzi na usalama kwenye mpaka ili kukabiliana na changamoto zilizopo za uharamia.” 

Ziara ya Rais Nyusi aliyewasili nchini siku ya Jumatatu inalenga kuimarisha ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji na masuala mengine kama ukuzaji mahusiano ya kidiplomasia na kisiasa kwa mataifa hayo mawili.

Licha ya kuwa na historia ya mashirikiano ya muda mrefu tangu enzi za kupigania uhuru, bado kiwango cha biashara na uwekezaji kwa pande zote mbili hakijawa cha kuridhisha. Mwaka 2022 kiwango cha biashara baina ya mataifa hayo kilifikia dola za Marekani milioni 57.8.

Related Posts