Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive, jijini Dar es Salaam imezidi kuikaba kooni Serikali kuhusiana na uthibitisho wa ugonjwa wa shahidi wake aliyeshindwa kutoa ushahidi katika kesi ya ukahaba wiki iliyopita kwa maelezo anaumwa.
Ni baada ya kuionya Serikali na kuitaka iheshimu amri na mamlaka ya mahakama.
Mbali na onyo hilo, ingawa shahidi huyo amefika mahakamani na kutoa ushahidi wake leo Jumanne Julai 2, 2024, mahakama imesisitiza bado inahitaji uthibitisho huo, huku ikielekeza uwasilishe mahakamani kesho Jumatano asubuhi, kabla ya kesi hiyo kuanza.
Washtakiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mfawidhi Rachael Kasebele ni Mariam Yusufu Mkinde (25) mkazi wa Magomeni, Mwazani Nassoro (25) mkazi wa Kigogo, Mwanaidi Salum (25) mkazi wa Mabibo, Faudhia Hassan (35) mkazi wa Ubungo na Tatu Omary (40) mkazi wa Ubungo.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 17277/2024, washtakiwa wanakabiliwa na shtaka moja la kufanya vitendo vya aibu mbele ya hadhara kwa ajili ya kufanya umalaya, kinyume na kifungu cha 176 (a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 Marejeo ya mwaka 2022.
Alhamisi ya wiki iliyopita, upande wa mashtaka uliieleza kuwa shahidi wake mmoja kati ya wawili waliokuwa wameandaliwa siku hiyo kutoa ushahidi aliugua, hivyo kuomba ahirisho, ili aende hospitali kupata matibabu.
Mahakama iliridhia ombi hilo, ikaahirisha kesi hiyo mpaka kesho yake, Ijumaa. Siku hiyo shahidi huyo alifika mahakamani, lakini upande wa mashtaka ukaieleza bado hali yake si nzuri na kwamba anahitaji kwenda hospitali.
Waendesha mashtaka katika kesi hiyo wa siku hiyo, mawakili wa Serikali, Winfrida Ouko na Tumaini Mafuru waliieleza mahakama wamemuite ili mahakama imuone, kisha aende hospitali na alipoitwa mbele ya mahakama alitembea huku akiwa ameshikiliwa.
Hata hivyo, mawakili wa upande wa utetezi, Peter Madeleka, Jebra Kambole na Maria Mushi walipinga maelezo hayo wakidai hawana imani shahidi huyo alikuwa anaumwa na kwamba mahakama haiwezi kupima ugonjwa kwa kumuangalia kwa macho.
Badala yake walidai shahidi huyo alipaswa kuwasilisha mahakamani vyeti vya matibabu, kuithibitishia mahakama.
Mawakili wa Serikali walidai jana yake hakuweza kwenda hospitali kwa sababu alikuwa na dawa nyumbani ambazo alizitumia na kwamba siku hiyo Ijumaa ndio alikuwa anakwenda hospitalini.
Baada ya mabishano ya pande hizo mbili, mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Hakimu Mfawidhi Lugano Kasebele imekubaliana na hoja za mawakili wa utetezi kuwa mahakama haiwezi kujua ugonjwa wa shahidi kwa kumuangalia.
Hata hiyo, Hakimu Kasebele aliridhia kuahirisha kesi hiyo, ili shahidi huyo aende hospitalini, lakini akaelekeza upande wa mashtaka uwasilishe mahakamani vyeti vya uthibitisho wa matibabu ya shahidi huyo na wa mashahidi wengine ambao upande wa mashtaka ulieleza walikuwa kwenye kazi maalumu.
Leo Jumanne, Julai 2, 2024 kesi hiyo ilipoitwa upande wa mashtaka uliowakilishwa na mawakili wa Serikali, Ouko na Cuthbert Mbilinyi umeieleza mahakama kuwa una mashahidi wawili, akiwemo shahidi huyo aliyekuwa anaumwa WP Konstebo Masadi Kassim Madenge.
Hata hivyo, hawakuwa na uthibitisho wa ugonjwa wa shahidi huyo kama mahakama ilivyoelekeza, jambo lililoibua mvutano mkali mpaka waendesha mashtaka wakaomba kama vyeti hivyo ni muhimu, kesi iahirishwe ili waende kuvitafuta.
Upande wa utetezi ulipinga hoja ya ahirisho, badala yake ukaomba kesi iendelee, lakini ukaiomba mahakama ichukue hatua kwa upande wa mashtaka kwa kupuuza amri hiyo na Hakimu Kasebele akasema atatoa uamuzi baada ya kumaliza kusikiliza ushahidi.
Hivyo, shahidi huyo alipanda kizimbani akiwa ni shahidi wa pili na wa mwisho kwa leo na kufanya jumla ya mashahidi wanne waliotoa ushahidi katika kesi hiyo kati ya 10 wanaotarajiwa.
Baada ya kuhitimisha ushahidi wake, ndipo Hakimu Kasebele akatoa uamuzi kuhusu upande wa mashtaka kupuuza amri yake.
Hakimu Kasebele amesema hakuna ubishi upande wa mashtaka hawakuwasilisha uthibitisho huo na kwamba hata shahidi mwenyewe mpaka amekamilisha ushahidi wake, hakuwasilisha vyeti vya matibabu.
Hivyo, amesema kitendo hicho kilichofanywa na upande wa mashtaka si sahihi na kwamba hata yeye hakijamfurahisha kwa kuwa vinaonyesha kupuuza amri ya mahakama.
Amesema mahakama lazima iheshimiwe kwa mujibu wa Katiba na mtu yeyote bila kujali umri wake wala hadhi yake.
“Hivyo, kwa leo mahakama inawaonya jambo hili lisirudie, lakini bado ninaomba taarifa ya Masadi (shahidi aliyedaiwa mgonjwa) kesho ije kwamba alikwenda hospitalini na amri za mahakama ziheshimiwe,” amesema Hakimua Kasebele na kusisitiza:
“Kama tutaendelea kufanyiana vitendo ambavyo havistahili tutachukua hatua zaidi. Mahakama inasisitiza heshima iwepo na taratibu zifuatwe. Nasisitiza kesho taarifa ya Masadi iwepo kabla ya kuanza mahakama.”
Pia, hakimu amesisitiza taarifa ya mashahidi wengine ambao ni maaskari polisi ambao upande wa mashtaka uliieleza hawakuweza kupatikana kwa kuwa wana kazi maalumu, nao uthibitisho wa majukumu hayo uwasilishwe, kabla au siku watakazofika mahakamani kutoa ushahidi.