Tanzania, Msumbiji kuanzisha kituo kimoja cha forodha

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema yeye pamoja na Rais wa Msumbiji, Philip Nyusi wamekubaliana kuanzisha sasa kituo kimoja cha forodha Mtambaswala kitakachohamasisha biashara. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumanne wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara ya Rais wa Msumbiji, Philip Nyusi Ikulu jijini Dar es Salaam.

Amesema mwaka juzi 2022 biashara ya Tanzania na Mozambique ilikuwa Dola milioni 57.8 lakini mwaka jana tumeshuka.

“Kwa hiyo tumekubaliana kuangalia sababu gani, labda usalama ulizorota, baadhi ya mipaka vile vichochoro wanavyopita wafanyabiashara tulifunga. Inawezekana pia baadhi ya transaction hazipatikani official. Kama mnavyojua mpaka wetu ni mrefu. Kwa hiyo wafanyabishara wanapenya penya na zile takwimu zinatupita,” amesema.

Aidha, amesema kwa kuwa nchi zinazozalisha korosho kwa wingi Afrika zimekuwa zikitofautiana bei ya zao hilo katika soko la dunia, sasa wakuu wa nchi hizo wamekubaliana kuwa na umoja wao.

“Tunakwenda njia tofauti ambazo ni za kuwafanya watu wanaonunua korosho ndani angalau basi inone kidogo. Kwa hiyo tumekubaliana kuunda umoja, na mnakumbuka alipokuja Rais wa Guinea Bissau, Mheshimiwa Embalo nilimuuzia wazo hili naye amekubaliana. Kwa hiyo kwa pamoja sasa wazalishaji wa korosho Afrika utakwenda kufanya umoja wetu ili tuwe na sauti moja katika masoko,” amesema Rais.

Rais Nyusi ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku tatu, anatarajiwa pia kuungana na Rais Samia kufungua rasmi maonesho ya kimataifa ya biashara maarufu kama sabasaba kesho Jumatano jijini Dar es Salaam.

Related Posts