Rais Samia amchangia Sativa Sh35 milioni

Dar es Salaam. Wakati Mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam, Edgar Mwakabela maarufu kama Sativa akiendelea na matibabu aliyoyapata baada ya kutekwa, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa miongoni mwa waliojitokeza kumchangia Sh35 milioni za matibabu.

Taarifa za mchango huo zimetolewa kupitia ujumbe uliochapishwa na Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa alimshukuru Rais Samia kwa mchango huo, ikiwa saa chache baada ya Zitto Kabwe, kiongozi mstaafu wa ACT Wazalengo kusema amezungumza na mkuu wa nchi na kumsihi aagize uchunguzi wa suala hilo, huku yeye akiahidi kubeba gharama za matibabu hayo.

Hata hivyo, jitihada za kumpata Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga kujua undani wa mchango huo na mazungumzo ya Rais na Zitto yalivyokuwa, hazikuzaa matunda.

Madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi wakati wakimtibu Edgar Mwakabela, maarufu Sativa.

Satavi aliyetoweka Juni 23, 2024 jijini Dar es Salaam na kupatikana Juni 27, 2024 katika Hifadhi ya Katavi akiwa na majeraha maeneo mbalimbali ya mwili, anapatiwa matibabu hayo katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa majeraha aliyonayo ni mpasuko wa taya ambalo baadhi ya mifupa inaonekana na mipasuko midogo.

Kupotea kwake kuliibua mijadala katika mitandao ya kijamii na kampeni za kupaza sauti ili apatikane zilitanda mitandaoni.

Alipopatikana kampeni ya kumchangia fedha za matibabu ziliendeshwa na watu mbalimbali walijitokeza kumchangia, waratibu wa matibabu hayo wakiwa Martin Masese na meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob.

Jana, Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe alikwenda kumtembelea Sativa hospitalini. Alipotoka alizungumza na wanadishi wa habari na kusema, baada ya kumwona mgonjwa, alimtafuta Rais Samia Suluhu Hassan.

“Jitihada za kumtafuta Rais, ni kuzungumza naye kumwelezea tukio la Sativa kutekwa, kupigwa risasi na kutupwa msituni Katavi, pamoja na matukio ya watu kupotea, ambayo yamekithiri katika siku za karibuni,” amesema Zitto na kuongeza:

“Nimenasihi ndugu Rais juu ya umuhimu wa yeye binafsi kuagiza ufanyike uchunguzi wa vyombo vya ulinzi na usalama juu ya tukio hili pamoja na mengine ya namna hii. Rais amenisikiliza na ameahidi kufanyia kazi ushauri wangu kwake,” amesema Zitto.

Kiongozi mstaafu wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe akizungumza na Edgar Mwakabela maarufu Sativa anayepatiwa matibabu katika hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam.Picha na Mpiga picha wetu

Baadaye mchana leo Julai 2, Ole Ngurumwa amechapisha ameweka ujumbe wa shukurani kwa Rais Samia kwa mchango wake.

Ujumbe huo ameuweka kwenye akaunti yake ya kijamii ya X (zamani Twitter) ukisema: “Tunatoa shukran za dhati kwa Mhe Mama Samia, kwa kutimiza ahadi na kulipia gharama za awali za upasuji mkubwa wa ndugu Sativa, tumepokea nakala ya malipo kiasi cha Sh35 milioni kwenda Hosptali ya Aga Khan.

“Leo jioni Sativa atafanyiwa upasuaji. Hizi ni gharama za awali, tuombe kila kitu kiende sawa na gharama zisiwe kubwa huko mbele. Kuna faida kubwa kwa Mhe Rais kuweka mkono wake katika hili. Hii ni salamu kwa walioko nyuma ya suala hili.

“Pili tunaamini pia ushauri wetu wa tume huru atafanyia kazi. Kama mzazi na mama suala hili pia limemgusa. Asante pia Mhe ZItto kwa jitihada zako.

“Tunashukuru sana Boni na MMM (martini) pamoja na wananchi wote online (mtandaoni) kwa kujitoa pia kwa hali na mali katika suala hili. Sote tuungane kulinda uhai wa mmoja wetu unapokuwa mashakani,” ameandika Olengurumwa.

Related Posts