Naibu wa Waziri wa Kilimo David jana amefungua rasmi maadhimisho ya wiki ya ushirika duniani, ambayo kwa kawaida yanaambatana na maonesho ya shughuli za ushirika, ambapo wadau mbalimbali, ikiwemo kampuni ya tumbaku ya Alliance One wakionesha shughuli zao kwa muhimu.
Kabla ya ufunguzi wa maonesho hayo yanayofanyika kwenye viwanja vya Nanenane Mkoani hapa, Mheshimiwa Silinde alifanya ziara ya kutembelea mabanda ya wadau hao ikiwemo Alliance One, ambalo banda lao linaonesha shughuli mbalimbali za kitumbaku.
Lakini pia, banda hilo linaonesha namna ushirika wa wafanyakazi wa kampuni hiyo unavyoshamiri, kwa maana ya Saccos yao iitwayo Dimon Morogoro Workers Saccos.
Akiwa bandani hapo Naibu Waziri alipewa maelezo na Mkurugenzi wa Uzalishaji Bw. David Mayunga ambaye alimuonesha madaraja mbalimbali na bei zake, huku akisisitiza kuwa mwaka huu wakulima wamepeta bei ya wastani wa dola 2.4 kwa daraja zuri.
Amesema kwamba kampuni yake, tofauti na makampuni mengine, imeweza kudumu na wakulima kwenye ushirika wao kwa zaidi ya miaka 25 iliyopita pasipo kuyumba.
“Kampuni ya Alliance One inaamini kwamba kwa kila jambo linalofanywa na kampuni hiyo,lengo kuu ni kubadilisha Maisha ya watu ili hatimaye watu wote waweze kuishi Maisha bora hapa duniani,” amesema Bw.Mayunga.
Naye Msemaji wa Kampuni hiyo Wakili John Magoti, alimweleza Naibu Waziri Silinde kwamba kampuni yake inatekeleza ushirika kwa vitendo ndani na nje ya kampuni hiyo.
“Sisi tunauishi ushirika, kwani tuna siyo tu tunafanya kazi na wakulima ambao wako kwenye mfumo wa ushirika, lakini tunacho chama cha wafanyakazi ambacho kilianza na mtaji wa shilingi milioni 5, lakini sasa hivi mtaji wetu umekua mpaka zaidi ya shilingi bilioni 2” amesema.
Katika shamrashamra za maonesho hayo ya ushirika yanayoendelea hadi Julai 6, bendi ya muziki ya Mrisho Mpoto imetunga na kuimba wimbo maalum wa kampuni ya Alliance One, wimbo ambao unatikisa na kukonga nyoyo za washiriki wa maonesho hayo uwanjani hapo.
Akiongea baada ya kumaliza kutembelea mabanda hayo, kwenye hotuba yake Naibu Waziri Silinde amesema serikali imeagiza Tume ya maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na wizara za kisekta kuhamasisha uanzishaji wa vyama vya ushirika kwenye sekta zingine za kiuchumi ili kuiwezesha sekta hiyo kuwafikiwa Wananchi wengi zaidi.
Amesema bado kuna mwamko mdogo hivyo kunahitajika mkakati wa dhati wa kuhamasisha maendeleo ya Ushirika kwenye sekta nyingine za kiuchumi ili kuongeza vyama vya ushirika na Wanachama wake.
“Kupitia siku hii ya Ushirika duniani naielekeza Tume ya maendeleo ya ushirika kwa kushirikiana na wizara za kisekta na Wadau wengine kuweka mikakati na kuhamasisha uanzishaji wa vyama vya ushirika katika sekta zingine za kiuchumi ili kuziwezesha sekta hizo kuwafikia Wananchi wengi zaidi” amesema.
Amesema Serikali kupitia wizara ya Kilimo na Tume ya maendeleo ya ushirika itahakikisha ushirika unaimarika ili Watanzania wengi wanaufaike na ametoa rai kwa Tume ya maendeleo ya Ushirika kuendelea kuwatangazia Wananchi umuhimu wa ushirika na kuonyesha mafanikio ya vyama vya ushirika kwa vitendo.
Ametoa wito kwa Vijana na Wanawake wote nchini kuanzisha vyama vya ushirika vinavyojishughulisha na shughuli za mazao ya kiuchumi ambazo wanafanya mmoja mmoja na Serikali itaangalia namna bora ya kuwawekea mazingira bora na mitaji.
Awali katika taarifa yake, Mkuu wa mkoa wa Tabora Paul Chacha aliyewakilishwa na Mkuu wa wilaya ya Tabora Deusdedith Katwale amesema uzalishaji wa mazao ya biashara unaongezeka, ambapo kwa zao la Tumbaku katika msimu wa 2021/2022 mkoa ulizalisha Kilo milioni 35 tu, lakini katika msimu huu wa 2024/2025 mkoa umezalisha zaidi ya kilo milioni 114.
Amesema kwa zao la Pamba kwa msimu uliopita mkoa ulizalisha Kilo milioni 16 tu, lakini msimu huu mkoa umezalisha zaidi ya kilo milioni 35 ongezeko ambalo kwa mazao yote mawili ni kubwa ndani ya muda mfupi.
“Mafaniko hayo yanatokana na jitihada kubwa za Serikali kwa kutengeneza na kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima ikiwemo kutoa mbolea ya ruzuku ambayo imewawezesha Wakulima kuzalisha kwa tija hata kufikia kiwango hicho” amesema.
Kampuni ya ununuzi wa Tumbaku ya Alliance one ni moja ya Wadau wa kiuchumi nchini na Zaidi sana mkoani Tabora ikiwa ndiyo inayoongoza kwa ununuzi wa zao hilo kwa wingi, huku ikiwalipa wakulima wake kwa wakati pasipo kuwachelewesha.
Naibu Waziri wa Kilimo Mh.David Silinde(wa tatu kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Kampuni ya Alliance One David Mayunga(wa pili kulia)wakati alipotembelea banda la kampuni hiyo jana kwenye ufunguzi maonesho ya wiki moja ya maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yanayofanyika kwenye viwanja vya Nanenane wilayani Tabora.Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya Tabora(Deusdeth Katwale),huku Msemaji wa Kampuni ya Alliance One Wakili John Magoti(Wa nne kulia) akishuhudia
Naibu Waziri wa Kilimo Mh.David Silinde akitoa hotuba ya ufunguzi wa maonesho ya wiki moja ya maadhimisho Siku ya Ushirika Duniani yanayofanyika viwanja vya nanenane mjini Tabora
Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Kampuni ya Tumbaku ya Alliance One, David Mayunga, akimpongeza mwanamuziki Mrisho Mpoto a.k.a Mjomba kwa kutunga na kisha kuimba wimbo maalum wa kuisifu kampuni yake ambapo alimkabidhi kofia maalum.Tukio hilo lilikuwa jana kwenye sherehe za ufunguzi wa maonesho ya wiki moja ya maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani yanayofanyika viwanja vya nanenane mjini Tabora