Dar es Salaam. Uhaba wa wataalamu, kodi kubwa na changamoto za kisera ni miongoni mwa vikwazo vilivyotajwa kusababisha idadi ndogo ya vyombo vya moto vinavyotumia nishati ya umeme katika uendeshaji wake nchini.
Kwa mujibu wa Ripoti ya E Mobility Alliance iliyotolewa Machi 2023, Tanzania ina vyombo vya moto vinavyotumia umeme 5,000 idadi ambayo ni ndogo kutokana na uelekeo wa dunia katika matumizi ya nishati safi, lakini ni kubwa kwa nchi za Afrika Mashariki.
Pengine idadi ya vyombo hivyo ingekuwa zaidi ya hiyo, lakini ripoti hiyo inaeleza uwepo wa changamoto za kodi kubwa katika bidhaa hizo, uelewa mdogo wa jamii, mafundi wachache, umbali wa huduma za umeme na kutokuwepo kwa sera za wazi unasababisha uchache wake.
Hata hivyo, Serikali imesema ipo katika hatua za kuhakikisha vyombo hivyo vinasajiliwa, ili kutumika barabarani.
Mwananchi limeshuhudia idadi kadhaa ya vyombo vya moto vinavyotumia nishati ya umeme katika Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba.
Akizungumzia hilo, Mhadhiri Msaidizi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Gerutu Bosinge amesema changamoto ya ombwe la wataalamu inaweza kutatuliwa kwa kuanzishwa kozi fupi, wakati mchakato wa kukamilisha maandalizi ya kozi ndefu yakiendelea.
Kwa mujibu wa mhadhiri huyo, tayari DIT imepokea vijana 600 wenye nia ya kujifunza kuhusu teknolojia hizo na baadhi yao wamesoma kozi za muda mfupi kuanzia mwezi mmoja hadi sita.
Ili kuendeleza mafunzo, amesema walianza kwa kubuni bajaji ya kutumia umeme kwa ajili ya kufanyia mafunzo kwa vitendo kwa vijana wanaosomea tasnia hiyo na uuzaji pia.
“Kilio cha watumiaji wa vyombo vya usafirishaji vinavyotumia umeme kusikika kwa Watanzania kujikita kwenye utengenezaji wa vyombo hivyo, kwani wamekuwa wakiharibiwa kwa kukosekana kwa wataalamu,” amesema.
Hata hivyo, amesema wanalazimika kubadili muelekeo wa sayansi na teknolojia, ili kuendana na matakwa ya dunia katika mapambano ya uchafuzi wa mazingira na kampeni ya matumizi ya nishati safi.
“Ili kufuata uelekeo wa dunia ya sasa katika nishati safi, kuna umuhimu mkubwa wa taasisi zinazoshughulika na masuala ya sayansi na teknolojia kuelekea huko, hususani katika ubunifu wa matumizi ya nishati mbadala kama ilivyokuwa kwenye gesi na sasa tunapaswa kuhamia kwenye umeme,” amesema Bosinge.
Muuzaji wa vyombo vya usafirishaji vinavyotumia umeme, Hamza Kessy amesema idadi ya vijana wanaonunua vyombo hivyo inaongezeka hasa pikipiki kwa sababu ya matumizi nafuu.
“Kampuni zimetumia fursa za kuleta hizi bidhaa kwa sababu ni nafuu na inamsaidia mtumiaji kuwa huru kwa sababu matumizi yake ni kama inavyochajiwa simu ya mkononi kwa upande wa pikipiki,” amesema Hamza.
Kwa kadri bei ya mafuta inavyopanda bila kueleweka, amesema na ndivyo ubunifu wa teknolojia ya vyombo vya moto vinavyotumia umeme unavyoongezeka.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhi (Latra), Habibu Suluo amesema wapo kwenye ubadishaji wa sheria, ili kurasimisha matumizi ya vyombo vinavyotumia umeme visivyohitaji leseni.
Katika kufanikisha hilo, amesema wanasubiri mabadiliko ya sheria itakayoruhusu usajili wa vyombo hivyo kwa kuwapatia namba za matumizi ya barabarani.
“Baada ya kukaa vikao tumekubaliana kupitishwa kwa muswada wa sheria ya fedha ya mwaka 2024/25, ili kusajili kwani bila TRA sisi hatuwezi kufanya utambuzi wa anuani wa chombo husika,” amesema Suluo.
Pia, amesema malengo ya Latra ni kuona matumizi ya nishati mbadala yanakuwa kwa kasi kwa ajili ya kutunza mazingira na kushawishi nishati mbadala kama ilivyo kwenye gesi.
Waziri wa Biashara na Viwanda, Ashatu Kijaji amesema lengo kwa sasa ni kuhakikisha watu wanatumia nishati safi, hivyo uwepo wa vyombo hivyo ni muendelezo wa kampeni hiyo.