Veta yadhihirisha uwezo wake kwa watu wasioona

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Watu wasioona sasa wanaweza kupata ujuzi katika fani ya ufundi alluminiam na nyingine zinazotolewa na vyuo vya Veta kutokana kuwapo kwa maarifa yanayowawezesha kujifunza kirahisi.

Raphael Mwambalaswa (39) asiyeona ambaye anaonekana kwenye banda la Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) amedhihirisha kwamba kujifunza ufundi alluminiam kwa watu wasioona inawezekana.

Mwambalaswa ambaye pia ni Mhadhiri Msaidizi Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) katika Fani ya Saikolojia ya Elimu na Mitaala, anafanya utafiti kujua namna watu wasioona wanavyoweza kupata ujuzi kupitia ufundi stadi.

Amesema kunahitajika mtaala ambao utampa ujuzi mtu asiyeona ili aweze kujitegemea.

“Niliona Veta wanaweza kumsaidia mwanafunzi asiyeona kujitegemea ndiyo maana nilichagua kuja kusoma mafunzo ya ‘alluminium’ ili kufanya utafiti wangu uwe kivitendo zaidi usiwe wa nadharia.

“Mtu asiyeona anaweza akapata taaluma kupitia masomo mbalimbali kama uraia, jografia, sayansi lakini kushindwa kuona, masomo hayo hayawezi kumfanya awe mtu mwenye uwezo wa kujitegemea hivyo, anahitaji kitu cha ziada,” amesema Mwambalaswa.

Hata hivyo amesema kuna changamoto mbalimbali ikiwemo ya miundombinu ya kufundishia kwani mingine si rafiki kwa watu wenye ulemavu hasa wasioona.

“Mfano hii (anamuonyesha mwandishi wa habari) inaitwa ‘Folding ruler’ ukiitazama utaona kama ni ya kawaida ina namba ambazo mimi siwezi kuziona, lakini kile ninachokiona huwezi kukiona pia. Ina mistari ambayo mimi nagusa kwa kidole, kwahiyo naweza kuhesabu sentimita kama ziko tatu au nne, kuna alama ambayo imewekwa kunionyesha kwamba kuna sentimita 20.

“Huu ni ujuzi ambao mwalimu anayenifundisha ameutumia kutengeneza hii rula, mwalimu mwingine ambaye hakuwa na utayari wa kumfundisha mwanafunzi asiyeona asingeweza kwa sababu haikutengenezwa kwa mwanafunzi asiyeona,” amesema.

Mkufunzi katika Fani ya Useremala Chuo cha Veta Dar es Salaam, Salehe Omary, amesema awali hawakuwa na mwanafunzi asiyeona lakini kupitia maarifa na ujuzi walionao wametengeneza vifaa mbalimbali kikiwemo kipimo cha rula ili kumwezesha mwanafunzi huyo kujifunza kirahisi.

“Moja ya majukumu yetu ni kuhakikisha kila mtu anapata ujuzi, awe mwenye uwezo wa viungo au asiye na viungo, nimepata mafunzo ya kuwahudumia watu wenye mahitaji maalumu. Changamoto aliyonayo mwanafunzi wangu Mwambalaswa kwangu ilikuwa ni kitu kipya lakini kwa sababu nina utayari haikuwa shida, mwanafunzi wangu pia alitumika kama mwalimu kwa kunipa mbinu za kumfundisha, zimetufanya mimi na yeye kazi yetu kuwa rahisi,” amesema Omary.

Amesema pia matumizi ya kompyuta yamerahisisha ufundishaji kwa sababu anatumia ufahamu wake wa kompyuta kumfundisha kuandika.

“Kama wenye changamoto ya viungo wanaweza kujifunza na kufanikiwa kwanini wenye viungo wasifanye hivyo…natoa wito kwa wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu wawalete Veta ndiyo suluhisho, inaweza ikawapa cha kufanya wasiwe tegemezi, wasiwe ombaomba,” amesema Mwalimu Omary.

Related Posts