Polisi yawasaka waliyemuua anayedaiwa kushiriki wizi wa pikipiki

Babati. Jeshi la Polisi mkoani Manyara linawasaka waendesha pikipiki za kubeba abiria maarufu bodaboda mjini Babati, kwa tuhuma za kumuua kijana anayedaiwa kuhusika na njama za kuiba pikipiki.

Kijana huyo mwenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya miaka 20 hadi 25, alifariki dunia baada ya kupigwa na kuchomwa moto na madereva bodaboda, baada ya kudaiwa kushiriki wizi wa pikipiki akiwa na wenzake wawili waliofanikiwa kutoroka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, George Katabazi akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Julai 3, 2024 ofisini kwake amesema wanawasaka bodaboda wote waliohusika na mauaji hayo.

Amesema tukio hilo lilitokea Jumatatu Julai Mosi, 2024, saa 6:30 mchana katika Mtaa wa Wang’warai, Kata ya Babati, kijana aliyeuawa anadaiwa kula njama za kuiba pikipiki ya dereva aliyemkodi.

Hata hivyo, Kamanda Katabazi amesema si jambo jema kwa watu kujichukulia sheria mkononi wakati vipo vyombo vya dola.

“Nawakumbusha wakazi wa mkoa huu wa Manyara, hakuna mtu aliyepo juu ya sheria, kama kuna jambo ni vyema mkatoa taarifa kwa polisi ili wachukue hatua zinazofaa badala ya kujichukulia sheria mkononi,” amesema Katabazi.

Amesema kama mtu huyo angekamatwa na kufikishwa kituo cha polisi, jeshi hilo lingefanya kazi ya kumuhoji kwa lengo la kuupata mtandao mzima wa wezi hao wa pikipiki.

Lakini amesema jeshi hilo linaendelea na operesheni ya kuwakamata watu wanaomiliki mali za wizi, zikiwamo pikipiki.

Amesema; “Raia wema wanapaswa kuendelea kutoa ushirikiano kwa polisi kwa kutoa taarifa za wizi ambazo tutazichukulia hatua mara moja.”

Baadhi ya wakazi wa Babati wamesema si jambo jema kuwaua wezi kwa sababu huko hakutibu tatizo na wengine wameenda mbali zaidi na kusema baadhi huuawa wakati siyo wahusika wa tukio na kunachangia pia kupoteza ushahidi.

Ismail Bomboo, mkazi wa Kitongoji cha Wang’waray, amesema tukio la watu kujichukulia sheria mkononi mbali ya kupoteza ushahidi, pia linawaathiri watu wasiohusika. “Japokuwa wanasema marehemu alikuwa anatumiana SMS na wezi wenzake, huo ni  ushahidi mzuri angepelekwa polisi labda angewataja aliokuwa anawatumia hizo meseji,” amesema Bomboo.

Lakini ametoa angalizo kwa Jeshi la Polisi lianze kujitathimini na kujihoji kwa nini watu wanafikai hatua ya kuchukua sheria mkononi.

“Mfano hapa kwetu kuna watu wnafanya makossa, ukiwashtaki polisi wanakaa ndani siku chache halafu tunakuja kukutana nao mitaani anadunda tu, huenda hii nayo ni sababu,” amesema Mwananchi huyo.

Mbunge mstaafu wa Babati Vijijini, Vrajlal Jitison amesema tukio la mtu asiyehusika na wizi kuuawa lilishawahi kutokea Kijiji cha Mapea, Kata ya Magugu.

Anasema mtu huyo aliuliwa kwa kudaiwa kuwa mwizi, lakini wahusika walioibiwa wakaja kusema aliyeuawa si aliyewaibia kwa sababu walikuwa wanamfahamu aliyewaibia.

“Kwa hiyo wananchi tunapaswa kuwa makini sana, tunajiingiza kwenye kesi zisizotuhusu,” amesema Jitison.

Related Posts