VUMBI na nyasi kutimka katika viwanja vya gofu vya Lugalo, ambavyo vitakuwa ni shuhuda wa miamba zaidi ya 150 watakaokuwa kuwania tuzo mbalimbali za mashindano ya wazi ya gofu yanayoanza kesho.
Yakija kwa jina rasmi la Lugalo Open, ni mashindano ya siku tatu yatakayowashirikisha wacheza gofu ya kulipwa (mapro) na wale wa ridhaa, kwa mujibu wa nahodha wa mchezo wa gofu wa klabu hiyo, Meja Japhet Masai.
Alisema wachezaji wa ridhaa watashiri kwa siku tatu mfulululizo kutoka Julai 5 hadi 7 katika mtanange ambao utachezwa katika mashimo 54.
Kwa kuwa ni mashindano ya wazi, Meja Masai alisema anategemea kupata washiriki kutoka klabu zote za gofu nchini.
Klabu zinazotegemewa kushiriki ni pamoja na Arusha Gymkhana, Dar es Salaam Gymkhana, Morogoro Gymkhana, Kili Golf na Mufindi.
Vodacom Tanzania ndiyo wadhamini wa mashindano ya mwaka huu, kwa mujibu wa Meja Masai.
Mmoja wachezaji wa kulipwa Daudi Helela kutoka klabu ya Lugalo, anaamini mashindano ya mwaka huu yatakuwa na ushindani mkubwa kutokana na zawadi nono zilizoandakliwa kwqa washindi wa vitengo mbalimbali.
“Nategemea kuona mchuano mkali kwa wachezaji wote wa ridhaa na wa kulipwa na huu ndiyo utamu hasa wa mchezo wa gofu,” alisema.
Akiongezea, Salum Dilunga ‘Ninja ambaye pia hucheza gofu ya kulipwa alisema yatakuwa ni mashindano ya jasho na damu katika vita kali ya kuwania ushindi na zawadi ya pesa nono.
“Lakini mimi niko imara na tayari kwa hayo yote,” alisema mchezaji huyo
Mashindano hayo ya siku tatu yameandaliwa na Chama cha Gofu Tanzania (TGU) kwa kushirikiana na klabu ya Lugalo ya jijini Dar es Salaam.
Siku zote tatu, kwa mujibu wa Meja Masai, yatakuwa yakichezwa kwa mfumo wa kuhesabu idadi ya mikwaju (stroke-play) na siyo wa kuhesabiwa pointi (stableford point).