Dar/Arusha. Matumizi ya gundi kama kilevi yamekuwapo nchini miongoni mwa waraibu, na hasa watoto wanaoishi mitaani katika mazingira magumu, suala linaloziweka afya za watumiaji hatarini.
Mbali na matumizi kwa waraibu, mafundi ambao kazi zao muda mrefu zinawafanya kutumia gundi, pia wako hatarini kiafya, kwa mujibu wa wataalamu.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika majiji ya Dar es Salaam na Arusha, umebaini miongoni mwa watumiaji wa gundi kama kilevi, ni watoto waishio mtaani, wenye umri chini ya miaka 18.
Baadhi ya watoto hao baada ya kutumia gundi hiyo wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya vurugu na uporaji, na wengine huwafanya kulala fofofo.
Gundi inayotajwa hutengenezwa kwa kutumia kemikali, miongoni mwa hizo zina viambata vyenye kulevya, kwa mujibu wa Dk Patrick Mfisi, kamishna wa kinga na tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Hata hivyo, Dk Mfisi anasema gundi si miongoni mwa bidhaa zinazozuiwa, japo wamekuwa wakijitahidi kuhamasisha matumizi sahihi ili kuzuia athari na uraibu inapotumika kama mbadala wa dawa za kulevya.
“Gundi na petroli ni kama aina ya dawa za kulevya ambazo sisi mamlaka hatuzidhibiti. Ni bidhaa zinazopatikana mtaani na huwezi kuzuia watu kutumia, japo zikitumiwa huwa na athari kiafya,” anasema Dk Mfisi.
Anasema tatizo la watoto kuvuta gundi lipo kwa kiwango kikubwa.
“Tunachofanya mamlaka ni kutoa elimu kwa sababu hatuna kibali cha kuwakamata au kuwadhibiti kama tunavyofanya kwa watumiaji wa dawa nyingine za kulevya.”
Dk Mfisi anashauri jamii kujiepusha na matumizi ya vilevi hivyo, kwa sababu vina madhara katika mfumo wa ubongo.
Saa nne usiku eneo la Ubungo Mataa, jijini Dar es Salaam, kijana wa miaka 17 (jina linahifadhiwa) aliyezaliwa mtaa wa Frelimo mkoani Iringa anasema yuko eneo hilo kutokana na mifarakano ya wazazi wake waliotengana na kila mmoja kuanzisha familia nyingine.
Anasema kutokana na kukosa mahitaji muhimu, aliacha shule akiwa darasa la tano akaanza kutafuta maisha mtaani na baadaye akasafiri hadi jijini Dar es Salaam anakoosha vioo vya magari na kuomba msaada kwenye maeneo ya Ubungo Mataa, Mwenge na Sinza.
Anasema yeye huvuta sigara, lakini wenzake hutumia gundi kama kilevi.
“Huwa wanaichukua gundi wanapima kwenye kikopo, wanaweka na dawa nyingine (hajaitaja) kisha huvuta puani na wakati mwingine mdomoni kwa muda. Wakishamaliza hulala fofofo mithili ya watu waliokufa.”
“Wakishavuta gundi huwa hawahisi njaa, kuna nyakati wanakuwa wakorofi, wanatupokonya hela,” anaeleza.
Saa sita usiku eneo la Ubungo Tanesco, kulikuwa na kundi la vijana wa kati ya miaka 13-18.
Mmoja kati ya hao, mzaliwa wa Mbeya (jina linahifadhiwa) anasema anatumia gundi kama kilevi.
“Tukiamka asubuhi tunaelekea Manzese sokoni, kuna mtu hutuuzia gundi kuanzia Sh1,500 kwenye kikopo. Huwa nakifungua naanza kunusa kwa muda, nikishavuta nalala kwa muda mrefu hata sihisi njaa,” anasema.
Kijana huyo na wenzake wanaolala chini ya daraja eneo la Ubungo, anasema alitumia gundi kwa mwaka mmoja. Anaeleza kuna siku baada ya kutumia gundi aliugua akapata msaada kutoka kwa msamaria mwema, aliyempeleka hospitali ambako aliambiwa hakuwa na damu na kifua chake kilikuwa na shida.
“Hiyo ndiyo siku niliacha kuvuta gundi,” anasema.
Kijana Ramadhani Hassan, mkazi wa eneo la Stadium jijini Arusha, anasimulia alianza kuvuta sigara, baadaye bangi na mwisho kwa muda mrefu amekuwa akitumia gundi. Hata hivyo, anasema kwa sasa ameacha baada ya kuugua kifua.
“Gundi ni mbaya kuliko bangi, inaweza kusababisha ukate moto (kufariki dunia) na kifua cha muda mrefu, kama mimi mpaka sasa naumwa kifua,” anasema.
Kwa mujibu wa vijana hao, kuna njia tofauti za matumizi ya gundi, ikiwamo kunusa kwa kutumia pua na wakati mwingine kuibandika puani kwa muda mrefu, pia kuivuta mdomoni.
Hassan anasema kabla ya kuitumia unaitikisa na “ukiiweka mdomoni unavuta harufu yake.”
Anasema wapo ambao huichanganya gundi na petroli kabla ya kuitumia.
