Wananchi wanavyombana Waziri Aweso uhaba wa maji Dar

Dar es Salaam. Wakazi wa Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam wamesema Serikali haiwezi kukwepa lawama ya kuwakosesha huduma ya majisafi, kwani moja ya jukumu lake ni kulinda usalama wao kwa kuwasogezea huduma muhimu.

Hata hivyo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amekubali hoja hiyo kwa kuwaomba msamaha, huku akieleza katika kukabiliana na ukubwa wa tatizo hilo, watafanya mambo mawili kwanza kuchukua hatua za dharura, ili wananchi wapate maji.

“Pili, tumeanza kuchukua hatua za kinidhamu kwa watendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao. Tumeanza kutekeleza hilo kwa sababu ukicheka na nyegele anayetambaa kwenye magoti atakung’ata pabaya,” amesema Aweso.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiwa katika mtambo wa  kuzalisha maji Ruvu chini. Picha na Mpiga Picha Wetu

Pia amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri kuhamishia ofisi yake kwa muda jijini Dar es Salaam kutoka Dodoma katika kuhakikisha wanasimamia pamoja wananchi wapate huduma.

Wakati akieleza hayo, tayari waziri huyo ameshawaweka kando viongozi watano, akiwemo Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Kiula Kingu, Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Huduma ya Maji, Shaban Mkwanywe.

Wengine ni Meneja wa Dawasa-Kinyerezi, Burton Mwalupaso, Mhandisi wa Kibamba, Regan Masami na kumuondoa kwenye nafasi yake Meneja wa Dawasa-Kibamba, Elizabeth Senkele, wote kwa madai ya kushindwa kuwajibika.

Katika maelezo yake akiwa tenki la Kibamba, waziri huyo amesema: “Uzembe, hujuma kwa baadhi ya watu kutokuwa na nia njema, kutotimiza wajibu wao, tutakwenda na watu wanaotaka kufanya kazi. Wasiofanya kazi tutawachukulia hatua.”

Waziri Aweso amechukua uamuzi huo katika ziara zake zinazoendelea Dar es Salaam na Pwani, mikoa inayohudumiwa na Dawasa. Anazungumza na wananchi wanaowasilisha kero zao, kukagua vyanzo vya maji na matenki ya kuyahifadhi maji maeneo mbalimbali.

Amefanya ziara hiyo takribani wiki moja imepita tangu Mwananchi Digital iliripoti hali ya upatikanaji wa maji Dar es Salaam.

Habari hiyo ya uchunguzi iliangazia jinsi baadhi ya wakazi za jiji hilo wanavyopata adha ya upatikanaji wa huduma hiyo. Mathalani eneo la Msumi, Kata ya Mbezi wanalazimika kutumia saruji kuyasafisha, ili kuwawezesha kuyatumia.

Kadhia hiyo ilimfanya Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew kufanya ziara Machi 20, 2024 maeneo mbalimbali kujionea hali halisi ya upatikanaji wa maji akieleza ameagizwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wakati mzigo wa lawama wakishushiwa watendaji, mameneja wa kimkoa wa kihuduma wa Dawasa wanawachongea watendaji wa makao makuu kwamba baadhi ya shughuli zao zinahitaji rasilimali fedha wanazotegemea kupata kutoka makao makuu.

Meneja mkoa wa kihuduma Makongo, Mkashida Kavishe alipoulizwa na Waziri Aweso inakuwaje watu hawaunganishiwi maji, alijibu changamoto inayowakuta ni uhaba wa vifaa.

“Nimetuma bajeti ya fedha tangu mwaka wa fedha uliopita hadi sasa hatujakubaliwa, ndio sababu ya kushindwa kuwaunganishia wananchi kwa wakati kama sheria inavyotaka mteja akilipia ndani ya siku saba anapaswa kuunganishiwa,” amesema.

Majibu hayo yalifanana na Meneja wa Kibamba, Elizabeth Sankere ambaye jana Jumanne aliondolewa katika nafasi hiyo, kwani alipoulizwa alisema ukosefu wa vifaa na utaratibu ulivyo wanapelekewa na makao makuu.

“Tunachokifanya ni kuwaandikia bajeti pekee kulingana na mahitaji ya vifaa tunavyohitaji,” alisema.

Wananchi walifunguka kwa kumuhoji Waziri jana Jumanne kwenye mikutano iliyofanywa katika mikoa ya kihuduma ya Dawasa katika maeneo yanayolalamikiwa.

Katika mikutano minne aliyofanya, Kibululu, Mbezi Luis, Malamba Mawili, Saranga, wananchi walisema Serikali haina mpango wa kuwasogezea huduma hiyo na badala yake wamewapa nguvu mawakala wa kuuza maji kwa maboza.

“Waziri gharama za maisha yetu imekuwa ikipanda kila uchwao, kwa kuwa fedha nyingi tunatumia kununua maji. Mfano, boza la lita 1,000 tunauziwa hadi Sh12,000 unaweza kutumia kwa wiki kwa kujibana kwa mwenye familia,” amesema mkazi wa Malamba Mawili, Helina Msuya.

Amesema kwa wale wanaonunua kwa ndoo za ujazo wa lita 20 wanauziwa kuanzia Sh250 hadi Sh500, gharama ambayo ni kubwa hawawezi kumudu, kwani kiwango hicho ni kikubwa kwa kuzingatia vipato vyao.

