DC MANGWALA "MTUMISHI ATAKAYEKULA FEDHA ZA MAENDELEO ATAZITAPIKA"

NA WILLIUM PAUL, ROMBO.

WATUMISHI wa Umma wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuhakikisha fedha zinazoletwa na serikali kwa ajili ya miradi ya maendeleo zitumike kama zilivyokusudiwa na yeyote atakayebaini kuzitumia kinyume atazitapika.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa wilaya ya Rombo, Raymond Mwangwala katika mkutano wa hadhara uliofanyika Tarafa ya Mengwe kata ya Mamsera ambapo alisema kuwa, lengo la serikali ni kupeleka maendeleo kwa wananchi.

Alisema kuwa, serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo mpaka sasa Bilioni 33 zimeshaletwa na bado fedha hizo zimeendelea kuletwa na kuwataka wanatumishi kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Niwaombe watumishi wenzangu kuweni makini na fedha za serikali zinazoletwa nataka kuona malengo ya serikali yakitimia hivyo sitamvumilia mtumishi yeyote atakayebainika amekula fedha za Umma niwahakikishie atazitapika hizo fedha” Alisema Mangwala.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa, serikali inatambua vipo baadhi ya vitongoji katika wilaya hiyo havina huduma ya umeme lakini kupitia wakala wa umeme vijijini REA vitongoji vyote katika wilaya hiyo vitafika na huduma hiyo na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu.

Aidha Mangwala amewataka wananchi kuhakikisha wanalinda na kuitunza miradi inayojengwa ili iweze kudumu muda mrefu na kuweza kutimiza lengo la serikali.

Wakitoa kero kwa mkuu huyo wa wilaya wananchi walidai kuwa vipo vitongoji vitatu vilivyopo katika kata ya Mamsera ambavyo havina huduma ya umeme na kuiomba serikali kuweza kuwapatia huduma hiyo.


Related Posts