Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza ufanisi katika makusanyo ya mapato yaliyofikia asilimia 97.67 katika mwaka wa fedha 2023/24, yakiwa yameongezeka kwa asilimia 14.5 ikilinganishwa na ya mwaka 2022/2023
Kufuatia ongezeko hilo, wataalamu wa uchumi wamesema ni vyema sasa nchi ikaanza kufadhili miradi yenyewe na kupunguza utegemezi wa mikopo kutoka nje.
TRA imesema ongezeko hilo limetokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi, mwitikio mzuri wa walipakodi katika uwasilishaji ritani, kuongezeka kwa uhiari wa kulipa kodi, na kuongezekwa kwa uingizwaji wa mizigo kutoka nje kama sababu za ufanisi huo.
Kwa mujibu wa TRA, kwa mwaka 2023/24 makusanyo yalifikia Sh27.64 trilioni kutoka Sh24.14 trilioni za mwaka uliotanguli wa 2022/2023.
Tangazo hilo limetolewa kipindi ambacho umemalizika mgomo wa pili wa wafanyabiashara wanaopinga utitiri wa kodi, ukubwa wa faini na mambo mbalimbali katika mfumo wa kodi.
Mtaalamu wa Uchumi, Dk Abel Kinyondo amesema kuongezeka kwa makusanyo ya mapato, zaidi ya mfumuko wa bei uliopo, kunapaswa kuwa chachu ya kupunguza mikopo kutoka nje kwa sababu nchi inakusanya zaidi kupitia ndani.
Hiyo ikiwa na maana kuwa, pengo ambalo lilikuwa linazibwa na mikopo linashuka kutokana na kuimarika ukusanyaji mapato.
“Tunaongeza mapato kupitia kodi na mikopo inaendelea kuwapo, basi kuna kitu sehemu hakiko sawa. Taasisi za Serikali zione hiki kama kitu cha kuwaamsha, na ili tuendelee ni vyema sekta na taasisi zisomane,” amesema Profesa Kinyondo.
Amesema taasisi za umma zinapaswa kuamka na kuangalia kwa nini nchi inaendelea kuongeza madeni wakati ukusanyaji wa mapato unaongezeka, nchi ina uwezo wa kufadhili miradi ya kiuchumi.
Amesema ikiwa malengo ya TRA yalikuwa halisi, basi inafanya vizuri kwa sababu wanaoweka malengo na kutaka kuyafikia ni wao.
Hata hivyo, aliitaka TRA kujitafakari juu ya yale yanayolalamikiwa na watu tofauti, ikiwemo wafanyabiashara ambao hivi karibuni waligoma ikiwa ni moja ya hatua ya kupinga njia zinazotumiwa na mamlaka hiyo katika makusanyo ya kodi na usimamiaji ulipaji kodi.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi kupitia fedha za ndani, Profesa Kinyondo amesema: “Kukusanya fedha ni jambo moja na kuhakikisha zinakwenda kufanya mambo yaliyokusudiwa liko nje yao. Kama matumizi hayaakisi uhalisia na utawala bora kuongeza mapato kupitia kodi hakuna maana sana.”
Mtaalamu mwingine wa Uchumi, Oscar Mkude amesema kukua kwa ukusanyaji wa mapato ni namna mojawapo ya nchi kujitegemea lakini ili kufikia uwezo huo lazima matumizi yapungue ili kupata akiba inayoweza kusaidia katika mambo mengine.
“Matumizi katika maeneo mengine kama vifaakazi, majengo, mikutano vina gharama kubwa sana, hivi karibuni kulikuwa na mjadala wa magari yanayonunuliwa na Serikali hata baadhi ya taasisi binafsi haziwezi kununua,” amesema Mkude.
Amesema ni vyema kuangalia namna ya kudhibiti matumizi ya fedha za umma kuiwezesha nchi kufadhili miradi yake yenyewe.
Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Tobias Swai amesema kukua kwa mapato hayo huenda kukawa kunaakisi sera za kikodi na kuwa uwezo wa kukisia mapato ya ndani umekuwa mkubwa lakini gharama ya kukusanya kodi hizo zilikuwaje?
“Gharama zilizotumika, je, wameongeza nguvu zaidi, kuwekeza katika software (mifumo ya kompyuta) ili kufikia ufanisi huu, wangetwambia,” amesema Swai.
Taarifa ya TRA kwa vyombo vya habari iliyotolewa Julai mosi inaeleza, makusanyo ya robo ya nne ya mwaka (Aprili hadi Juni, 2024) yalikuwa Sh7.09 trilioni sawa na ufanisi wa asilimia 99.46 ya lengo la kukusanya Sh7.09 trilioni.
Makusanyo haya ni ongezeko la asilimia 24 ukilinganisha na Sh5.72 trilioni zilizokusanywa katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha uliopita 2022/23.
“Ongezeko hili limechochewa na ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini, hususani uzalishaji viwandani na kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea nchini kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo,” imesema taarifa hiyo.
“Kusogeza huduma jirani na walipakodi kwa kuanzisha divisheni za walipakodi wadogo na walipakodi wa kati, pamoja na kuendelea kusuluhisha pingamizi za kodi nje ya mahakama ni sababu nyingine,” imesema TRA.
Mamlaka pia imesema kuongezeka uingizwaji wa mizigo kutoka nje ya nchi kutokana na uboreshwaji wa mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini umechangia katika ongezeko hilo.
“Pamoja na mafanikio haya, vitendo vya ukwepaji kodi na kutozingatia sheria vimeendelea kushamiri miongoni mwa makundi mbalimbali ya walipakodi, wakiwemo watu binafsi, makampuni ya ndani na yale ya kimataifa. TRA itaendelea kuhimiza ulipaji kodi kwa kufuata sheria zilizopo na utekelezaji wake kuzingatia misingi ya utawala bora,” imesema.
Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) nayo kwa mwaka wa fedha 2023/24 imetangaza kukusanya Sh718.7 bilioni kati ya lengo la kukusanya Sh675.6 bilioni sawa na ufanisi wa asilimia 106.
Kwa makusanyo hayo, mambo manane yametajwa kuchangia ufanisi huo, ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa mifumo, ulipajikodi kwa hiari, weledi wa watendaji wa mamlaka na mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa ZRA, Yusuph Juma Mwenda, Julai 2, 2024 imesema makusanyo hayo yameongezeka kwa asilimia 27.01 sawa na Sh152.8 bilioni, ikilinganishwa na mapato halisi ya mwaka uliopita 2022/23 ambayo yalikuwa Sh565.8 bilioni.
Kamishna Mwenda amesema kuimarika kwa uhusiano na ushirikiano kati ya ZRA na wafanyabiashara kumechangia ongezeko hilo.