Arusha. Mahakama ya Rufani imebatilisha hukumu ya kunyongwa hadi kufa aliyohukumiwa Chipukizi Chondi, mkazi wa Kigoma kwa kosa la mauaji na sasa atatumikia kifungo cha miaka 15 jela kwa kosa la kuua bila kukusudia.
Mahakama hiyo imesema imezingatia ushahidi wa mazingira kuhusiana na mauaji katika shauri hilo, hivyo imemhukumu kifungo hicho kilichoanza kuhesabiwa tangu alipotiwa hatiani, Julai 9, 2022.
Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, ilimhukumu adhabu hiyo Chipukizi na wenzake wawili ambao si warufani, baada ya kushtakiwa katika kesi ya mauaji namba 3/2022 kwa tuhuma za mauaji ya Magezi Kagwesihire.
Mahakama hiyo iliwahukumu mrufani huyo na mwenzake mmoja kunyongwa hadi kufa, huku mshtakiwa wa pili aliyekuwa mke wa pili wa marehemu Kagwesihire akihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa kutiwa hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia.
Rufaa hiyo ya jinai namba 466/2022 ilisikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na Jaji Mwanaisha Kwariko, Zephrine Galeba na Dk Benhajj Shabaan Masoud ambao walitoa uamuzi huo Juni 28, 2024.
Katika kesi ya msingi, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi 10 na vielelezo 10.
Ilielezwa mrufani na mshtakiwa wa pili (mke wa pili wa Kagwesihire) walikuwa na uhusiano wa kimapenzi kwa muda mrefu na siku ya tukio walipanga kukutana nyumbani kwa mshtakiwa wa pili.
Baada ya kukutana kwa lengo la kufanya mapenzi kama walivyokubaliana, Kagwesihire alifika nyumbani hapo, ndipo Chondi akakusanya nguo zake na kukimbilia chumba walichokuwa wamelala watoto ambako pia alikuwemo shahidi wa tatu.
Baada ya Chondi kukimbia, mshtakiwa wa pili alimfungulia mlango Kagwesihire, kisha wakaenda kulala, huku akidhani mrufani angetoka, hivyo aliacha mlango bila kuufunga na kufuli.
Kinyume chake, Chondi aliingia ndani ya chumba alichokuwamo Kagwesihire na mshtakiwa wa pili, ndipo ukazuka ugomvi mkali kati ya mrufani na marehemu. Kutokana na hali hiyo, Chondi alimnyonga na kumshambulia Kagwesihire kwa panga.
Baada ya kutekeleza mauaji hayo, alitoa mwili huo ndani na kuutupa kwenye shamba la migomba na kuoondoka ambapo mwili huo ulipatikana siku tatu baadaye, baada ya kufuatilia, upekuzi ulifanyika ndani ya chumba cha marehemu na kukutwa damu ikiwa imetapakaa.
Mshitakiwa wa pili aliwekwa chini ya ulinzi baada ya kushukiwa kuhusika na mauaji hayo na alipopelekwa polisi alikiri mrufani kuhusika na mauaji hayo.
Mbali na kukiri kosa hilo lililomhusisha mrufani, kulikuwa na ushahidi wa mtoto mwenye umri wa miaka 10, ambaye alidai siku ya tukio alishuhudia mrufani akiingia ndani ya nyumba hiyo, ila hakuona akitoka.
Shahidi huyo ambaye ni mtoto wa marehemu, alidai akiwa bado macho chumbani kwake, alimsikia baba yake (marehemu) akiugulia na kulalamika kuwa mrufani anamuua na kuwa alisikia mzozo mkali kati ya mrufani na marehemu uliochukua muda mrefu.
Ushahidi wa daktari aliyeufanyia mwili uchunguzi Juni 25, 2021 alieleza mahakama kuwa mwili ulikuwa na majeraha mawili ya kukatwa chini ya taya ambayo yalikwenda hadi kwenye mfupa, sehemu ya mbele ya shingo kukatwa na sababu ya kifo ni kutokwa damu nyingi.
Akijitetea mrufani alikuwa na mashahidi wengine wawili ambapo mbali na ushahidi wa mrufani, ushahidi wa mshtakiwa wa pili ulikubaliana na ushahidi wa upande wa mashtaka.
Ushahidi huo ulidai ugomvi uliozuka chumbani na kusababisha mapigano kati ya marehemu na mrufani, ulisababisha amnyonge marehemu na kuwa mshtakiwa wa pili alikimbilia sebuleni na mtoto wake, aliporejea chumbani alimkuta mrufani akimkatakata marehemu.
Aidha, tofauti pekee kati ya ushahidi wa mshtakiwa wa pili na upande wa mashtaka, ni jinsi mrufani alivyopata panga alilotumia kumshambulia marehemu. Mshtakiwa wa pili wakati wa kuhojiwa alikana kumpa mrufani panga hilo.