Hassan anaeleza hali anayohisi baada ya kutumia gundi ni kuwa, “mwili huisha nguvu na kudhoofu, nahisi kama nataka kufariki, kuumwa kifua, kuhisi ganzi mwilini, kujiamini kuliko kawaida na wakati mwingine kulala usingizi usio wa kawaida.”
Kwa mujibu wa vijana hao, upatikanaji wa gundi ni mgumu kwa sababu askari polisi katika baadhi ya maeneo kama vile Manzese, Dar es Salaam wamepiga marufuku uuzaji wa gundi kuanzia Sh1,000, badala yake inauzwa kuanzia lita moja ambayo ni Sh10,000.
Paulinah Jacob, mkazi wa Dar es Salaam anasema ili kuzuia uraibu kwa vijana, udhibiti uanzie ngazi ya familia ili kuhakikisha watoto wahakimbii nyumbani kwenda kuishi mtaani.
Mussa Charles, mkazi wa Mianzini mkoani Arusha anashauri waraibu na vijana wapewe elimu waachane na matumizi ya gundi na siyo kuwanyanyapaa.
Diwani na Mwenyekiti wa kamati ya huduma za jamii Jiji la Arusha, Isaya Doita anasema matumizi ya gundi ni tatizo sugu, licha ya juhudi zinazotumika kuyadhibiti.
Athari kwa watumiaji wengine
Mbali ya uraibu kwa watoto, watumiaji wengine wa gundi kama vile mafundi viatu na mikoba, pia wako hatarini kuathiriwa kiafya.
Hili linathibitishwa na mfanyabiashara na mtengenezaji wa mikoba na viatu katika Soko la Machinga Complex, Dar es Salaam, Stephan Venace anayesema harufu ya gundi inapoingia kwenye mfumo wa hewa huwasha, hivyo kuna wakati kichwa huuma.
Venance, aliyefanya kazi hiyo kwa zaidi ya miaka saba, anaeleza baadhi ya mafundi wamefariki dunia kutokana na maradhi ya kifua, chanzo kikiwa matumizi ya gundi.
“Nimeanza kazi hii mwaka 2016, ninapotumia gundi kwa kuipaka, huwa nahisi inaingia hadi kwenye mishipa puani. Nikilala usiku huwa sishtuki hadi asubuhi, yaani nalala usingizi si wa kawaida,” anasema.
“Sijui kama ni gundi hiyo au uchovu tu. Kuna baadhi ya wenzetu tumewapoteza kwa ugonjwa wa kifua kikuu na wakati mwingine inaweza kuwa ni hizohizo kemikali kama gundi na nyinginezo,” anasema.
Fundi mwingine katika eneo hilo, Goodluck Masawe anasema amekuwa akitumia gundi kwa miaka zaidi ya minane katika shughuli za ufundi na kuna wakati hujihisi vibaya anapoitumia.
Mafundi wanaeleza gundi zipo za aina tofauti kulingana na kampuni na bei yake ni Sh45,000 kwa lita tano.
Inaelezwa watoto waishio mtaani na waraibu hununua inayopimwa kuanzia Sh1,000.
Thobias Msofe anaeleza kuwa kuna wakati upatikanaji wa gundi huwa na changamoto, hivyo humlazimu kununua dumu la lita tano na kuwauzia wengine.
“Dumu hili naliuza kwa kipimo kwa wafanyabiashara wengine, kipimo huanzia Sh2,000 na kuendelea. Kati ya ninaowauzia ni vigumu kujua anainunua kwa malengo gani,” anasema.
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani, mapafu na mfumo wa upumuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mwanaada Kirima anasema matumizi ya gundi kama kilevi ni hatari kiafya kwa mwili na akili.
Anasema hiyo inatokana na kemikali nyingi zilizo ndani yake, ambazo baadhi hupatikana kwenye sigara kama vile toluene (toluini), hydrocabon na nitrate oxide.
Kutokana na kemikali hizo, matumizi ya gundi yanaleta athari kiafya kama mapafu kushindwa kufanya kazi ghafla, saratani ya mapafu, mapafu kusinyaa na wakati mwingine kifo cha ghafla.
Dk Kirima anataja athari nyingine ni kuharibika kwa kinga za njia ya hewa, ikiwamo vimelea vidogovidogo vinavyojulikana kama ‘siria’ vilivyopo katika njia ya mfumo wa hewa, hivyo kupata bakteria na virusi vinavyoathiri mfumo mzima wa upumuaji.
“Matumizi ya gundi kwa kunusa ni hatari kutokana na kemikali nyingi zilizopo, hivyo huweza kusababisha saratani ya mapafu, kifo cha ghafla na kuharibu mfumo wa hewa,” anasema Dk Kirima.
Anasema hatua za kuchukua kuepuka athari hizo, hasa kwa mafundi wanatakiwa watumie barakoa au vifaa maalumu.
Kwa waathirika wa gundi, anasema wanatakiwa kufika katika vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi na kupatiwa matibabu ili kuzuia madhara zaidi.
Pia anashauri kampuni zinazotengeneza bidhaa hizo kutoa elimu kuhusu matumizi ili kuepusha madhara zaidi.
Imeandaliwa kwa msaada wa Bill and Melinda Gates