TAYARI Joshua Mutale kiraka wa Zambia ameshatambulishwa rasmi Msimbazi. Jana mchana ilikuwa zamu ya Steven Mukwala, staa wa Uganda.
Lakini sasa unaambiwa Simba imetuma tiketi mbili za ndege katika mataifa mawili tofauti ili kuwashusha nchini wachezaji wawili matata akiwemo mrithi wa Clatous Chama aliyetangazwa kujiunga na Yanga, juzi.
Kati ya tiketi hizo moja imeenda Kinshasa, DR Congo kwa winga Elie Mpanzu ambaye Mwanaspoti liliripoti dili lake kwenye toleo la jana na nyingine imetumwa Abidjan, Ivory Coast kwa kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua (22), anayetazamiwa kuwa mrithi wa Chama pale Msimbazi.
Kama ilivyokuwa kwa Mpanzu ndivyo imekuwa kwa Ahoua aliyemaliza msimu akiichezea Stella Club, Abidjan kwani Simba imepigana vikumbo na timu mbalimbali Afrika ikiwemo Esperance ya Tunisia ili kupata saini ya kiungo huyo na Mnyama yuko katika hatua za mwisho kushinda vita hiyo.
Mmoja wa vigogo wa usajili wa Simba alisema Ahoua aliyewahi kuzichezea timu za Sassandra na Sewe Sports zote za Ivory Coast, ni kiungo mshambuliaji wa kisasa mwenye nguvu lakini pia ana uwezo wa kucheza kama winga wa kulia au kushoto.
Msimu uliopita aliibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Ivory Coast tuzo ambayo msimu uliopita ilichukuliwa na Pacome Zouzoua na msimu mmoja nyuma aliibeba Stephen Aziz Ki na wote sasa wanacheza Yanga.
Katika msimu huo, Ahoua alifunga mabao 12 na kutoa pasi za mwisho sita. Endapo dili hili litakamilika, Ahoua ataungana na Muivory Coast mwenzake, Aubin Kramo katika kikosi cha Simba kwa msimu ujao.
Mwanaspoti linajua hadi sasa Simba imezinasa saini za mastaa wazawa watatu, viungo Yusuph Kagoma kutoka Singida na Omary Omary aliyekuwa Mashujaa sambamba na beki kiraka Lameck Lawi kutoka Coastal Union.
Simba imewasajili winga Mzambia Mutale, straika Mganda Steven Mukwala, beki Mbukinabe Valentino Nouma huku viungo Mnigeria Augustine Okajepha na Mkongo Debora Fernandez Mavambo mazungumzo yakiendelea.
Mukwala ni mshambuliaji anatarajiwa kuongoza ushambuliaji ya Simba ambapo msimu uliopita akiwa na Asante Kotoko ya Ghana alipachika mabao 14 akishika nafasi ya pili katika ufungaji, huku Mutale anamudu winga ya kulia na kushoto, na wakati mwingine anacheza nyuma ya mshambuliaji yaani namba 10. Uwezo wa kumudu nafasi nyingi unaweza kuwa msaada mkubwa kwa Simba.