Ujerumani kuwalipa fidia maelfu ya waathirika walio hai – DW – 02.07.2024

Kansela Olaf Scholz amesema Ujerumani inamipango ya kutoa msaada kwa walionusurika ukatili uliotokana na ukaliaji kwa mabavu wa utawala wa Wanazi nchini Poland wakati wa vita vya pili vya dunia.

Kiongozi huyo wa Ujerumani ametoa ahadi hiyo akiwa katika ziara nchini Poland ambako yanafanyika mazungumzo ya pamoja kati ya serikali za mataifa hayo mawili jirani.

Kansela Olaf Scholz amefanya mazungumzo na waziri mkuu wa Poland Donald Tusk mjini Warsaw na baadae wakazungumza na waandishi wa habari katika  mkutano wa pamoja, ambapo  kiongozi huyo wa Ujerumani alibaini kwamba nchi yake inatambuwa ukubwa wa dhambi iliyofanyika na dhima yake kama nchi kwa mamilioni ya wahanga kutokana na uvamizi  wa kimabavu dhidi ya Poland na kilichotokana na hatuwa hiyo.

”Sisi wajerumani tulisababisha mateso yaliyovuka mipaka kwa raia wa Poland ambayo ni jirani yetu wakati wa vita vya pili vya dunia. Ujerumani inatambua uzito wa kosa hilo na jukumu lake kwa mamilioni ya wahanga wa uvamizi wa Ujerumani na yaliyotokana na hilo. Ujerumani kwa hivyo inaridhia kuchukua hatua ya kuwasaidia walionusurika na mashambulizi ya Ujerumani pamoja na uvamizi tulioufanya katika miaka ya 1939 hadi 1945”

Ujerumani kuilipa Poland fidia

Kansela Scholz aliongeza kusema kwamba hali inawatia wasiwasi mkubwa zaidi ni ile ya waathirika ambao sasa ni wakongwe,na kuahidi kuchukuwa hatua kuhusiana na kundi hilo.

Hata hivyo hakuweka wazi ni lini au ni kiasi gani cha fidia kitakachotolewa kwa waathirika ambao bado wako hai, takriban 40,000 , wa madhila ya Wanazi walioikalia kwa mabavu Poland.

Japo waziri mkuu wa Poland Donald Tusk amesema fidia hiyo itaanza kutolewa hivi karibuni huku pia akiwahakikishia wandishi wa habari kwamba hatua hiyo iliyochukuliwa na Ujerumani inaweza kuimarisha mahusiano kati ya mataifa hayo mawili kwasababu nia njema pia  ni suala muhimu katika mazingira ya kisiasa.

Waziri mkuu wa Poland alipomkaribisha Olaf Scholz.
Kansela Olaf Scholz akikaribishwa kijeshi Poland.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Katika utawala uliopita nchini Poland ulioongozwa na chama cha kizalendo cha PiS kilikuwa kikiishinikiza Ujerumani ilipe fidia ya yuro trilioni 1.3 kutoka na madhila yaliyofanywa na utawala wa Wanazi wa Ujerumani.

Waziri mkuu wa Poland hivi sasa Donald Tusk ameonesha kuchukuwa mwelekeo mwingine katika mahusiano yake na Ujerumani, ukiwepo mjongeleano wa urafiki.Tusk amesisitiza kwamba kwake yeye ni muhimu Ujerumani kuchukuwa dhima kubwa zaidi katika kulinda usalama wa bara la Ulaya.

”Pia tunatambua kikamilifu hivi sasa, na hili tumelijadili leo hii kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja au miwili ulimwengu huu tunaouona sasa huenda ukabadilika kabisa na kuwa tofauti. Tunapaswa kujitegemea wenyewe, Ulaya inapaswa kujitegemea. Uthabiti wa Nato utategemea ikiwa Ulaya itaweza kujilinda yenyewe.”

Viongozi wa Ujerumani na Poland
Kansela Olaf Scholz na waziri mkuu wa Poland Donald TuskPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kwenye mazungumzo yao viongozi hao wawili walikuwa na dhima ya kuimarisha zaidi mahusiano ya pande hizo mbili katika wakati ambapo barani Ulaya wimbi la kuimarika kwa uungaji mkono wa vyama vya siasa kali vyenye mitizamo ya kutoupendelea Umoja wa Ulaya, linaongezeka.

Kwenye ziara hiyo Kansela Scholz ameandamana na mawaziri wake 12 akiwemo waziri wa ulinzi Boris Pistrorius.

 

Related Posts