Mufti azindua kitabu chake – Mtanzania

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dk. Abubakar Zubeir, amezindua kitabu chake kiitwacho ‘Mmomonyoko wa Maadili Nani Alaumiwe?’, ambapo amesema kilichomsukuma kufanya hivyo ni hali ya kumomonyoka kwa maadili iliyopo kwa sasa nchini.

Kitabu hicho chenye sura saba kimezinduliwa leo Julai 3,2024, BAKWATA Makao Makuu, jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dk. Doto Biteko.

Sheikh Zuber amesema kila mmoja anahusika katika jukumu la kusimamia maadili kuanzia baba, mama, mtoto na jamii nzima na kitabu hicho kitasadia kuelewa wapi nchi napokwenda kimaadili.

“Kwa nini nimeita kitabu hiki Mmomonyoko wa Maadili Nani Alaumiwe? Ni kwamba kila mmoja ana katika suala la maadili, ikiwa ni baba, mama. mtoto. Zamani ilikuwa mtoto si wako peke yako, majirani, mtaa au kijiji walikuwa wanamfundisha mtoto. Ni zama ambazo zilijaa uadilifu maadili lakini sasa hivi yote yamepotea,” ameeleza Mufti.

Naye Dk. Biteko amebainisha kuwa Serikali itaendelea kusimamia na kukuza uadilifu wa maadili kama msingi wa maendeleo endelevu kupitia Sera na Sheria bora kwa kushirikisha wadau wa kidini, elimu, na jamii ili kuendeleza utamaduni ambapo maadili yatajumuishwa katika kila sehemu ya maisha ya watanzania.

Dk. Biteko ameiagiza Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kushirikisha wadau, kuhakikisha inahamasisha ushiriki wa familia katika malezi bora na ya kimaadili, kushiriki kikamilifu kulinda maadili katika jamii zetu kukuza uhusiano imara ndani ya familia na kukuza mafundisho ya maadili ndani ya kaya ili jamii itakuwa imara.

“Kwa kukuza misingi ya uaminifu, haki, uadilifu, uwajibikaji, umoja wa kijamii, na ustawi endelevu. tutahakikisha kuwa safari ya maendeleo ya Tanzania inabaki imara katika maadili yetu ya thamani, pamoja na mustakabali ambao vijana wetu watarithi Taifa lenye uadilifu na fursa,” amesema Dk. Biteko

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,Dk. Dorothy Gwajima, amesema wizara yake itatumia kitabu hicho kama rejea katika machapisho yanayolenga kukemea ukiukaji wa maadili nchini.

Related Posts