Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kutoa elimu ya Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira kwa wananchi ambapo elimu hiyo imehusisha umuhimu wa ulipaji wa Ada za Mazingira, usimamizi wa taka hatarishi na athari zake, matumizi salama ya Kemikali ya Zebaki kwa Wachimbaji Wadogo wa dhahabu pamoja na umuhimu wa kutenganisha taka kutoka kwenye chanzo.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Julai 2,2024 katıka Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika katika viwanja vya Julius Nyerere Barabara ya Kilwa Temeke, jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu NEMC, Mary Mushi amesema katika banda lao wanatoa namba ya kumbukumbu kwa ajili ya kusaidia kufanya malipo ya ada ya mazingira kwa mwaka mzima ambazo zinasaidia kuwafikia wadau mbalimbali kwaajili ya kuwapa elimu ya uhifadhi wa mazingira.
Amesema kuna umuhimu mkubwa kwa wadau kufika katika banda lao kwani wanaweza kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo kupatanamba ya kumbukumbu kwa ajili ya kusaidia kufanya malipo ya ada za mazingira kwa wale ambao bado hawajalipia.
Aidha kwa upande wake Mhandisi kutoka NEMC, Geatitud Albert amesema taka hatarishi zisiposimamiwa vyema zikachanganywa na taka zisizo hatarishi zitapelekea athari katika mazingira.
“Mfano wa taka hatarishi aina ya chuma chakavu tunazisimamiaje ,unapokua umezalisha chuma chakavu cha kwanza unatakiwa kuzihifadhi katika eneo ambalo limesakafiwa kwa sababu zikinueshewa na mvua zinaweza kuleta athari katika udongo na vyanzo vya maji”. Amesema
Ameeleza kuwa anayehitaji kutunza taka chakavu anapaswa kuwa na kibali cha NEMC ambapo watampatia utaratibu wa uhifadhi wa mazingira kwa kuzihifadhi taka hizo kwa utaratibu.
Naye, Afisa Mwandamizi Elimu ya Jamii, Suzan Chawe amesema kanuni ya mwaka 2021 ya mazingira imeanisha mchakato wa kufanya tathimini ya athari ya mazingira kwa kutumia washauri elekezi ambapo wananchi wote wanaalikwa kujifunza namna ya kufanya tathimini ya mazingira.
Chawe ametoa rai kwa wasomi watakaopenda kuwa washauri elekezi wa mazingira kwa ajili ya kufanya tafiti na kuandaa ripoti za tathimini ya mazingira kuomba cheti ambacho kitawapa kibali kufanya tafiti kwa kutumia tovuti yao ya eia.nemc.or.tz
NEMC inaendelea kuwakaribisha wananchi katika banda lao lililopo viwanja vya sabasaba jengo la Karume ili kupata elimu ya Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira kwa maendeleo endelevu ya Taifa.