Hoja kama hiyo imezungumzwa pia na mkazi wa mtaa Mpya, Kata ya Makongo, Bernad Mapalala amesema kwa sasa hawafanyi maendeleo kwa sababu wanatumia fedha nyingi kununua maji kwenye maboza, baada ya kukosa huduma ya Dawasa.

“Tunajua ni hujuma zinaendelea tumepitiwa na miundombinu ya maji, lakini hayatoki. Waziri kuna watu wanatuuzia huduma hii kwa bei ghali, boza moja la lita 1,000 ni Sh12,000 hadi Sh 13,000 kwa matumizi ya nyumbani,” amesema.

Akionekana kwenye hasira, Mapalala amesema wanachoamini wanafanyiwa hujuma na viongozi wa Dawasa kwa kukubalina na wauza maboza wafanye biashara.

“Tunashauri kiongozi wetu safisha viongozi hawa, tuletee wengine wananchi wapate huduma,” amesema.

Mkazi wa Msumi, Moses Mussa amesema wanajiona kama wametengwa kihuduma, kwanza hata miundombinu hawajafikishiwa na wanatumia maji ya chumvi.

“Tumeahidiwa kuchimbiwa visima vitatu sijajua itakuwaje kwa sababu tuliambiwa maji yetu yana madini, lakini shauku yetu waziri tupate maji ya bomba, ” amesema.

Amesema wananchi wengi wako hatarini kupata magonjwa kwa sababu maji wanayotumia ni machafu na wanalazimika kutumia saruji kuyasafisha.

Mkazi wa Msakuzi, John Ndunguru amesimulia namna walivyokodi Coaster, ili iwapeleke Dawasa Makongo kuhoji inakuwaje wanazungukwa na matenki ya maji, lakini hawapati huduma hiyo.

“Isingekuwa mwenyekiti wetu wa mtaa kututaka tutumie busara tusifanye hivyo, tulitaka kwenda kuhoji haiwezekani tumefikishiwa miundombinu ya maji, lakini hatuoni huduma ikija,” amesema John.

Diwani wa Mbezi, Isimail Mangata amempigia magoti Waziri Aweso katika mkutano uliofanyika Mbezi Luis akimtaka kutumia ushawishi wake kuwapatia huduma ya maji wananchi wake, huku akieleza amechoka kutukanwa kila uchwao.

Diwani Isimail amesema miundombinu ipo, lakini kama kiongozi anakosa majibu ya kuwapa wananchi wake.

“Tafadhari Waziri naomba fanya utakavyofanya, tupatie maji itakuwa furaha, wataacha tabia ya kunitukana kila siku, wananchi wote unaowaona hapa shida yao ni maji,” amesema.

Mkazi wa Mbezi, Samson Tambi amesema kwa wiki anatumia Sh60,000 kununua maji kwenye maboza.

“Hatuna maji, UTI nyingi huku Mbezi, waziri utakuwaje na urafiki na kiongozi uliyemchagua na anapaswa kusaidia kutatua changamoto,” amesema.

Kwa upande wake, Anna Kajigili amesema katika mtaa wao wa River View wana miezi mitatu sasa hawana maji ya Dawasa, lakini wanashangaa kila mwezi wanatumiwa bili.

“Waziri inakuwaje hatupati maji, lakini tunaletewa bili za maji kila mwezi zinatoka wapi? Hii changamoto inatutesa na kutuondolea furaha ya kuishi. Tunaomba majibu kabla hujaondoka,” amesema.

Kwa upande wake, Diwani wa Goba, Ether Ndoha amesema licha ya changamoto hizo, Dawasa wana shida ya kutunza nyaraka za wananchi wanaomba kuunganishiwa huduma hiyo.

“Wameomba wananchi wengi kuunganishiwa maji, lakini hakuna kinachoendelea, wakifuatilia hawana taarifa wanaanza mchakato upya, wakati mwingine wanajibu hawana vifaa inakuwa shida,” amesema.

Amesema kata hiyo imezungukwa na matenki matatu ya maji, ikiwemo Chuo Kikuu cha Ardhi, Mshikamano na Kibamba, lakini huduma hiyo wanaisikia kwa majirani.

Waziri Aweso amesema hawatakuwa na urafiki na watendaji wasiowajibika, huku akieleza kinachoendelea anaamini ni hujuma na kutaka kuichonganisha Serikali kwa wananchi wake.

“Tutasafisha watendaji wote wazembe, na wanaojiona hawako tayari ni muhimu waseme mapema watupishe,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Aweso ametoa maagizo kwa watumishi wa Dawasa kuacha utamaduni wa kuwakatia maji wananchi siku za sikukuu, Jumamosi na Jumapili “wikiendi’.

“Kufanya tabia hiyo ni roho mbaya, ni marufuku mtumishi yeyote wa Dawasa kuwakatia huduma ya maji wananchi siku za sikukuu na wikiendi,” amesema.

Aweso amesema hata wananchi wanapaswa kutambua wajibu wao wa kulipa bili kwa wakati, ili kuisaidia taasisi hiyo kujiendesha, ikiwemo kuwalipa mishahara watendaji.

Related Posts