Simba yafuata mrithi wa Saido Asec

BAADA ya kipigo cha mabao 2-1, wekundu wa Msimbazi Simba wameamua kuingia sokoni kusaka mashine mpya na sasa iko mezani na kiungo mshambuliaji wa ASEC Mimosas Pokou Serge.

Mwanaspoti linajua Simba inataka huduma ya kiungo huyo kiraka ili aje kufanya mambo mawili kutumika kama winga wa kushoto, pia kama kiungo mshambuliaji nyuma ya mshambuliaji wa mwisho.

Hesabu hizi kama zikienda sawa ina maana Simba inafanya maamuzi ya kumsaka mrithi wa mkongwe Said Ntibazonkiza ‘Saido’ ambaye Mwanaspoti linafahamu mabosi wa klabu hiyo hawana mpango wa kumWongezea mkataba.

Hata hivyo, Simba italazimika kumpandia dau Pokou ambaye bado ana mkataba na Asec uliobakiza mwaka mmoja na lazima wekundu hao watalazimika kununua mkataba wake.

Simba imegundua imekosa watu wa maana eneo lao la kiungo na hata ushambuliaji na sasa inataka kuleta watu wa maana waliofanya vizuri mashindano ya Afrika msimu unaomalizika.
Mipango hiyo imewafanya wakatua kwa Pokou ambaye ni miongoni wa mastaa wenye rekodi nzuri za ushambuliaji akiwa na kikosi cha ASEC akiwa pia amewahi kuwatibulia Simba pale Benjamin Mkapa.

Kiungo huyo mshambuliaji anayetumia vizuri mguu wa kushoto aliifungia Asec bao pekee la kusawazisha akiitibulia Simba kushinda nyumbani dhidi ya Waaivory Coast hao dakika ya 77 akitumia asisti ya staa wao wa zamani Sankara Karamoko ambaye aliuzwa msimu huu huu.

Rekodi yake ya msimu huu ni kwamba Pokou amefunga mabao matatu na asisti moja kwenye ligi ya mabingwa akifungana na Karamoko kwa rekodi hizohizo lakini jamaa ndiye kinara wea mabao akiwa na asec kwenye ligi akiwa na mabao nane.

Mwanaspoti linafahamu tayari Simba imshamlainisha Pokou na kwamba mfupa mgumu pekee uliosalia ni wekundu hao kumaliza na wenzao wa Asec. Simba inataka kumaliza hesabu za usajili mapema kwa msimu ujao baada ya mabosi wa klabu hiyo kukunja uso kufuatia kiwango duni cha kikosi chao msimu huu ambacho kinaweza kuwa na uhakika wa kuchukua taji moja pekee la ngao ya jamii baada ya kupishana na mataji mengine matatu.

Kocha wa Asec Jullie Chevalier ameliambia Mwanaspoti kiungo huyo ameomba kuondoka mwisho wa msimu lakini bado hajajua wapi anakwenda ingawa klabu inayomtaka italazimika kuilipa Asec kutokana na bado yuko kwenye mkataba.

“Ameniambia (Pokou) anataka kuondoka mwisho wa msimu lakini sijajua kama ni Simba ndio weanataka kumsajili lakini bado watahitaji kuilipa Asec kwa kuwa huyu bado ana mkataba na unajua hii klabu haizuwii wachezaji kuondoka,” alisema Chevalier.

Related Posts