Akijitetea, mshtakiwa huyo alikana kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mshtakiwa wa pili, huku mashahidi wake wawili wakiunga mkono kuwa siku ya tukio alikuwa nyumbani kwake.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma ilimkuta mrufani na hatia ya mauaji na iliegemea ungamo la mshtakiwa wa pili na mashahidi wengine wa upande wa mashtaka.
Katika rufaa, mrufani huyo aliwakilishwa na Wakili Eliutha Kivyiro, huku mjibu rufaa akiwakilishwa na mawakili wawili, wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Shaban Masanja.
Katika rufaa hiyo mrufani alikuwa na sababu tano na wakati wa kuziwasilisha aliacha sababu mbili zilizokuwa kwenye hati ya rufaa.
Sababu alizotumia kuunga mkono rufaa yake ilikuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha bila kuacha shaka yoyote, hivyo ilikosea kumtia hatiani mrufani kutokana na kukiri kwa mshtakiwa wa pili bila uthibitisho.
Kuhusu hoja ya pili, alidai ungamo la mshtakiwa wa pili halikuthibitishwa na shahidi yeyote wa upande wa mashtaka.
Hoja ya tatu ilikuwa utofauti wa ushahidi kati ya shahidi wa tatu wa mashtaka na mrufani ambaye anadaiwa kuonwa na mtoto wa marehemu, hivyo kutofautiana na madai kuwa mrufani alikimbilia kwenye chumba cha watoto.
Wakili Masanja, aliieleza mahakama kuwa ushahidi wa mashtaka, ikiwemo wa kimazingira ulithibitisha kosa hilo bila kucha shaka, ikiwemo ushahidi wa mtoto aliyemuona akiingia ndani ya nyumba yao. Pia alimsikia marehemu akilalamika kuwa mrufani alikuwa anamuua.
Kingine alidai ni mwili wa marehemu kukutwa umetupwa baada ya kuburuzwa kutoka chumbani kwa marehemu kama ilivyothibitishwa pia na mshtakiwa wa pili na wa tano.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, jopo la majaji walieleza hawakupata chochote kilichorejelewa na wakili wa mrufani kilichoruhusu kutilia shaka ushahidi wa shahidi wa tatu aliyeeleza mrufani alikwenda nyumbani kwao siku ya tukio.
Kuhusu endapo mshtakiwa wa pili alimpa panga mrufani na kumkata nalo marehemu, utata unaodaiwa haupingi ukweli ni kwamba mrufani alikuwa eneo la uhalifu na alihusika na kifo cha marehemu.
“Katika uchunguzi wetu wa ushahidi uliotajwa hapo juu kama mahakama ya awali, hatukupata chochote kwenye rekodi mbele yetu kinachotufanya tuwe na makosa katika uamuzi wa mahakama hiyo kuwa mrufani alikuwa eneo la tukio siku ya kifo cha marehemu.
“Tumeridhika kwamba ushahidi wa upande wa mashtaka ulioonyeshwa hapo juu unathibitishwa na vielelezo vya saba na tisa, ambavyo mshtakiwa wa pili alivirekodi na ambavyo havikuambatana tu na ushahidi wa shahidi wa tatu, bali pia havikupingwa na mrufani,” walisema.
Katika kutatua sababu mbili za rufaa za awali, majaji hao walieleza ni msimamo wao kwamba malalamiko yaliyotolewa katika misingi tajwa, hayana mashiko hivyo wanayaondoa.
Walieleza kwa kuwa wamejiridhisha kwamba mrufani ndiye aliyehusika na kifo cha marehemu na swali linalofuata na linalogusa msingi wa mwisho wa kukata rufaa ni iwapo mauaji hayo yalifanywa kwa nia mbaya na kusababisha mauaji.
“Kwa mujibu wa kumbukumbu iliyo mbele yetu, hakuna upande wowote uliopinga au kubishana katika kesi hiyo unathibitisha kuwa ugomvi huo ulichukua muda mrefu, uliishia kupigana na kusababisha mauaji ya marehemu,” walieleza majaji hao.
Walieleza kwa upande wao, wanadhani mahakama hiyo ya awali, ingefikia hitimisho kwamba mauaji hayo hayakuwa ya makusudi, kwani yalitokana na ugomvi huo.
Walieleza kwa kuzingatia ushahidi wa rekodi ya rufaa, wahitimisha kwamba kifo cha marehemu kilitokea wakati wa kupigana na mrufani na kuwa kwa sababu ni sheria iliyotungwa kwamba, kifo kinachotokana na mapigano au kwa sababu ya uchochezi, si mauaji bali kuua bila kukusudia.
“Tunaruhusu rufaa kubatilisha hukumu ya mauaji na kuibadilisha na hatia ya kuua bila kukusudia. Kwa hiyo, tunatengua hukumu ya kifo kwa kunyongwa iliyotolewa kwa mrufani,” walieleza.
“Kwa kuzingatia mazingira yanayohusiana na mauaji na muda ambao mrufani amekuwa rumande, tunamhukumu kifungo cha miaka 15 ambacho kitaanza tarehe aliyotiwa hatiani,” walihitimisha.