Mtandao wa X ulivyomtoa Matarra gerezani

Dar es Salaam. “Nilipokuwa si kuzuri hata kidogo, nawashukuru wanamtandao wa X.”

Haya ni maneno ya Japhet Matarra, kijana aliyechiwa huru baada ya kufungwa gerezani kwa makosa ya mtandao.

Kijana huyo aliyetiwa hatiani kwa kuhoji utajiri wa marais wa Tanzania kupitia mitandao ya kijamii, ameachiwa baada ya marafiki na wanaharakati kuchangisha fedha kupitia mtandao wa X (zamani Twitter) na kumlipia faini.

Matarra, mkazi wa Kilimanjaro alihukumiwa mwaka 2023 kifungo cha miaka mitano jela au faini ya Sh7 milioni.

Baada ya familia yake kushindwa kumudu faini hiyo, alipelekwa gereza la Karanga, lilipo Mkoa wa Kilimanjaro kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka mitano.

Hadi anaachiwa huru leo Jumanne, Julai 2, 2024, tayari kijana huyo ameshaitumikia adhabu yake kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kupitia mtandao wa X, marafiki wa kijana huyo walichanga Sh10 milioni kwa saa 24, ikiwa ni fedha za faini pamoja na kiwango kingine cha kumsaidia Matarra kuanza maisha.

Matarra baada ya kuachiwa huru, amezungumza na Mwananchi Digital, kwanza amewashukuru marafiki zake wa mtandao wa X kwa kumkumbuka katika nyakati ngumu alizopitia, akiwaomba upendo waliouonyesha kwake uendelee kwa wengine.

“Namashukuru Mungu na marafiki zangu kwa kunikumbuka, si jambo jepesi hili, walichokifanya moyo huu uendelee kwa wengine, nilipokuwa si kuzuri hata kidogo,” amesema Matarra.

Devota Tweve, mmoja wa marafiki wa Matarra kupitia mtandao wa X ambaye pia aliliibua suala la kijana huyo kutoonekana muda mrefu mtandaoni na baada ya kuhoji mara kwa mara, alishirikiana na marafiki zake wengine kumtafuta mtu wa karibu wa kijana  huyo.

Devota ametaja marafiki zake wengine walioibua changamoto ya Matarra ni Miriam Mkanaka, Tito Magoti, Charles Mwita na wote walishikiriana kuhamasisha michango kwa njia ya mtandao wa X kila uchwao hadi leo Jumanne Julai 2, 2024 walipofanikiwa kumtoa gerezani.

“Tunamshukuru Pius Mrema ambaye naye alimfuatilia ndugu yetu na wakili alishughulikia taratibu za faini tukalipa na sasa yupo huru, niwashukuru sana  watumiaji wa mtandao wa X kwa upendo waliounyesha, upendo huu hautaishia kwa Matarra na Edger Mwakalebela (Sativa) tutaendelea kusaidia na wengine,” amesema.

Kwa upande wake, Twaha Mwaipaya ambaye naye alishiriki kuhamasisha michango ya kumtoa kijana huyo gerezani, amesema kiwango cha faini waliyolipa watakiweka wazi baadaye, kwani faini ilipungua kutokana na adhabu ambayo Matarra aliitumikia.

“Niwapongeze wenzangu Miriam Mkanaka, Tito Magoti na Devota Tweve na familia yote ya mtandao wa X kwa kazi kubwa waliyoifanya na kuonyesha upendo mkubwa, sasa ndugu yetu yupo huru. Serikali sasa ione faida ya mtandao huu kwa sababu kuna watu walianza kujitokeza wakitaka ufungwe,” amesema.

Kwa upande wake, baba mzazi wa Japhet, Ibrahim Matarra amesema furaha yake haina kipimo kwa kumuona mtoto wake kwa mara nyingine akiwa bado yupo hai.

Amesema baada ya kusikia kifungo cha miaka mitano gerezani aliondoa imani ya kumuona mtoto wake huyo wa kwanza.

“Nawashukuru watumiaji wa mtandao wa X kwa kuwasaidia wanyonge, wasichoke kutupambania leo wametimiza ndoto yangu ya kumuona mtoto wangu nasema ahsante,” amesema.

Related Posts