Na. Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imesema itaendelea kuwahudumia wananchi na kuhakikisha wanapata huduma bora na kwa wakati unaotakiwa kwa lengo la kuwaletea maendeleo na Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa tarehe 03 Julai, 2024 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati alipotembelea banda jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizopo chini yake katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (SABASABA) ili kujionea jinsi watumishi wa ofisi hiyo wanavyotoa huduma kwa wananchi na wadau kwa ujumla.
Akiwa katika banda la ofisi hiyo Waziri Mhagama amepongeza huduma zinazoendelea kutolewa pamoja na elimu juu ya shughuli zinazotekelezwa na ofisi yake huku akiwasihi watumishi wa ofisi hiyo kuzingatia weledi, ufanisi, huduma nzuri na kuzingatia misingi ya utumishi wa umma wawapo katika utekelezaji wa majukumu hayo.
“Tuendelee kuwahudumia wananchi, na tumeamua kuwafikia kwa karibu kupitia maonesho haya hivyo tunawakaribisha wananchi wote kuendelea kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu, tumejiandaa vizuri kuwa hudumia,” alisema Waziri Mhagama.
Aidha alitumia nafasi hiyo kueleza juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha diplomasia na kuimarisha sekta zote nchini katika kuhakikisha nchi inajipatia maendeleo zaidi.
“Mhe. Rais ameendelea kuwa kinara na mpambanaji kwa ajili ya Wananchi wote na niwahakikishie kuwa mama yupo kazini na ameendelea kusimamia sekta zote na kuhakikisha miradi yote ya kimkakati inaimarika ili kujiletea maendeleo yetu,” alisema Mhe. Mhagama
Katika Maonesho hayo Waziri Mhagama aliambatana na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bi. Zuhura Yunus pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizopo chini ya Ofisi hiyo.
Maonesho hayo ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Tanzania: Mahali Sahihi Pa Biashara na Uwekezaji,”.