Nyota Lille awafuata Ronaldo, Messi wapya Bongo

NILETEENI wachezaji wa maana’. Ndivyo alivyoagiza mchezaji wa zamani wa Lille ya Ufaransa, Souleymane Youla ambaye Juni mwaka huu, atatua nchini akiongoza jopo la maskauti kutoka barani Ulaya kwa kazi moja tu kuhakikisha wanaondoka na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wapya kutoka Tanzania.

Youle ambaye kwa sasa amejikita katika kutafuta vipaji huku akifanya kazi kwa ukaribu na klabu mbalimbali kubwa ambazo alizichezea ikiwemo Lille ya Ufaransa, Lokeren na Anderlecht za Ubelgiji na Besiktas ya Uturuki, anatambua kuwa Tanzania ni nchi ya mpira, hivyo anategemea kupata wachezaji ambao wanaweza kufanya makubwa kwa miaka michache ijayo.

Kwa nini Ronaldo na Messi? Nyota huyo anafafanua kwa kusema: “Sote tunajua kile ambacho wachezaji hao wamefanya kwa zaidi ya miaka 10 na bado pamoja na umri wao kusogea wanaendelea kufanya vizuri, Afrika tumebarikiwa kuwa na wachezaji wenye vipaji sana, lakini vimekosa malezi ya msingi bora ndio maana nimesema nataka Messi na Ronaldo wapya kutoka Tanzania, tukawaendeleze.”

Youle ambaye makazi yake kwa sasa ni Uturuki, licha ya kwamba alizaliwa Conakry, Guinea miaka 42 iliyopita, anadai kuifahamu Tanzania kutokana na kufanya vizuri kwa nahodha wake, Mbwana Samatta katika Ligi ya Ubelgiji ambayo amekuwa akiifuatilia kutokana na kuanza hapo safari yake ya kucheza soka la kulipwa kabla ya kwenda Ufaransa.

“Nilianza rasmi kucheza soka la kulipwa Ubelgiji, ni moja kati ya ligi ambazo nimekuwa nikizifuatilia, kuna kipindi Samatta alicheza huko na niliona kile ambacho alikuwa akikifanya akiwa na Genk, ndio maana sikuona tatizo niliposhirikishwa mpango wa kuja Tanzania kutafuta vipaji.

“Ninashauku ya kukutana na wachezaji wa Kitanzania na kuona kwa namna gani ninaweza kushiriki katika mpango wa kuwaendeleza, natamani kuwa sehemu ya ukuaji wa vijana ambao baadaye wanaweza kuitikisa Afrika na dunia, kama Messi na Ronaldo wameweza, kwa nini ishindikane kwa mchezaji wa Kiafrika au kutoka Tanzania,” anasema na kuongeza;

“Nimezunguka mataifa mengi na kuona vipaji vingi ndio maana nadiriki kusema Afrika tumebarikiwa, ukitazama kile ambacho walifanya kina Jay-Jay Okocha, Samuel Eto’o, Didier Drogba unaweza kukubaliana na mimi na hata Mohamed Salah na Sadio Mane, tunachotakiwa kufanya ni kuzalisha idadi kubwa tu ya wachezaji.”

Youle alikuwa sehemu ya Timu ya Taifa ya Guinea katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2004, ikimaliza nafasi ya pili katika kundi lao na kutinga hatua ya robo fainali, kabla ya kutolewa na Mali kwa mabao 2-1.

Nyota huyo pamoja na maskauti wengine kutoka Ulaya, wanaletwa nchini na Taasisi ya Kulea na Kuendeleza Vipaji vya Vijana (AYE) ambayo kila mwaka imekuwa ikifanya hivyo na kuzunguka mikoa mbalimbali kwa ajili ya kusaka vipaji, hivyo vya vijana ambao wapo mitaani na kuwashika mkono kuzifuata ndoto zao.

Akiongelea ujio wa Youle na namna walivyojiandaa na mchakato wa kusaka vipaji vya mastaa wajao kwa Tanzania, mkurugenzi Mtendaji wa AYE, Gerald Muyimba amesema tayari wameanza kufanya mawasiliano na wadau wao ikiwa ni pamoja na Serikali kwa ajili ya kuwasapoti katika mchakato huo.

“Malengo yetu makubwa ni kusaidia, hatupo hapa kwa ajili ya kunufaika, tulikaa na wenzangu na kuona ni skauti gani anafaa kuja nchini kwa awamu hii, ndipo tulipoona kuwa Youle anafaa (skauti mkuu) na kwa bahati nzuri amecheza soka katika kiwango cha juu, anaweza kutusaidia katika uvumbuji wa vipaji.

“Sio kwamba atakuwa peke yake, hapana, ataongozana na wengine ambao majina yao tutayaweka wazi hapo baadaye, nitoe wito kwa wazazi kuhamasisha vijana wao kwa sababu wakifanikiwa wanaweza baadaye kuwa msaada katika familia,” anasema na kumtolea mfano Shafii Omary Lumambo.

“Shafii ni kati ya vijana ambao walitoka mtaani na sasa wanafanya vizuri, pengine huenda msimu ujao akapiga hatua zaidi maana amekuwa akifuatiliwa na Besiktas huko Uturuki ambako anaichezea Tuzlaspor.”

Youla alianza kucheza soka la kulipwa Ubelgiji 1999, wakati Lokeren alipomsajili kuchukua nafasi ya straika mwenye mwili jumba, Jan Koller, ambaye alikuwa amehamia Anderlecht. Mshambuliaji huyo alifunga mabao tisa katika mechi 14.

Kiwango alichokionyesha akiwa na Lokeren kiliifanya Anderlecht kumsajili. Akiwa Anderlecht, alikabiliwa na ushindani mkali wa namba kutoka kwa Koller, Tomasz Radzinski, Aruna Dindane na Oleg Iachtchouk.

Alikuwa katika kikosi hicho kwa msimu mmoja pekee lakini anakumbukwa na mashabiki wa Anderlecht kwa bao lake la ushindi dakika za majeruhi dhidi ya PSV Eindhoven katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2000-01, ambalo liliifanya timu hiyo kutinga hatua ya 16 kama washindi wa kundi.

Youla alihamia Uturuki ambako alisajiliwa na Geclerbirligi SK na kucheza misimu mitano kama mchezaji wa kikosi cha kwanza. Baadaye akasajiliwa na Besiktas J.K, akapata muda mfupi zaidi wa kucheza, hivyo ikabidi atolewe kwa mkopo msimu mmoja kwenda FC Metz ya Ufaransa kabla ya kutua Lille.

Baada ya msimu mmoja, alitolewa tena kwa mkopo katika Klabu ya Uturuki ya Eskisehrspor ambako alishirikiana na Umit Karan na kuifanya timu hiyo kuwa na safu kali ya ushambuliaji kwa wakati huo.

Msimu uliofuata, alisajiliwa na timu hiyo moja kwa moja. Baadaye, Youla alifurahia misimu miwili zaidi nchini Uturuki.

Related Posts