Watanzania tumieni fursa ya Maonesho ya 48 ya Saba saba

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ametoa wito kwa Watanzania kushiriki maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) ya mwaka huu ili kujifunza na kubadilishana uzoefu na washiriki wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza Julai 2, 2024 mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali ya Maonesho hayo, akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Mhe.Balozi John Stephen Simbachawene, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara wa Wizara Bw. Sempeho Manongi na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania Bi Latifa Mohamed.

Aidha, Dkt. Kijaji amesema Maonesho hayo yamekuwa mfano wa kuigwa kwa sababu yamekidhi viwango vya kimataifa kwa sababu waonyeshaji kutoka nje ya nchi wameongezeka tofauti na ilivyokuwa awali.

Aidha, amebainisha kuwa Maonesho hayo yanatoa fursa mbalimbali kwa Watanzania kujifunza kutoka kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ambapo nchi 26 zimeshiriki maonesho hayo ambazo zitaonyesha bidhaa zao mbalimbali.

” Nchi hii ni ya viwanda hivyo kwenye Maonesho hayo kuna viwanda vingi vimeshiriki lengo ni kubadilishana uzoefu”. Amesema Dkt. Kijqji.

Vilevile, amebainisha kuwa Maonesho hayo yatafunguliwa Julai 3, 2024 na Marais wawili ambao ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Filipe Nyusi ambaye ndio Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Maonesho hayo.

Related Posts