WIKIENDI iliyopita ulitokea msuguano mkali kati ya Anthony Joshua (AJ) na Daniel Dubois kiasi cha kutaka kuzichapa ‘kavukavu’ mbele ya wasimamizi wao, uliamsha hisia zaidi za pambano lijalo, Septemba 21, mwaka huu.
Waingereza hao watapigana katika Uwanjani wa Wembley siku hiyo kuwania mkanda wa IBF ambao upo mikononi mwa Oleksandr Usyk ambaye imemlazimu auachie ushindaniwe na Dubois dhidi ya Joshua kutokana na kusaini kwake mkataba wa kupigana na Tyson Fury.
Pambano la pili baina ya Usyk na Fury litakalofanyika Desemba limemzuia Usyk kutetea mkanda wa IBF na kukubali kuuachia ushindaniwe na Waingereza hao.
Hii inamaanisha pambano la pili litakuwa la kuwania mikanda mitatu badala ya minne kama ilivyokuwa pambano la kwanza aliloshinda Usyk, akishikilia mikanda yote ya uzito wa juu inayotolewa na IBF, WBA, WBO na WBC.
Hapo ndipo AJ anapata nafasi ya kushikilia tena mkanda mmoja wa IBF aliokuwa nao miaka miwili kabla ya kuupoteza kwa Usyk katika mapambano mawili aliyopigwa kwa pointi za majaji. Kazi inayobaki kwake sasa ni kuhakikisha anamchapa Dubois ili apate haki ya kusubiri mikanda mitatu iliyobaki mikononi mwa Usyk.
Kama AJ atafanikiwa kumpiga Dubois atasubiri mshindi wa pambano la Usyk na Fury ili kusaka tena bingwa wa mikanda minne ya dunia mwakani.