Mke asimulia wasiojulikana walivyomteka mumewe

Handeni. “Niliamka asubuhi nikaanza kufanya usafi, akaja mtu mmoja akawa anazunguka hapa nyumbani kwetu, tukasalimiana, akaniuliza “huu msingi (wa nyumba) anayepandisha ni nani”? Nikajibu mama na mume wangu wanajenga hapa, akataka kuniuliza maswali zaidi, nikamwambia anisubiri nimuite mhusika.

“Nikaingia ndani nikamwambia mume wangu kuna mtu yupo nje nimemuona anazungukazunguka hapa nyumbani, ila simfahamu lakini anaulizia msingi unaojengwa ni wa nani, kamsikilize. Ndipo mume wangu akatoka nje na huo ndiyo ulikuwa mwisho wa kuongea naye.”

Ndivyo Mariam Rajabu (20) anavyoanza kusimulia jinsi alivyoshuhudia mumewe, Kombo Mbwana, kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akichukuliwa na watu wasiojulikana Jumamosi Juni, 15, 2024 akiwa nyumbani kwake, Kijiji cha Komsala, Kata ya Kwamatuku, Handeni Mkoa wa Tanga.

Anasema baada ya kumweleza alichokuwa anahoji mtu huyo, Mbwana alitoka kwenda kumsikiliza.

Mariamu anasema katika mazungumzo yao, alimsikia mtu huyo akimwambia mumewe kuwa eneo hilo ameuziwa yeye tayari na ni shamba la ekari tatu, kama atahitaji kuona nyaraka, waende kwenye gari lililokuwa limeegeshwa jirani na nyumba yao akazione.

“Basi wakaondoka kuelekea kwenye gari huku wakionyeshana eneo na alipoingia tu kwenye gari, nilishtuka kuona gari hilo linaondoka kwa kasi. Ndiyo mpaka leo sijamuona tena mume wangu na sijui chochote kumuhusu yeye na hakuna mawasiliano,” anasimulia Mariam mwenye mtoto mmoja.

Anasema bado anajiuliza nini kimempata mumewe na sababu ya kuchukuliwa kwake.

“Hivi sasa naishi kwa shida sana, yeye ndiyo nilikuwa namtegemea kwa kila kitu,” anasema dada huyo.

Anasema licha ya kuwa ya shemeji yake kumsaidia mahitaji madogo madogo, bado hali si nzuri, kuna siku hulazimika kupata milo miwili tu asubuhi na jioni kwa kuwa chakula hakitoshi.

“Naiomba Serikali imtafute mume wangu wapi alipo nijue, nina mtoto mdogo ambaye anahitaji huduma nyingi na baba yake, ndiyo alikuwa kila kitu,” amesema Mariamu.

Kombo Mbwana mkazi wa kijiji cha Komsala kata ya Kwamatuku wilaya ya Handeni ambae ni kada wa Chadema anayedaiwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana tangu Juni 15,2024.

Akizungumzia hilo, Mark Sango (20) mdogo wake Mbwana pia ameiomba Serikali kuongeza nguvu ya kumtafuta yake yake.

“Hatujui hawa watekaji wanania gani, je ndugu yetu bado mzima au kuna kitu wamemfanya, familia nzima hatuna amani,” amesema Sango.

Amesema licha ya kuendelea kumsaidia shemeji yake kupata mahitaji muhimu, hali si nzuri kwa sababu hana kipato.

“Baada ya kaka kuchukuliwa majukumu yake tunayabeba na sisi, licha ya kwamba sina uwezo wa kuyabeba kama kaka mwenyewe, lakini inanibidi nipambane, tuna mtoto mdogo hapa, lazima nimsaide shemeji,” anasema Sango.

Akisimulia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Komsala, Joseph Minango amesema hana taarifa kama shamba la Mbwana limeuzwa kama ilivyodaiwa na mtu aliyeondoka naye.

“Ninachofahamu mimi na ofisi yangu, eneo hilo ni mali ya Mbwana, labda kama kuna mauziano yalifanyika zamani kabla ya mimi sijaingia madarakani. Lakini cha kujiuliza kwa nini wameondoka naye na hajarudi mpaka sasa,” amehoji Minango.

Amesema wao kama serikali ya kijiji wanaendelea kufuatilia kwa karibu tukio hilo ambalo tayari lilisharipotiwa kwa Jeshi la Polisi.

Awali akielezea tukio hilo, katibu wa Chadema Jimbo la Handeni Mjini, Kombo Matulu alisema wamefuatilia sehemu mbalimbali lakini hawajapata majibu yupo wapi.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando amesema tukio hilo lipo kwenye uchunguzi chini ya Jeshi la Polisi na amewaomba wanafamilia na wananchi kuwa watulivu wakati Serikali ikilishughulikia.

“Serikali haijawahi kushindwa jambo, nawaomba tuwe watlivu,” amesema Msando.

Vilio vya watu kutoweka na kutekwa vimeendelea kuibua hofu na wasiwasi nchini, huku wadau wakiinyooshea kidole Serikali kwa kushindwa kuvikomesha.

Kwa mujibu wa wadau hao wa kada mbalimbali, pia vipo viashiria vya ushiriki vyombo vya dola, ikidaiwa baadhi ya watekaji wanapomchukua mtu hudai wao ni askari, madai ambayo Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Yusuf Masauni ameyakanusha akisema ni uhalifu kama mwingine.

Related Posts