Alichosema Lissu kuhusu Mchungaji Msigwa kutimkia CCM

Dar es Salaam. Siku chache tangu Mchungaji Peter Msigwa kutimkia Chama cha Mapinduzi (CCM), Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu ameeleza kusikitishwa na uamuzi huo akisema: “Kwa kujiunga na maadui zangu wa kisiasa, sasa nitalazimika kukutana naye kama hasimu wake wa kisiasa.”

Lissu amesema hayo leo Jumanne Julai 2, 2024 ikiwa ni siku nne zimepita tangu Mchungaji Msigwa, aliyewahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini na Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Nyasa kutimkia CCM.

Msigwa alitambulishwa kuwa mwanachama mpya wa CCM Juni 30, 2024 mbele ya wajumbe wa halmashauri kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho, katika kikao kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam na kuongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.

Kabla ya kuhamia CCM, Msigwa alikuwa akisubiri kusikilizwa kwa rufaa yake aliyoikata kupinga uchaguzi wa uenyekiti Kanda ya Nyasa kupinga ushindi wa Joseph Mbilinyi maarufu Sugu aliyemshinda kwenye nafasi ya uenyekiti.

Mbali na kukata rufaa, Msigwa amekuwa akimlalamikia Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kupitia mikutano ya waandishi wa habari na mitandaoni, kuwa ndiye chanzo cha kushindwa uchaguzi huo.

Mchungaji Msigwa aliyekuwa akitetea nafasi hiyo alishindwa na Sugu kwa kura 54 dhidi ya 52 za Msigwa. Uchaguzi ulifanyika Mei 29, 2024 na kushuhudia mvutano mkali.

Baada ya Msigwa kutimkia CCM, ikiwa ni siku chache zimepita tangu aliposhiriki ziara ya Lissu mkoani Singida, Mwananchi Digital imemtafuta Lissu ili kupata mtazamo wake juu ya uamuzi wa mwanasiasa huyo ambaye amekuwa akieleza ni rafiki yake.

Katika maelezo yake, Lissu amesema: “Mchungaji Peter Msigwa amekuwa rafiki yangu wa karibu kwa takriban miaka 20 ambayo tumefahamiana. Tumefanya kazi pamoja bungeni na nje ya Bunge kwenye chama.

“Tumekuwa naye kwenye Kamati Kuu ya chama kwa miaka mingi. Tumekuwa na misimamo ya pamoja kwenye masuala mengi ya kisiasa ya chama chetu na ya nchi yetu. Tumetofautiana kwenye masuala kadhaa ya chama na ya nchi vile vile,” amesema Lissu.

“Hili la kuhamia CCM limekuja kwangu ghafla kama ninavyoamini limekuja kwako ghafla pia. Nilimkaribisha kushiriki nami kwenye ziara yangu ya Mkoa wa Singida mwezi uliopita, na alikuja mara mbili na kila siku aliyokuwa kwenye ziara nilimpa fursa ya kuzungumza na wananchi wetu.”

Akigusia suala la yeye kupata taarifa awali, Lissu amesema: “Hata hivyo, mara zote alizokuwa na mimi hakunishirikisha au kunifanya nifikiri alikuwa na mpango wa kuhamia CCM.”

“Ni wazi alikuwa na mengi moyoni mwake ambayo hakutaka yajulikane. Sasa yamejulikana. Kwa kujiunga na maadui zangu wa kisiasa, sasa nitalazimika kukutana naye kama hasimu wake wa kisiasa. Sikuwahi kufikiria itakuwa hivyo. Hicho ndicho kinachoniumiza moyo,” amesema.

Lissu amewahi kusema Mchungaji Msigwa ni rafiki yake na alikuwa miongoni mwa watu waliochangia chupa ya damu kunusuru uhai wake, aliposhambuliwa kwa risasi Septemba 7, 20217.

Tukio hilo lilitokea alasiri, Area D jijini Dodoma, wakati Lissu akitoka kushiriki mkutano wa Bunge uliokuwa ukiendelea.

Wakati Lissu akieleza hayo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye anaendelea na ziara mikoa ya kaskazini na sasa yupo Mkoa wa Tanga, ametumia kurasa zake za kijamii kuzungumzia siasa za upinzani na CCM.

“Kuwa chama cha upinzani hasa Chadema sio suala jepesi, linahitaji ujasiri wa namna ya pekee. Viongozi wengi wa upinzani na Watanzania wazalendo wa nchi hii wanapitia nyakati ngumu kutokana na uoga wa Serikali ya CCM.

“Marehemu Mzee Lowassa alithubutu kuingia Chadema, japo baada ya muda alirudi CCM.Tunatambua ujasiri wa maamuzi yake.  Kitu pekee kitakachiokoa Tanzania kutoka kwenye mikono ya watawala ni ujasiri na uthubutu wa mwananchi mmoja mmoja; tuanze sasa kulipigania taifa letu,” ameandika Mbowe.

Related Posts