Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema Tanzania iko salama na vitendo vya utekaji havipaswi kukaliwa kimya, akirejea chapisho la gazeti la Mwananchi la Julai 2, 2024 lililokuwa na kichwa cha habari: Nani mtekaji?
Masauni amesema hayo leo Jumatano Julai 3, 2024 aliposhiriki uzinduzi wa kitabu cha mmomonyoko wa maadili nani alaumiwe? kilichotungwa na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir katika Msikiti wa Mohammed wa Sita uliopo Kinondoni, jijini hapa.
“Baadhi ya wanasiasa wanaufanyia siasa uhalifu huu wa utekaji, nadhani mmesoma gazeti moja la Mwananchi limeandikwa utekwaji, taharuki kubwa inazushwa katika jamii, kwamba Tanzania kuna kutekwa tekwa hovyo, tena kunasibishwa na vyombo vyenye dhamana ya kulinda watu au Serikali. Nihakikishe tu Tanzania iko salama,” amesema Waziri Masauni.
Masauni amesema kuanzia Januari mwaka huu hadi leo Jumatano, Julai 3, 2024 kuna matukio takribani manane yanayohusu uhalifu yanayosemekana ya watu kutekwa.
Waziri Masauni amejitokeza kuzungumzia matukio hayo siku moja baada ya gazeti na tovuti ya Mwananchi kuripoti habari kwa kina juu ya kuanza kurejea kwa matukio ya watu kudaiwa kutekwa.
Msingi wa habari hiyo ilikuwa matukio mawili ya watu kudaiwa kutekwa. La kwanza ni la Mkazi wa Mbezi, jijini Dar es Salaam, Edgar Mwakabela maarufu kama Sativa aliyetoweka Juni 23 na kupatikana Juni 27 porini katika Hifadhi ya Katavi, akiwa na majeraha mwilini.
Kwa sasa Sativa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan, jijini Dar es Salaam.
Tukio la pili linamuhusu Kombo Mbwana, mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga aliyetoweka Juni 29, mwaka huu na hadi sasa hajaonekana.
Kombo alitoweka baada ya kufuatwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake, waliomchukua kwa nguvu kwa mujibu wa mama yake, Hellena Joseph. Mpaka sasa hajapatikana.
Masauni ataja matukio ya utekaji
Waziri Masauni akizungumzia sakata hilo ametaja matukio akisema: “Juni 24, 2024 jijini Dar es Salaam mtuhumiwa aliteka msichana na kumbaka, mtuhumiwa huyo ameshapatikana.
“Jingine lilitokea Katavi linahusiana na migogoro ya ardhi, watuhumiwa wanne kesi yao iko mahakamani, Juni 17, huko Muleba Kagera kuna mtoto alitekwa ana ulemavu wa ualbino, akapatikana amekufa hivi sasa watuhumiwa tisa na vidhibiti wamekamatwa na kesi ipo mahakamani,” amesema.
“Juni 24, Geita kuna mtoto alitekwa na walipigiwa simu wazee wake, ili ilipwe fedha mtoto na mtuhumiwa wamepatikana. Pia, Februari 12, huko Handeni pamoja na Mei 15, Mbeya kesi za kuteka nyara, ili kujipatia kipato watuhumiwa wote wamepatikana,” amesema.
Mei 29, amesema huko Geita kuna tukio watuhumiwa wanaendelea kusakwa na uchunguzi unaendelea.
“Mwisho hapa juzi kuna mtu alisemekana ametekwa (Sativa) na kwa sasa yuko Aga Khan hospitali, kwa sasa Serikali inaendelea na uchunguzi,” amesema Masauni.
Waziri huyo amesema Serikali inachukua hatua na hao waliopatikana kwa uthibitisho na inaendelea kuwasaka ambao hawajapatikana.
“Vyombo vinaendelea kuwatafuta kwa kuwa vina uwezo wa kuwakamata,” amesema.
Amesema uhalifu umepungua tangu Julai 2023 hadi Aprili 2024 kwa asilimia tano kutokana na polisi kuwezeshwa kuwa na mifumo ya kisasa.
Amesema jukumu la Serikali ni kuhakikisha usalama wa wananchi, hivyo amewatoa hofu kwamba hali ya usalama nchini iko salama.
“Usalama wa jamii maana yake tunapambana na aina zote za uhalifu na hata suala la mmomonyoko wa maadili hatuwezi kutenganisha na uhalifu,” amesema.